ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 30, 2015

BENKI KUU YATOA TAARIFA UPOTOSHAJI SARAFU YA SH. 500


Asilimia 94 ya madini katika sarafu ya sh. 500 ni chuma na asilimia 6 ni Nickel, ameeleza Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki katika Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Marcian Kobello.
Pia ndivyo ilivyoelezwa wakati wa uzinduzi wa sarafu hii mnamo mwezi Septemba mwaka jana kabla haijaingizwa katika mzunguko mwezi Oktoba 2014.
Bw. Kobello amesema hadi sasa sarafu zenye thamani ya sh. 1,162,000,000/- zimekwishasambazwa kote nchini na kwamba kuna kiasi cha kutosha cha sarafu hiyo endapo itahitajika.
"Hakuna kabisa madini ya fedha katika sarafu ya sh. 500," amesema Bw. Kobello na kuongeza kuwa haitegemewi kwamba mfanyabiashara yeyote anaweza kununua sarafu hiyo kwa bei ya juu kuliko thamani yake halisi.
"Kwa hiyo, tunapenda kuwafahamisha wananchi kwamba kuna kiasi cha kutosha cha sarafu za sh. 500 nchini na kwamba kununua sarafu hiyo kwa bei ya juu kuliko thamani yake ni kujiingizia hasara," ameeleza mkurugenzi huyo.
Pia ameongeza kuwa Nickel sio miongoni mwa madini maarufu kwa ajili ya kutengeneza vidani vya thamani.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki

No comments: