Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amevitaka vyama kurekebisha katiba zao kwenye kipengele kinachoruhusu kuanzishwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama.
Vyama vyenye vikosi cha ulinzi na usalama ni Chadema chenye Red Brigade, CCM (Green Guard), CUF (Blue Guard) na sasa ACT-Wazalendo (ACT Amani).
Mutungi alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo unakwenda kinyume na Katiba ya nchi inayolipa jeshi la polisi mamlaka ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza baada ya mkutano wake na vyama hivyo jana, Jaji Mutungi alisema katiba za vyama vingi vilivyosajiliwa kabla hajaingia ofisini vilikuwa na kifungu kinachoruhusu kuanzishwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama wa mali za chama au viongozi wao wawapo katika mikutano.
“Haturuhusu kifungu hicho kuwapo kwenye katiba za vyama vinavyosajiliwa sasa (hakugusia ACT - Wazalendo). Hatuvifundishi vyama vya siasa namna ya kuandaa katiba zao lakini tunasimamia kifungu hiki kwa vile kinapingana na sheria.”
Jaji Mutungi alisisitiza kuwa vyama vya siasa nchini havina uelewa wa sheria ya vyama vya siasa ambayo ndiyo inayovisimamia, ndiyo maana vinashindwa kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria hiyo.
Kauli ya polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu alisema watapambana na vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu endapo vitaingilia majukumu ya jeshi la polisi.
Alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo ni kinyume cha sheria inayolipa Jeshi la Polisi dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Alisema vikundi hivi vilianzishwa kama chipukizi au halaiki lakini baadaye vilikuwa na kubadili malengo na kuanza kuingilia majukumu ya polisi na kuhatarisha amani.
Maoni ya wadau
Hata hivyo, kauli za Msajili na Mangu zilipokewa kwa hisia tofauti na viongozi wa vyama hivyo na baadhi vikiweka wazi kuwa havipo tayari kuachana na vikundi hivyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema vijana wa Green Guard hawaandaliwi kijeshi na kuwa tishio kama vyama vingine, bali kuwafanya wawe vijana bora, wakakamavu na kuwajengea uzalendo ndani ya nchi yao.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema chama chake hakipo tayari kuivunja Red Brigade huku akiilaumu CCM kuwa kikundi chake cha Green Guard kimepata mafunzo ya kijeshi kikifundishwa na askari tofauti na wao ambao wanafundishwa na raia.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Nzega jana, Mbowe alisema suluhisho la tatizo hilo haliwezi kuwa sheria bali kuhakikisha haki inatendeka na inaonekana kutendeka kwa kila chama, akitolea mfano jinsi viongozi wa chama hicho walivyopigwa na Green guard bila polisi kuchukua hatua.
MWANANCHI
1 comment:
Ali vuai. Usizue, tunajua kila kitu. Genge lako linapiga watu mitaani bila hatia. Watu wanavunjwa miguu, wanatobolewa macho na wengine hadi kufa kutokana na mateso. Kundi lako kinatumia mapanga, mabao yenye misumari, visu, na munawapa na usafiri. Pita ulizia mitaa yote ya ng'ambu Zanzibar utapewa habari hizo. Pia magenge yenu Ni wezi na wahalifu. Unasema nini wewe!?
Post a Comment