Tulianza kuangalia namna ya kushughulikia tatizo hili inapotokea mwenzi wako anachukiwa na wazazi na wanakushinikiza uoe au uolewe na mtu ambaye wao ndiyo wanamtaka. Tuendelee kuanzia pale tulipoishia.
ZUNGUMZA NA KILA UPANDE
Baada ya kufuata hatua ya kwanza ambayo nilisema ni kutafuta chanzo cha tatizo, hatua ya pili ni kuzungumza na kila upande. Ukishakijua chanzo, anza kuzungumza na mwenzi wako, mueleze jinsi unavyojisikia vibaya kutokana na uhasama uliopo kati yake na wazazi wako na mueleze msimamo wako.
Baada ya hapo, hamia upande wa pili, zungumza na wazazi wako kwa heshima na uwaeleze jinsi unavyoumia kutokana na matatizo yanayoendelea kati yao na mwenzi wako. Kamwe usioneshe dharau kwao, zungumza nao kwa adabu huku ukiwapa heshima zote wanazostahili kisha waeleze msimamo wako.
Kama kuna jambo aliwahi kuwaudhi ndiyo maana hawamtaki na wanataka akawaombe msamaha, waahidi kwamba utasimamia hilo hadi litimie ila kama wanataka muachane, nadhani huo hautakuwa uamuzi sahihi, endelea kuzungumza nao mpaka muafaka upatikane.
WAPATANISHE
Baada ya kuwa umeshazungumza na pande zote mbili, andaa muda maalum ambao utawakutanisha wote, kama inawezekana unaweza pia kuwaita baadhi ya watu wachache unaowaamini kama washenga au viongozi wa dini waliofungisha ndoa yenu kisha kila mmoja azungumze dukuduku lake na mwisho, anayestahili kuomba radhi afanye hivyo.
Mpaka hapo tayari utakuwa umefanikisha kupatikana kwa suluhu, busara kubwa itumike kuwapatanisha ili mkimaliza kikao hicho cha suluhu, asiwepo ambaye bado atakuwa na dukuduku.
Baada ya kupatikana kwa suluhu, kuwa makini ili yale yaliyosababisha matatizo awali, yasijirudie tena kwa sababu wazazi wako hawawezi kumchukia tu mwenzi wako, lazima ipo sababu ambayo unapaswa kuhakikisha kuwa baada ya muafaka, haijirudii tena.Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.
GPL
No comments:
Post a Comment