Baadhi ya watoto 18 katika tukio la kwanza walikuwa wakihifadhiwa kwenye nyumba iliyopo Kata ya Pasua kwa lengo la kuwafundisha dini ya Kiislamu, mkoani Kilimanjaro. Picha ya Maktaba
Moshi. Mambo mazito zaidi yamezidi kubainika mkoani Kilimanjaro baada ya polisi kugundua nyumba nyingine yenye watoto kumi na mmoja waliokusanywa kutoka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kufundishwa dini.
Hii ni mara ya pili katika muda usiozidi wiki moja baada ya polisi kubaini nyumba iliyohifadhi watoto 18 kwa lengo kama hilo Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo linafanya wapelelezi kuumiza vichwa kwa kuwa mikoa waliyotoka ndio ile ile waliyotoka watoto 18 waliokutwa kwenye nyumba moja mjini Moshi.
Nyumba hiyo imebainika wakati kukiwa na madai kwamba baadhi ya misikiti katika maeneo ya Pasua, Njoro na Kibosho yanaendesha mafunzo ya judo na karate.
Kamanda Kamwela alieleza kuwa kama ilivyokuwa awali, watoto waliobainika juzi wanatoka katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Singida, Tabora na Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, watoto hao waligunduka katika nyumba iliyoko eneo la Lyamungo wilayani Hai. Alisema umri wao ni kati ya miaka 14 na 17 na walikuwa wanafundishwa dini na ushonaji.
Alisema kituo hicho ambacho hakijasajiliwa, kinaitwa Umm Sukhail na kinamilikiwa na mwalimu mstaafu, Abubakar Juma (64) mkazi wa Tanga ambaye kwa sasa anaishi maeneo ya Kibosho Mweka.
Kamwela alisema watoto hao wamechukuliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi ili kujua sababu za wao kuishi katika eneo hilo pia kubaini ukweli wa mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.
“Kutokana na kugundulika kwa mafunzo haya yasiyo rasmi yanayotolewa na walimu ambao pia si rasmi, lazima tuchunguze kama baada ya kuhitimu wanapewa vyeti na wanafanya kazi wapi,” alisema.
Kamwela pia alisema polisi wanafanya uchunguzi ili kubaini kama watoto hao walipata elimu ya msingi kama sheria inavyoelekeza na kama walifaulu ama la na kwanini hawakuendelea na masomo. Kamanda alisema upo uwezekano wa watoto 18 waliokutwa Pasua kuhamishiwa kituo cha Narumu na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kubaini kama wenye vituo hivyo wanafanya kazi pamoja.
Kuhusu watoto 18 wa Pasua, Kamanda Kamwela alisema wametambuliwa na wazazi wao na kuchukuliwa, lakini bado uchunguzi unaendelea kujua uhusiano wao na mmiliki wa nyumba hiyo.
“Tunachunguza kujua kama wazazi walikuwa wakifahamu maisha wanayoishi na sababu za kuwatoa kwenye shule za Serikali na kuwapeleka kwenye shule za dini wakati elimu ya msingi ni ya lazima,” alisema.
Pamoja na wazazi wo kudai waliridhia watoto wao kwenda kupatiwa masomo hayo, kamanda alisema uchunguzi umebaini watoto hao walikuwa wanaishi kwenye mazingira magumu kutokana na ufinyu wa eneo na hivyo hulazimika kulala chini.
“Upelelezi kuhusu tukio hili bado unaendelea kwa sababu kuna maswali mengi yanayohitaji majibu kwa kuwa watoto hawa bado ni wadogo na walitakiwa wawe wanasoma shule ya msingi,” alisema.
“Lakini wakawa wanaishi kwenye nyumba hii lazima tujue uhalali wa wao kuacha shule na kwenda kujifunza dini kwenye nyumba ambayo haijasajiliwa na nyumba ambayo huduma za kijamii sio rafiki.”
Kamanda alisema: “Elimu inayotolewa kwa siri ambayo hata Serikali haijui na majirani hawajui inatia shaka na ndio maana polisi wanafanya uchunguzi kujua ni siri gani imejificha.”
Kuhusu Jeshi la Polisi kuwa na taarifa ya kuwapo mafunzo ya judo na karate kwenye baadhi ya nyumba za ibada, alisema watachunguza madai hayo.
Inadaiwa mafunzo hayo hutolewa usiku katika baadhi maeneo ya Pasua, Njoro, Kibosho, na wilaya za Mwanga na Same.
Aprili mwaka jana, raia 20 wa Yemen walikutwa vichakani alfajiri wilayani Same na walipohojiwa na kiongozi mmoja wa kisiasa, walidai wamekuja kufundisha dini.
Habari zinadai miezi kadhaa iliyopita, polisi mjini Moshi walivamia msikiti mmoja uliopo Kibosho na kukuta vijana wadogo kutoka Singida, Babati na Kondoa wakifundishwa mbinu hizo za kupigana.
Katibu wa Baraza la Waislamu (Bakwata) wa Kilimanjaro, Rashid Mallya aliliambia gazeti hili juzi kuwa wamestushwa na wimbi hilo la watoto kuletwa mkoani hapa kwa mafunzo ambayo aliyaelezea kuwa hayafahamika.
“Tumeshtushwa na hatuliungi mkono hili kwa sababu maeneo ya kufundishia dini yetu yanajulikana na si nyumbani kwa mtu. Vyombo vyetu vichunguze jambo hili kwa uzito,”alisema.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment