“Natumia nafasi hii kueleza juu ya maneno ambayo yalitolewa na mchungaji fulani, sikumbuki anaitwa nani… nasema nimemsamehe kutoka ndani ya moyo wangu wote anaweza kuwa na sababu zake ila nimemsamehe kabisa” Kardinal Pengo
Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema, amemsamehe Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye hivi karibuni alimtolea maneno makali kutokana na kutofautiana naye juu ya msimamo wa viongozi wa Kikristo kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Kardinali Pengo alitoa msamaha huo mbele ya waumini katika Kanisa la St Joseph, Dar es Salaam jana, siku mbili baada ya Askofu Gwajima kuhojiwa na Polisi kwa madai ya kumkashifu kiongozi huyo, mbele ya hadhara.
Askofu Gwajima anadaiwa kutoa kauli za kumkashifu kiongozi huyo kwamba amewasaliti wa viongozi wenzake wa Kikristo kwa kuwataka waumini wa dini hiyo kuamua wenyewe suala la Katiba Inayopendekezwa kinyume na msimamo wa waraka wa kupinga katiba hiyo uliotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (CCT).
Baada ya kutolewa kwa waraka huo ulioagiza waumini kuipigia kura ya hapana katiba hiyo, Askofu Pengo alinukuliwa akisema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuzuia wananchi kuikubali Katiba hiyo huku akisisitiza waachiwe uhuru wao wa kuamua.
Akizungumza jana wakati wa ibada ya Jumapili ya Matawi, inayoadhimishwa wiki moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, Kardinali Pengo, bila ya kumtaja jina alisema: “Natumia nafasi hii kueleza juu ya maneno ambayo yalitolewa na mchungaji fulani, sikumbuki anaitwa nani… nasema nimemsamehe kutoka ndani ya moyo wangu wote, anaweza kuwa na sababu zake ila nimemsamehe kabisa.
“Sina ghadhabu wala chuki ila kinyume chake, naomba tumwombee yeye na watu wote waliokuwa wamehusika pengine nyuma yake ili Mungu aweze kutulinda na kutudumisha katika hali ya amani ya Taifa letu.”
Alisema hatua ya Polisi kumkamata ni sehemu ya kutekeleza utaratibu wa jeshi hilo tu, lakini yeye kwa nafsi yake ameshamsamehe.
Atolewa ICU, wafuasi wakamatwa
Katika hatua nyingine, Askofu Gwajima ametolewa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kuhamishwa katika wodi ya kawaida baada ya afya yake kuendelea vizuri.
Askofu huyo alikuwa ICU kwenye Hospitali ya TMJ, Mikocheni, alikofikishwa usiku wa Ijumaa baada ya hali yake kubadilika ghafla alipokuwa akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Askofu huyo alijisalimisha kituoni hapo akiitikia wito wa polisi uliomtaka kufanya hivyo kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Kardinali Pengo.
Akizungumza jana, mke wa Askofu huyo, Grace Gwajima alisema baada ya madaktari kumuona anaendelea vizuri, wameamua kumtoa ICU na kumpeleka kwenye wodi ya kawaida.
“Tunamshukuru Mungu sasa hivi anaendelea vizuri tofauti na alivyokuwa jana (juzi) alikuwa hawezi kula chakula na kuongea lakini sasa hivi anaongea na anakula chakula,” alisema na kuongeza:
“Tunashangazwa ni nini kimetokea Polisi wakati akihojiwa. Alitoka nyumbani akiwa mzima na ametolewa polisi akiwa amebebwa hajitambui.”
Mke wa Askofu huyo alisema wakiwa hospitalini hapo usiku wa kuamkia leo, walikuja askari polisi na kuwakamata baadhi ya viongozi na walinzi wa kanisa hilo na kuchukua magari yao.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema inawashikilia na kuwahoji watu 15 ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama pamoja na kujaribu kumtorosha Askofu Gwajima.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kamanda Kova alisema jana saa 9.30 usiku watu hao 15, katika hali isiyo ya kawaida walifika hospitalini hapo wakidai kwamba walikuwa wanataka kwenda kumuona mgonjwa huyo.
“Askari ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia shaka hivyo waliwakatalia kuingia. Kundi hilo la watu 15 lilijaribu kutumia nguvu kuingia katika chumba alicholazwa Askofu Gwajima lakini walikamatwa na kikosi maalumu cha Polisi ambacho kabla ya tukio hilo kilikuwa kinafuatilia mwenendo wa kundi hilo.”
Alisema baada ya kukamatwa, watuhumiwa hao walipekuliwa hapohapo TMJ na kukutwa na begi ambalo lilikuwa na vitu mbalimbali mojawapo vikiwa ni bastola aina ya Berreta ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za bunduki aina ya Shortgun, vitabu viwili vya hundi na hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Josephat Mathias.
Alisema baada ya upekuzi kukamilika, watuhumiwa walifikishwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa mahojiano zaidi ikiwa ni pamoja na kupata uhalali wa wao kumiliki silaha hizo na risasi.
“Upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni ya kubaini sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote zilizotumika kutaka kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment