ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 26, 2015

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMA ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA BRIGEDIA HASHIM MBITA

 Mjane wa marehemu Brigedia Jenerali mstaafu Hashim Mbita, Ngeme Mbita (katikati) akiwa na waombolezaji wengine nyumbani kwa marehemu, Chang’ombe jijini Dar es Salaam leo.  Brigedia Mbita amefariki leo katika Hospitali ya Lugalo.(Picha na Francis Dande)
 Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akiwa nyumbani kwa marehemu, Brigedia Jenerali Hashim Mbita Chang'ombe jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mjumbe wa Heshima wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Said El Maamry na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku.
Waombolezaji
 Ndugu na jamaa wakiwa katika msiba wa Brigedia Hashim Mbita.
 Waombolezaji wakiwa na huzuni nyumbani kwa marehemu.
Baadhi ya ndugu na jamaa wakiwa na majonzi.
Wanafamilia wakiwa katika hali ya huzuni leo.
Baadhi ya ndugu na jamaa wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa marehemu.
 Mtoto wa marehemu, Idd Mbita akitoa taarifa za shughuli za mazishi ambapo marehemu atazikwa katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam siku ya Jumatano saa 10 jioni.

Na Mwandishi Wetu
Rais Jakaya Kikwete amepokea kwa majonzi makubwa kufuatia kifo cha mmoja wa watumishi wa miaka mingi wa Serikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), Chama cha TANU na Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Africa – Liberation Committee of the African National Unity (OAU), Brigedia Jenerali Hashim Mbita.


Rais Kikwete amemwelezea marehemu Mbita kama mmoja wa viongozi ambao wameifanyia Tanzania mambo  mengi na kwa miaka mingi. 



Kutokana  na taarifa za msiba huo, Rais Kikwete ameelekeza Serikali na Jeshi kushirikiana na familia kusimamia msiba huo na kuandaa mazishi yake.


Rais Kikwete alipokea taarifa hiyo ya msiba alipoingia tu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuongoza maelfu ya wananchi kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, aliuelezea msiba huo kama msiba wa simanzi kubwa.


“Ni wachache katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na Mzee Hashim Mbita kwa kiwango cha utumishi uliotukuka, wa miaka mingi na usiokuwa na kasoro. Katika utumishi wa Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari Mkuu wa Idara ya Habari na pia kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais kabla na baadaye kuwa Balozi wa Tanzania katika Zimbabwe. Kazi zote alizifanya kwa ufanisi mkubwa sana,”alisema Rais Kikwete na kuongeza:


“Katika Chama cha TANU alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama na katika Jeshi letu makini, Mzee Mbita alipata na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali, yote mambo makubwa kweli kweli.




“Lakini ilikuwa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Afrika ambako Mzee Mbita alikamilisha utumishi wake kwa kusimamia shughuli nzito ya kuwasaidia ndugu zetu Kusini mwa Afrika kwa miaka 20 mfululizo, miongo miwili, na kuweza kupata uhuru wao. Hakuna mpigania uhuru katika Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola na hatimaye katika Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango wa Mzee Mbita. 

Wote hawa amewatumia vizuri, kwa ufanisi, kama mlezi, kama kiongozi, kama kamanda hadi wakafanikisha kazi ya ukombozi. Huu ni mchango mkubwa kweli kweli.



 “Kitendo chake cha mwisho cha utumishi, kilikuwa kuongoza shughuli za Mradi wa Hashim Mbita wa Kuweka Kumbukumbu za Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika na Kuenzi Viongozi Wakuu (Hashim Mbita Project to Honour Outstanding Leaders), kazi ambayo nayo aliifanya kwa uwezo na ufanisi mkubwa na ripoti yake tukaizindua mwaka jana pale Victoria Falls, Zimbabwe wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),”alisema Rais Kikwete.



Alisema Zimbabwe ilitangaza kumpa Mzee Mbita Nishani ya The Royal Order Munhumutapa yenye kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe. 

Mzee Mbita amekuwa raia wa sita wa kigeni, na wa kwanza asiyekuwa rais, kupata heshima hiyo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe kwa wageni ambao wamechangia Uhuru wa Zimbabwe. 

Viongozi watano wa mwanzo kupata Nishani hiyo, mwaka 2005, walikuwa ni Marais na Viongozi Waanzilishi wa Kundi la Nchi za Frontline States dhidi ya Ukoloni na Ubaguzi wa Rangi, Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Kenneth David Kaunda wa Zambia, Marehemu Sir Seretse Khama wa Botswana, Marehemu Samora Moises Machel wa Musumbiji na Marehemu Augustinho Neto wa Angola.


Brigedia Jenerali mstaafu, Hashim Mbita amefariki dunia katika Hospitali ya Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dare es Salaam.



Mbita ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), alifariki dunia leo majira ya saa 3 asubuhi.


Akizungumza nyumbani kwa marehemu Chang’ombe, Temeke, mtoto wa marehemu, Iddi Mbita amesema baba yake alifariki kutoka na kusumbuliwa na shinikizo la damu.

“Mzee alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu na leo (jana) ameamka salama, akanywa chai na dawa, kisha akaomba kupumzika. Baada ya muda mfupi akafariki dunia asubuhi muda saa 3,” alisema Iddi.

Alisema marehemu Mbita alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la hilo tangu Agosti mwaka jana, hivyo kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema akiwa katika hospitali hiyo, aliwekwa chini ya Uangalizi Maalum wa Daktari (ICU).

Alisema alikaa katika hospitali hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu na ilipofika Oktoba mwaka jana alipelekwa nchini India kwa matibabu zaidi. 

Iddi alisema alikaa nchini India kwa miezi miwili na Januari mwaka huu alirudishwa nchini na kuendelea na matibabu nyumbani kwake Chang’ombe jirani na Klabu ya TCC Chang’ombe.

Alisema kwamba Machi 23 mwaka huu Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania JWTZ walimfuata na kumchukua kwa ajili ya kumpatia matibabu zaidi.

Alisema baada ya vipimo mdaktari katika Hospitali ya Lugalo walibaini kuwa kuna matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakimsibu hivyo aliendelea kupata matibabu hadi alipoaga dunia.

“Unajua ugonjwa ulikuwa umemla sana hivyo kusababisha organ (mfumo wa viungo vya mwili)  mbalimbali kupata hitilafu,” alisema Iddi.   
Alisema marehemu ataswaliwa nyumbani kwake Chang’ombe na mwili utapelekwa katika msikiti wa kwa Mtoro, Kariakoo na baadaye mazishi yatafanyika siku ya Jumatano katika makaburi ya Kisutu saa 10 jioni.

No comments: