Advertisements

Wednesday, April 1, 2015

Majambazi waua polisi wawili, IGP apangua makamanda 160

Eneo la kizuizi cha magari Mbagala Kongowe nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam lilipotokea tukio la kuvamiwa kwa askari na kusababisha wawili kuuawa kwa kupigwa risasi, juzi usiku. Picha na Venance Nestory.

Dar/Moshi. Askari polisi wawili wameuawa na mmoja kujeruhiwa baada ya kuvamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa na viashiria vya ama ugaidi au ujambazi katika kizuizi cha barabara ya Kilwa, Kipara Mpakani, Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Tukio hilo ambalo tayari limelaaniwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu, limekuja katika kipindi ambacho Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amepangua makamanda na maofisa wa polisi 160 nchini kote.
Wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ikisema inachunguza chanzo cha vifo vya askari hao ambao ni wa kanda hiyo, Chikawe alisema tukio hilo linawezekana kuwa la kigaidi au ujambazi lenye lengo la kuchukua silaha kwenda kufanyia matuko mbalimbali.
Askari waliouawa ni D.2865 SGT Francis na  E.177 CPL Michael wakati aliyejeruhiwa ni D 5573 D/SGT Ally.
Mashuhuda
Walioshuhudia tukio hilo walisema lilitokea juzi saa mbili usiku na kudumu kwa dakika 10 na kufanya eneo hilo kuwa kama uwanja wa vita kutokana na milio ya risasi.
Mkazi wa eneo hilo, Mohamed Ali alisema aliwaona watu watano wakitokea katika Pori la Kipara Mpakani, mmoja akiwa ameshika bunduki na mwingine panga.
“Niliwaona wakiwafuata askari karibu na kizuizi, mmoja alimpiga polisi risasi kifuani na mwingine akamkata polisi kwa panga shingoni,” alisema na kuongeza kuwa aliwaona askari hao wakiwa wamelala chini baada ya kuuawa... “Baada ya tukio hilo, watu wote waliokuwa karibu na eneo hili walikimbia kujificha wakihofia usalama wao.”
Shuhuda mwingine, Shiraz Abdul alisema alimwona mmoja wa askari mwingine akikimbia pamoja na wananchi baada ya tafrani hiyo... “Niliwaona askari watatu wakiwa wamelala chini, mmoja akiwa analia kuomba msaada,” aliongeza.
Shuhuda, Rehema Yusuph ambaye anaishi karibu na barabara kilipo kizuizi hicho alisema, walianza kusikia watu wakipiga kelele na kuhisi kwamba ilikuwa ajali.
“Mara nyingi huwa ajali zinatokea hapo barabarani, kwa hiyo sisi tulidhani kwamba ilikuwa ajali. Lakini baada ya sekunde chache tulianza kusikia milio ya risasi. Mara nikaona watu wanakimbilia  kwenye veranda yangu, baada ya kuuliza wakasema kuna watu wamevamia hicho kituo na wameua na kujeruhi askari.”
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jeshi hilo linachunguza kama waliofanya mauaji hayo ni magaidi au majambazi.
“Kwa jinsi walivyofanya uvamizi wa kushtukiza, kuna viashiria vya ugaidi, Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini,” alisema.
Alisema askari hao walivamiwa na kundi la watu wanaokadiriwa kuwa kati ya wanane hadi kumi wakiwa na mapanga na silaha nyingine.
“Ghafla waliwavamia askari watatu waliokuwa kazini katika kizuizi hicho kisha kupora bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30 ndani ya magazine na kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Alisema polisi mwenye namba D.5573 D/SGT Ally alipambana na wauaji hao kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo ya SMG lakini alizidiwa na kujeruhiwa kwenye paja la mguu wa kushoto na amelazwa katika hospitali ya Temeke.
Majeruhi azungumza
Akizungumza kwa tabu katika Wodi namba 5 kwenye hospitali hiyo, Ally alisema walivamiwa na kundi la watu wenye mapanga.
Alisema alipambana nao lakini kutokana na wingi wao walipora silaha ya askari mwenzake na kuondoka nayo.
Ahadi ya Chikawe
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema Serikali imesikitishwa na mauaji ya askari hao na kwamba itahakikisha wahalifu hao watapatikana na kuchukuliwa hatua kali.
“Hii hali haiwezi kuhimilika, askari wangu wawili wameuawa tena wakiwa kazini na hii si mara ya kwanza ni lazima hatua zichukuliwe kama ambavyo tulishafanyia kazi matukio ya awali. Ningekuwa na uwezo ningesimama mwenyewe na kuwa wakili katika kesi za wahalifu hao mara watakapopatikana.”
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, nayo imeeleza kusikitishwa na kulaani vikali mauaji ya askari hao wakiwa kazini.
Tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo,  Bahame Nyanduga imesema mbali na tukio hilo, imelaani kujeruhiwa vibaya kwa wafuasi 25 wa Chama cha Wananchi (CUF) lililotokea Machi 25 Makunduchi, Zanzibar.
“Tume inawataka wananchi kuheshimu haki za binadamu na kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliwa na matukio makubwa ya kuipigia kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu Oktoba,” lilisema tamko hilo.
Mabadiliko polisi
Wakati hayo yakitokea, IGP Mangu amefanya mabadiliko makubwa ambayo yanagusa vigogo 160 wa jeshi hilo nchi nzima.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na jeshi hilo, zimeeleza kuwa mabadiliko hayo yamegusa pia safu ya juu ya uongozi wa jeshi hilo, ikiwa ni mabadiliko makubwa tangu ashike wadhifa huo.
Katika mabadiliko hayo, baadhi ya makamanda wa mikoa wamehamishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine huku baadhi ya wasaidizi wao wakipandishwa vyeo.
“Uhamisho huu utekelezwe mara moja na mishahara yao ihamishiwe vituo vyao vipya,” inaeleza taarifa hiyo iliyolewa juzi na kusambazwa kwa makamanda wa mikoa nchini na kusainiwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), G.A. Semiono.
Katika mabadiliko hayo, DCP Ally Mlege aliyekuwa Kanda ya Dar es Salaam, anakwenda kuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia uhalifu makao makuu.
DCP Daniel Nyambabe aliyekuwa idara ya uhusiano wa kimataifa, anakwenda kuwa mkuu wa operesheni wa jeshi hilo. Kadhalika, DCP Valentino Mlowola aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza anakwenda kuwa Mkurugenzi wa kitengo cha intelijensia.
DCP Robert Mikomangwa anatoka Makao Makuu ya Polisi kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha upelelezi cha kukabiliana na changamoto ya ongezeko la uhalifu.
Mabadiliko hayo pia yamemgusa DCP Maria Nzuki aliyekuwa RPC Ilala ambaye sasa anakuwa mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela amerudishwa makao makuu ya polisi kitengo cha upelelezi.
Maofisa wengine waliohamishwa ni SACP Lucas Mkondya anayetoka CO Vehicle Management kwenda kuwa RPC Ilala wakati RPC Pwani, Ulrich Matei akihamishiwa Kanda ya Dar es Salaam.
SACP Fulgence Ngonyani anatoka kuwa RPC Njombe na kwenda kuwa RPC Kilimanjaro na SACP Ferdinand Mtui anatoka Idara ya Operesheni kwenda kuwa RPC Kigoma.
RPC Tanga, Frasser Kashai anatoka Tanga na kuwa Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
ACP Franco Kibona anatoka RCO Njombe na kupanda cheo kuwa RPC Njombe, ACP Zuberi Mwombeji ambaye ni RCO Iringa naye anakuwa RPC Tanga.
Uhamisho huo pia umemgusa ACP Gemini Mushi aliyekuwa Ofisa Mnadhimu mkoa wa Manyara anayekwenda kuwa RPC Mkoa wa Simiyu. Uhamisho huo umegusa Ma-RCO, wakuu wa polisi wa wilaya (OCD), wakuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CID), wakuu wa vituo (OCS) na maofisa wanadhimu.
Mabadiliko hayo yamekuja wakati jeshi hilo likitikiswa na vitendo vya uhalifu likiwamo wimbi jipya la kuvamiwa na kuuawa kwa polisi na kuporwa bunduki za kivita.
IGP Mangu alithibitishwa kuwapo kwa mabadiliko hayo na kuthibitishwa pia na msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba.
Imeandikwa na Susan Mwillo, Raymond Kaminyoge na Daniel  Mjema, Moshi wa Mwananchi

No comments: