Advertisements

Friday, March 6, 2015

WAZAZI WANA NAFASI GANI KATIKA KUKUCHAGULIA MKE/MUME?

Nianze kwa kumshukuru Jalali aliyenipa pumzi ya kuiona siku ya leo. Ni matumaini yangu kwamba na wewe msomaji wangu, umzima buheri wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku. Wewe ambaye afya inaleta matatizo, nakuombea upone haraka.

Je, upo kwenye uhusiano wa kimapenzi, unampenda sana mume, mke, mchumba au mpenzi uliyenaye lakini wazazi wako hawamkubali na matokeo yake wanakuchagulia mtu wa kuishi naye?

Mada ya leo ni kwa ajili ya wewe msomaji wangu ambaye upo kwenye mazingira kama haya, ya wazazi kumkataa umpendaye kwa sababu ambazo wanazijua wao. Kwa ambao wamewahi kupitia changamoto hii au bado wapo ndani yake, watakuwa wanaelewa vizuri ugumu uliopo linapokuja suala kama hili.

Wazazi wako wamekuzaa na kukulea tangu ukiwa mdogo mpaka umekuwa mkubwa, umempata umpendaye lakini wao wanamkataa na kukwambia unatakiwa kuchagua moja, wao (wazazi) au huyo unayempenda. Utachukua uamuzi gani? Utamuacha kwa sababu wazazi hawampendi? Utakubali kuwadharau wazazi wako na kuendelea naye?

Bila shaka kila mmoja atakuwa na jibu lake tofauti, lakini tunachokihitaji hapa, ni kujadiliana, kupanuana mawazo, kupeana uzoefu ili mwisho kila mmoja awe na uwezo wa kuivuka changamoto hii kwa sababu hata kama bado haijakukuta, huenda ipo siku na wewe yatakutokea.

MFANO HAI

Hebu soma ushuhuda wa msomaji wangu mmoja ambaye yupo kwenye hali mbaya na anahitaji ushauri:

“Mimi ni mwanaume mwenye umri wa miaka 42, nilioa miaka kumi iliyopita na tumejaliwa kupata watoto wawili. Tatizo linalonisumbua na kuniweka njia panda, wazazi wangu hawamkubali kabisa mke wangu badala yake kuna mwanamke mwingine ambaye ndiyo wao wanataka mimi nimuoe. Naomba ushauri, nifanyeje?”

Amehitimisha msomaji wangu huyu, bila shaka umemuelewa. Najua huyu ni mmoja tu lakini wapo wengi ambao wanatokewa na visa kama hivi. Naomba tujadiliane pamoja, ungekuwa ni wewe kwenye nafasi ya msomaji huyu, ungefanya nini? Kama ungepewa kazi ya kumshauri, ungemwambia nini?

TAFUTA CHANZO CHA TATIZO

Hakuna chuki ambayo huwa haina chanzo. Kama mumeo, mkeo anachukiwa na wazazi wako, jambo la kwanza ambalo unatakiwa kulijua, ni kwamba lazima kuna chanzo kilichosababisha hali hiyo. Na kama yalivyo matatizo mengine yote, huwezi kupata muafaka kama hujakijua chanzo.

Wengi hushindwa kutumia busara katika kutafuta chanzo. Yawezekana umpendaye ndiyo chanzo cha kuwafanya wazazi wako wasimkubali ila kwa sababu ya mapenzi yako kwake, unaukataa ukweli na kumtetea. Hutaweza kupata suluhu, matokeo yake utajikuta unawachukia wazazi wako mwenyewe.

Yawezekana pia wazazi wako ndiyo tatizo lakini kwa sababu ya malezi uliyopewa, huwezi kumkosoa mzazi wako. Mwingine atasema anaogopa laana ya wazazi kwa hiyo hata kama anajua tatizo linaanzia wapi, hatakuwa na uthubutu wa kulizungumza, matokeo yake, ataungana na wazazi wake mwisho ataachana na ampendaye na kwenda kuoa mwanamke asiyempenda.

Tukutane wiki ijayo kuangalia sehemu ya pili ya mada hii kujua nini unapaswa kufanya unapokutana na changamoto kama hii. Kama una maoni, ushauri au swali, nicheki kwa namba za hapo juu.

GPL

No comments: