ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 6, 2015

DC WA MISSENYI AWAPATIA MATIBABU YA BURE WATU WENYE UALBINO

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mh. Fadhil Nkurlu akimpatia mmoja wa walemavu wa ngozi kadi za afya zitakazowawezesha kupata matibabu bure wao pamoja na wategemezi wao katika vituo vya huduma za afya za serikali na zile binafsi vilivyosajiliwa na mfuko wa afya ya jamii (CHF).
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mh. Fadhil Nkurlu (wa nne kutoka kulia walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na walemavu wa ngozi pamoja na viongozi wa dini na serikali za mitaa wilayani Missenyi.


MKUU wa wilaya ya Missenyi mkoani Kagera Fadhili Nkurlu, amewalipia gharama za matibabu watu wote wenye ulemavu wa ngozi (albino) walioko katika wilaya hiyo, ili kuwawezesha kupata matibabu  kwa kipindi cha mwaka mzima kuanzia sasa.

Kadi kwa ajili ya matibabu hayo zilikabidhiwa jana na mkuu huyo wa wilaya, wakati wa hafla fupi ya chakula cha pamoja na watu hao wenye ulemavu wa ngozi, iliyofanyika katika wilaya hiyo na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini.

Akizungumza katika hafla hiyo Nkurlu alisema kuwa, kadi hizo walizokabidhiwa watu hao, zitawawezesha kupatiwa matibabu bila kudaiwa kutoa malipo wao na wategemezi wao, katika vituo vya serikali vinavyotoa huduma za afya na vile vya binafsi vilivyosajiliwa na mfuko wa afya ya jamii (CHF).

Alisema kuwa, mbali na kukabidhiwa kadi hizo, tayari amekwishafanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kagera, ili albino wote watakaofika katika kituo cha afya kilichoko katika kiwanda hicho wapatiwe matibabu bure, na kuwa ombi lake limekubaliwa.

Mbali na hilo pia mkuu huyo wa wilaya ametoa simu za mkononi kwa watu hao, ili kuwawezesha albino wasio na mawasiliano kutumia simu hizo kutoa taarifa, pindi wanapoona watu wanaowatilia mashaka katika maeneo yao, ili hatua za haraka zichukuliwe kabla ya kutokea madhara makubwa zaidi.

“Naendelea kufanya mawasiliano na vyama vya watu wenye ulemavu wa ngozi vya nje ya nchi, ili waweze kuwasaidia kupitia chama chenu, kupata vitu ambavyo havipatikani huku kwa urahisi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo gharama kubwa, mfano mafuta ya kuimarisha ngozi” alisema.

Aidha Nkurlu alitumia fursa hiyo kupiga marufuku wakuu wa shule za msingi na sekondari zilizoko katika wilaya hiyo, kuwafukuza shule watoto wa albino na kuwa atakayekaidi agizo hilo atamchukulia hatua za kinidhamu.

“Kimsingi albino ni watu ambao hawawezi kufanya kazi za kuzalisha mali kama ilivyo kwa mtu ambaye siyo albino, kwa hiyo uwezo wao kiuchumi ni mdogo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kuhimiri mikikimikiki katika shughuli mbalimbali, hivyo wahahitaji kusaidiwa,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwenyekiti wa baraza la waislamu Tanzania (Bakwata) wa wilaya hiyo alhaji Abubakari Rutashobya, alisema kuwa madhara yote yanayowakumba albino yanatokana na watu kuhama kwa Mungu na kwenda katika masuala ya ushirikina.

“Viongozi wenzangu wa dini mbalimbali, tujitahidi kuwarudisha watu wetu kwa Mungu, watu wafundishwe wajue kuwa Mungu ni mgawaji kila mtu anayeingia hapa duniani ameandikiwa riziki yake, hivyo sio busara kuua wenzetu kwa madai ya kupata utajiri” alisema alhaji Rutashobya.

Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika hivi karibuni, wilaya ya Missenyi inakisiwa kuwa na watu wenye ulemavu wa ngozi 14.

No comments: