ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 27, 2015

COKE STUDIO AFRIKA MSIMU WA TATU YAANZA

 Msanii Ali Kiba
Msanii Vanessa Mdee

Na Mwandishi wetu
KUFUATIA mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Msimu wa Pili wa Coke Studio Africa, Kampuni ya Coca-Cola kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Kenya, inayo furaha kutangaza kuanza tena msimu wa tatu wa burudani ya muziki maarufu kwa jila la Coke Studio Africa. msimu huu utajumuisha wanamuziki wakali 26 barani Afrika huku nyimbo mpya 52 kutumbuizwa ikiambatana na maonyesho 9 ya wanamuziki wanaotamba hapa duniani.

Maonyesho hayo ya muziki ya Coke Studio Africa ni tofauti na mengine ya aina hiyo yanayolenga zaidi kupatikana mshindi. Badala yake, maonyesho haya yanalenga kujumuisha pamoja vipaji tofauti vya wanamuziki mbalimbali kutoka barani Afrika. Aidha, yanatoa fursa kwa wasanii wanaochipukia kufanya pamoja kazi zao na wanamuziki nguli wa ndani na wale wa ngazi za kimataifa.

Msimu huu unaozinduliwa utawakutanisha wanamuziki kutoka katika nchi za Tanzania, Msumbiji, Kenya, Uganda na Nigeria, na kwa mara ya kwanza wasanii hawa wataweza kukonga nyoyo za wapenzi wa muziki kwa kushirikiana katika staili ya kipekee ijulikanayo kama mash-ups – ambayo inatawala kwa sasa katika tasnia ya muziki duniani. “Kufurahia muziki wa Kiafrika” ikiwa ndiyo kiini kikuu cha burudani hiyo, msimu huu mpya wa Coke Studio Africa utawakutanisha wasanii maarufu ambao wameonyesha mafanikio makubwa katika kazi zao, na pia maonyesho hayo yatawaleta pamoja wasanii nyota wanaochipukia katika ulimwengu wa muziki.

Chini ya ushirikiano huo mpya na Kampuni ya Coca-Cola, Shirika la Ndege la Kenya kwa upande wake litawasafirisha wasanii wote na waandaaji wa muziki wanaoshiriki katika Msimu wa Tatu wa Coke Studio Africa. Mpango huo wa ushirikiano wa makampuni haya makubwa unatokana na imani ya kwamba hatua hiyo itajenga msingi wa ubia muhimu wa kufanya kazi kwa pamoja.

Akizungumzia juu ya Coke Studio Africa Msimu wa Tatu, Meneja Bidhaa wa Coca-Cola Tanzania, Maurice Njowoka alisema: “Lengo letu ni kuufanya na kuwezesha namna ambayo muziki unavyoweza kuchukua nafasi katika kukonga nyoyo za watu katika Bara letu. Coke Studio Msimu wa Tatu si kwa ajili ya kuwakutanisha tu wanamuziki wa Afrika, bali pia maonyesho haya yanatoa fursa ya pekee ya ushirikiano ambao ni imani yetu kuwa wateja wetu pamoja na umma kwa ujumla wangependa kuusikia.”

Bwana Njowoka alisema kwamba, msimu huu wa Coke Studio Africa Msimu wa Tatu unatarajiwa kuwa na mambo makubwa na mazuri zaidi na utatoa fursa ya kipekee kwa kila mtu kuburudika zaidi. Miongoni mwa nyota watakaotoa burudani msimu huu ni pamoja na Ali Kiba, Vanessa Mdee Ben Pol na Fid Q kutoka Tanzania.

Wengine ni AVRIL, Wangen, The Unstoppable Elani na Juacali kutoka Kenya il-hali kwa mara ya kwanza Malkia wa Afrika, 2Face Idibia, ataonyesha vitu vyake motomoto akiungana na nyota wengine kama vile Yemi Alade. Magwiji wengine katika tasnia hiyo ya muziki watakaokuwapo ni pamoja na Dr. Jose Chameleone, Neyma, Dama Do Bling kutoka Msumbiji.

Mkuu wa Idara ya Masoko wa Shirika la Ndege la Kenya, Jacquie Muhati, alisema ya kuwa ushirikiano kati ya shirika lake na Kampuni ya Coca-Cola utatoa fursa kwa wasanii hao wa Afrika kufurahia huduma nzuri za usafiri zinazotolewa na shirika hilo. “Hii ni fusa kubwa kwetu kulitangaza bara letu kupitia huduma zetu bora zinazotolewa katika ndege zetu. Tumedhamiria kukuza vipaji vya wasanii wachanga barani Afrika.”

Bi. Muhati aliongeza kwa kusema kuwa ushirikiano huo ni uthibitisho wazi unaodhihirisha jinsi shirika hilo linavyojitolea katika kukuza fani ya muziki barani Afrika, na pia utashi na mapenzi makubwa ya shirika hilo kuona kuwa linakuwa sehemu ya kukuza vipaji na maendeleo ya wasanii wa Afrika.

Mwanamuziki ambaye ni mshindi wa tuzo ijulikanayo kama Grammy Award ambaye pia ni mwandaaji wa muziki, Zwai Bala, magwiji wa Kwaito kutoka Afrika Kusini, Kikundi cha TKZee, wataongoza maonyesho hayo ya muziki. Brett Lotriet, ambaye ni mwandaaji na mwongozaji wa kimataifa wa maonyesho ya TV ni miongoni mwa vinara ambaye ataoongoza uandaaji wa maonyesho ya Coke Studio Msimu wa Tatu kadri matukio yatakavyokuwa yakitokea. 

Wanamuziki wakiwa pamoja na bendi za wasanii nyota wa ndani watatoa nyimbo mpya kila wiki ambazo zitaandaliwa na waandaaji wa ndani na wale wa kimataifa. Baadhi ya waandaaji ni pamoja na Jaaz Odongo, Eric Musyoka na Kevin Provoke kutoka Kenya, Cobhams Asuquo, Masterkraft na Chopstix kutoka Nigeria, Owour Arunga kutoka Marekani, Nahreel kutoka Tanzania na Silvastone kutoka Uingereza. Yakiwa yamesheheni nyota wakali wa muziki, maonyesho haya ya msimu huu yataufanya muziki wa Afrika ukue na kufikia katika hatua mpya ya juu zaidi.
Kwa Mhariri:

Mash-up ni wimbo au tungo ya muziki ambao umeandaliwa kwa kuchanganya nyimbo mbili au zaidi zilizorekodiwa mapema, na kwa kawaida hufanywa kwa kuchanganya nyimbo hizo ili kutoa kitu kipya kinachowajumuisha wanamuziki wote wahusika katika nyimbo zilizochanywa.
Kwa habari na taarifa zote kuhusu Coke Studio Africa ikiwa ni pamoja na wasanii, lyrics & Television airing times tufuate kwa #cokestudioafrica au online katika link zifuatazo:

No comments: