Advertisements

Friday, March 20, 2015

Zitto: Mwisho ama mwanzo.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, jana alitangaza kujiuzulu ubunge kwa kusambaza waraka kwa vyombo vya habari.

Baadaye Zitto alikwenda bungeni katika kikao cha jioni kwa ajili ya kuwaaga wabunge wenzake na kuwaeleza sababu za uamuazi wake.

Hata hivyo, kabla ya kuwasili bungeni akisubiri kupewa fursa ya kuwaaga wabunge, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda amemzuia kuchukua uamuzi huo na kwamba yeye (Zitto) alikuwa akiendelea kumshawishi Spika.

ALIYOELEZA KATIKA WARAKA
Zitto alisema kwamba amejiuzulu rasmi wadhifa huo na kuahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo lake na Taifa kupitia jukwaa lingine atakalolitangaza hivi karibuni.

Aidha, Zitto aliwaaga wabunge akieleza hana nia ya kukata rufaa mahakamani kutetea uanachama wake na badala yake amesema anasubiri taratibu za kisheria na kikatiba kuondoka rasmi kwenye wadhifa wake wa ubunge.

Zitto aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akitoa maelezo binafsi kwa kutumia kifungu cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013 kinachosema: “Mbunge yeyote anaweza, kwa idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi Bungeni yanayolenga kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia jamii.”

Alisema pamoja na kwamba ameamua kuondoka Bungeni, ataendelea kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa wananchi wa kawaida bila ubaguzi.

SABABU ZA KUJIUZULU
Alisema kwa muda mrefu amekuwa kwenye msuguano wa kiuongozi kati yake na viongozi wenzake ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uliosababishwa na tofauti za kimtazamo ambazo ni chanzo cha Novemba 2013, avuliwe nyadhifa alizokuwa nazo ndani ya chama hicho ukiwamo Unaibu Katibu Mkuu.

Alisema hakuridhika na maamuzi hayo, hivyo alikata rufaa katika Baraza Kuu la Chadema kwa mujibu wa taratibu za kikatiba za chama hicho lakini Ofisi ya Katibu Mkuu haikumpa fursa hiyo.

“Na huo ndiyo ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya uanachama wangu hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika vikao vya chama. Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye Mahakama Kuu imetoa hukumu yake Machi 10, 2015. Katika hukumu hii, nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi letu liliwasilishwa kimakosa,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba hajaridhika na mwenendo wa kesi hiyo iliivyoamuliwa pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe, hatakata rufaa na kwamba anaheshimu maamuzi hayo ya Mahakama.

Hata hivyo, Zitto alisema kwa mujibu wa Katiba ya Chadema baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu ilipaswa kukaa na kumpa rasmi mashtaka yanayohusu uanachama wake, aitwe kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi wake, lakini imefanyika kinyume chake.

Alisema baada tu ya hukumu ya Mahakama Kuu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, aliitangazia dunia nzima kuwa Chadema imemvua Zitto uanachama kauli ambayo imekuwa ikirudiwa na viongozi waandamizi wa chama hicho mara kwa mara.

“Baada ya hapo viongozi wangu wametoa matamko mbalimbali yote yakionyesha kwamba sitakiwi tena katika chama hiki, pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo (jana) sijawahi kukabidhiwa barua yoyote inayonitaarifu kufukuzwa kwangu katika chama…kutokana na maelezo ya hapo juu, ni wazi kwamba uanachama wangu wa kisiasa ndani ya Chadema umeshaondolewa,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Ninaweza kuendelea kupigania uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na misingi yote kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini mimi ni mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya kushinda kesi mahakamani.

Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba huwezi kuwa mbunge bila udhamini wa chama cha siasa…kwa mujibu wa viongozi wangu katika chama ni kwamba udhamini wa chama changu umekwishaondolewa.”

Zitto alisema: “Kutokana na maelezo ya hapo juu, ninaomba kukutaarifu wewe na Bunge lako tukufu kwamba sina mpango wa kuendelea kupigania uanachama wangu wa Chadema katika viunga vya mahakama. Kwa hiyo ninatangaza rasmi leo (jana), kwamba taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu nitaachia uanachama wa Chadema, chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na viongozi katika chama changu.”

“Nimeona kuwa kuendelea kupigania uanachama kisheria ni kutatiza na kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini katika wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo wa vyama vingi vya siasa. Kwa kuwa taratibu hizo sijui zitakamilika lini, natumia fursa hii kuwaaga wabunge wenzangu,” alisema.

Alisema vyama vya siasa ni jukwaa muhimu la kujenga demokrasia na kwamba havipaswi kuwa juu ya matakwa ya wananchi hivyo wakati umefika wa kukomesha ufalme wa vyama vya siasa hapa nchini ambao unavipa vyama vya siasa mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya wananchi kwa kumvua uanachama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.

“Mimi ninaondoka bungeni siyo kwa sababu wananchi wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka niondoke.

Siondoki kwa sababu nimeshindwa kufanya kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki kwa sababu wanachama wenzangu katika Chadema wametaka niondoke. Ninaondoka kwa sababu mfumo wetu wa kisheria unavipa vyama vya siasa mamlaka juu ya wananchi na wapiga kura,” alisema.

Kutokana na mwanya huyo, alimwomba Spika kutumia mamlaka ya Bunge kutunga sheria kuzuia vyama vya siasa kupora mamlaka ya wananchi.

Aidha, Zitto amewataka wafuasi wake wasisikitike kwa maamuzi aliyochukua ya kujiuzulu ubunge kwa kuwa bado anafursa ya kuwatumikia kupitia jukwaa lingine ambalo atalitangaza siku chache zijazo.

Alisema anatarajia jukwaa hilo jipya litamrudisha tena bungeni katika Bunge la 11 kwa nguvu za wananchi.

Katika hotuba hiyo, Zitto aliwaomba radhi wananchi akieleza kuwa kwa miaka 10 aliyokuwa bungeni kuna mambo ambayo amekosea.

“Siwezi kuanza maisha yangu mapya kisiasa bila ya kulishukuru Bunge lako Tukufu. Kwanza, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samuel Sitta, mzee wa kasi na viwango! Bado ninakumbuka vizuri jinsi hoja ya Buzwagi ilivyotikisa Bunge lake na hatimaye kupelekea nchi yetu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo kukuza mapato ya sekta ya madini kutoka Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450 bilioni kwa mwaka,” alisema.

Alisema katika Bunge la Kumi, amekuzwa, amejifunza, amepambana, amefurahi na amelia lakini alipigania maslahi ya wananchi kwa juhudi na maarifa na hivyo kuleta mabadiliko ikiwamo kujenga ‘Bunge lenye Nguvu’ katika mfumo wa Bajeti ya nchi.

Aliwashukuru pia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambao alisema amefanya nao kazi ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi.

CHADEMA
Zitto pia alitumia muda huo kuwashukuru viongozi wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wanachama wenzake akisema wamemlea na kumuamini kufanya kazi kwa kipindi chote tangu alipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika chama na bungeni.

“Najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Inawezekana tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika dhamira kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, yaani Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo,” alisema.

“Ninawahakikishia kuwa changamoto nilizokumbana nazo na ambazo zimenilazimisha leo niondoke bungeni zimechochea zaidi dhamira, nia na sababu yangu ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya. Mheshimiwa Spika, asanteni sana na kwa herini!” alisema.

Zitto alitimuliwa Chadema Machi 10, mwaka huu baada ya Mahakama Kuu Tanzania kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali kesi yake dhidi ya Chadema ya kuhoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama hicho.

Baada ya hukumu hiyo ya Mahakama Lissu alitangaza kuvuliwa rasmi uanachama wa Mbunge huyo aliyekuwa analiwakilisha jimbo la Kigoma Kaskazini.

Lissu alisema Katiba ya Chademainaeleza wazi kwamba endapo mwanachama yeyote atakishtaki chama hicho mahakamani na iwapo atashindwa atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye chama.

KUZUIWA NA SPIKA
Taarifa zinaeleza kuwa azma ya Zitto ilishindikana baada ya kuitwa na Spika Makinda juzi na kufanya mazungumzo ya muda mrefu.

Inaelezwa kuwa Makinda alimzuia kuchukua hatua yoyote ya kuachia wadhifa huo, lakini mbunge huyo aliendelea kufanya maandalizi ikiwamo kuandika hotuba na kuisambaza kwa waandishi wa habari kwa njia ya mtandao jana.

Mbali ya kusambaza hotuba hiyo, jana mchana Zitto alikutana na wajumbe wa PAC, ambao aliwaaga rasmi.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alipoulizwa kuhusiana na azma hiyo, alisema hafahamu chochote kuhusiana na Zitto kutaka kuzungumzia ubunge wake bungeni wala Spika Makinda kumzuia.

Muda mfupi baadaye, aliwaambia waandishi kuwa Spika Makinda amemzuia kujiuzulu na kwamba bado alikuwa akiendelea kumshawishi.

ILIVYOKUWA JANA
Zitto aliwasili katika viwanja vya Bunge saa 11:15 jioni akiwa na faili alilokuwa ameandika hotuba yake ya kujiuzulu.

Baada ya kuwasili kwenye viwanja hivyo, alifanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Profesa Mark Mwandosya, baadaye Mwanasheria wake, Albert Msendo na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, kisha kuingia katika ukumbi wa Bunge.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Changa la macho wandugu!!!