Tarehe: 14/05/2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini limeona picha chafu na zisizo na maadili za Msanii Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole alipokuwa akifanya onesho lake nchini Ubeligiji hivi karibuni.
Katika picha hizo ambazo zimelaaniwa na watanzania wengi nchini kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, Shilole anaonekana akiwa Jukwaani huku viungo vyake vya sehemu za siri vikiwa hadharani na zaidi akionesha tabia ambazo kwa kiasi kikubwa zimefedhehesha na kuidhalilisha sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla.
Aidha, BASATA limepokea malalamiko kwa njia ya simu na mawasiliano ya internet kutoka kwa watanzania waishio ughaibuni wakilaani tukio la Msanii huyo. Katika mawasiliano yao wameeleza kwamba wamefedheheshwa na kudhalilika na tabia hiyo chafu iliyooneshwa na msanii huyu.
Ikumbukwe kwamba, Shilole ni msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa, hivyo anapokwenda nje ya nchi kabla hajapata visa anapewa barua ya utambulisho kama msanii wa Tanzania, hivyo anapokuwa nje ya nchi anatambuliwa kama msanii Mtanzania, anapofanya kinyume na misingi ya kazi ya Sanaa, anajifedhehesha yeye mwenyewe, kazi ya Sanaa na nchi yetu pia.
Aidha, ikumbukwe kwamba BASATA limeshapata kumwita na kumuonya msanii huyu kutokana na tabia yake ya kutokujiheshimu pale awapo jukwaani na yeye aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo chafu. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio hayo na kwa sasa katika ardhi ya nchi nyingine ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu Sanaa kama kazi nyingine.
BASATA linapenda kueleza kwamba;
Litamuita kwa mara nyingine tena kumtaka ajieleze kwa nini alifanya onesho hilo la kujidhalilisha na kudhalilisha hadhi ya mwanamke, msanii na Sanaa kwa ujumla
Kama maelezo yake hayataridhisha hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake maana tayari ameshadhihirisha kwamba akifanyacho si Sanaa na hakina uhusiano na kazi ya Sanaa ambayo ina heshima yake na inahitaji ubunifu, weledi na kujitambua
BASATA linawakumbusha wasanii wote nchini kuwa Sanaa ni kazi kama kazi zingine lakini siku za hivi karibuni wasanii wengi wamekuwa wakikiuka suala zima la maadili kwa kutengeneza kazi chafu zisizofaa mbele ya jamii ya watanzania wanaoipenda na kuiheshimu kazi ya Sanaa yenye staha. Tuungane kwa pamoja kukemea kazi chafu zinazozalishwa na wasanii wasiojitambua kwani suala la maadili ni suala mtambuka na linaanzia katika ngazi ya familia.
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapopata mialiko ya kikazi kwenda nje ya nchi. Linawakumbusha kwamba haiwezekani msanii kutumia picha chafu na mavazi dhalili na kuonyesha utupu katika kuvuta mashabiki.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI


5 comments:
anatakiwa afungiwe shows kwa muda kama miezi 6 hivi ndo atajua umuhimu wa public presentation
MMESHINDWA KUFUATILIA VITU VYA MAANA MNAKIMBILIA VIDOGO VIDOGO. SITTI MTEMVU MPAKA LEO HAMJACHUKULIA HATUA NA MNAJUA KABISA KUWA ALIFOJI PASSPORT NA VYETI FEKI VYA KUZALIWA ILI AWE MISS TANZANIA....NA MLIKUWA MNAJUA KUWA ALISEMA UONGO NA MNAJUA PIA ALIPENDELEWA NA LUNDENGA LAKINI MMEKAA KIMYA...AU KWA VILE NI MTOTO WA MBUNGE WA TEMEKE HAMNA UBAVU WA KUMUADHIBU?? MNAFIKIRIA KUWAADHIBU WASANII MASIKINI WASIO NA BABA AU MAMA WENYE TITLE KWA SABABU MNAOGOPA AJIRA ZENU ZITAONDOKA....TENDENI HAKI KWA KILA MTU!!!
Sasa swala la Siti hapa limeingiaje? Kutokuwa na baba na mama ndio ujidhalilishe kwa kuonyesha utupu wako?ukae jukwaani uchi?Tukumbuke kuwa kukaa uchi kwa msanii jukwaani sio tu anajidhalilisha yeye bali yaweza kuleta maafa kwa watazamaji hasa wanaume.Mwenye dini atanielewa.
Sanaa ni kazi kama kazi nyingine, yapwaswa tuiheshimu kazi hii,haijalishi wewe ni yatima au ni masikini.Mungu haangalii uyatima wako.Ulaya na marekani isitupumbaze tukaona hakuna mungu,,vitu vinakuja tu kibahati.KWA HAKIKA HUU NI MSIBA,LAKINI TUKUMBUKE KUNA KUFA NA KUNA KUJIBU ULIISHI VIPI HAPA DUNIANI.
Hakuna aliezaliwa kavaa nguo kwa hivyo sidhani kumba muumba atajali hilo siku ya mwisho
Sasa selekali imekua baby sita -- Kwani BASATA ndio inamlipa mshahala?
Tanzania a million problems, and Shilole's nipples a'int one.
Post a Comment