ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 2, 2015

Treni Dar-Kigoma kama ndege

> Mwonekano wa ndani ya treni ya kisasa ya abiria ya Kampuni ya TRL iliyozinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shabaan Mwinjaka, Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory

Dar es Salaam. Treni ya kisasa (Delux), kwenda Bara yenye mabehewa 22 ilianza safari yake ya saa 30 kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ikiwa ni tofauti ya saa sita ikilinganishwa na safari ya treni ya zamani.
Kutokana na tofauti hiyo, abiria walioanza safari kwa furaha na matumaini jana saa tano asubuhi wanatarajiwa kufika Kigoma leo saa 11 jioni badala ya saa tano usiku.
Hata hivyo, abiria hao watalazimika kuingiza mikono yao zaidi mifukoni, kutokana na kiwango kipya cha nauli kuwa Sh79,400 badala ya Sh75,700 za awali kwa daraja la kwanza.
Huku nauli za daraja la pili ikishuka kutoka Sh55,400 hadi Sh,47,600 zile za daraja la tatu zimepanda kutoka Sh27,700 hadi Sh35,700.
Kwa mtazamo wa haraka, mabehewa hayo yanavutia yakilinganishwa na yale ya awali yaliyokuwa yamekithiri kwa uchakavu, yaliyokuwa yamejaa mende na yenye milango na madirisha mabovu.
Mabehewa hayo yana viti vya kutosha, huduma ya intaneti, swichi za umeme za kuchajia simu na kuunganisha kompyuta na safari zake zimeongezeka kutoka mbili hadi tatu kwa wiki.
Akizungumza muda mfupi kabla uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mhandisi Kipallo Kisamfu alisema wamelazimika kupandisha viwango vya nauli kutokana na gharama zitakazokuwa zinatumika katika uendeshaji wa treni hiyo.
“Licha ya kuongeza kidogo kiwango cha nauli, dhamira yetu ni kuwapatia abiria huduma safi na ya raha... kila msafiri atasafiri akiwa ameketi kwenye kiti chake. Hakuna abiria atakayesafiri akiwa amesimama,” alisema na kuongeza: “Treni inayozinduliwa leo inatumia mabehewa mapya 22 yaliyonunuliwa kutoka Korea Kusini na kichwa cha treni kiliundwa upya kwenye karakana ya TRL iliyopo Morogoro mabehewa mapya yamegharimu Serikali Sh28.6 bilioni.”
Kuhusu vituo vya ambavyo treni hiyo alisema itasimama kwenye vituo vikubwa ambavyo vingi ni vile vya miji, wilaya na mikoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shabaan Mwinjaka aliwataka abiria kuwa walinzi wa treni hiyo ili kuhakikisha usafiri huo unadumu.
“Kumekuwa na tabia ya watu kujiamulia kuharibu mali za umma, ninawaomba abiria mtakaopanda treni hii muwe walinzi wa wenzenu kwa sababu baadhi ya abiria wamekuwa na tabia ya kuchora kwenye viti,” alisema Dk Mwinjaka.
Mmoja wa abiria, Saida Roman alisema Serikali inahitaji kupewa pongezi kwa hatua hiyo kwani hivi sasa abiria wanaotumia usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma watasafiri kwa raha tofauti na ilivyokuwa zamani.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Ndege ikiwa hivyo haitapata abiria