Advertisements

Thursday, May 28, 2015

Kijana ajitosa kumwoa mtoto wa Obama

Rais Barrack Obama wa Marekani akiwa na mtoto wake Malia.

Naroibi, Kenya. Mwanasheria kijana nchini ametuma ombi la kumuoa mtoto wa Rais Barack Obama anayeitwa Malia.

Mwanasheria Felix Kiprono alisema jana kwamba yupo tayari kutoa ng’ombe 50, kondoo 70 na mbuzi 30 ikiwa ni mahari ya kumposa mtoto huyo.

Alisema kuwa analazimika kufanya hivyo ili kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kumuoa mtoto wa Rais Obama.

“Nimevutiwa kumchumbia Malia tangu mwaka 2008,” alisema Kiprono baada ya kuhojiwa na gazeti la The Nairobian.

Wakati mwanasheria huyo akivutiwa na binti huyo mwaka 2008, Obama alikuwa Rais wa Marekani katika awamu ya kwanza na Malia alikuwa na umri wa miaka 10.

“Ukweli ni kwamba sijawahi kuwa na uhusiano na mwanamke yeyote tangu nilipovutiwa na Malia. Nimeieleza familia yangu na wameniunga mkono,” alisema Kiprono.

Kiprono alisema ana nia ya dhati ya kumuoa Malia, pia, ana imani kwamba wakati Obama atakapoitembelea nchi hiyo Julai, mwaka huu atampelekea binti hiyo.

“Hivi sasa nimeanza kuandika barua kwa Obama ya kumwomba aje na Malia katika ziara yake. Nina imani kwamba ubalozi wa Marekani nchini hapa utafikisha barua yangu kwake,” alisema Kiprono.

Mwanasheria huyo alifafanua kwamba ana nia ya dhati ya kumposa binti huyo na wala hafuati fedha za kiongozi huyo mweusi wa Marekani.

“Watu wanaweza kufikiri kwamba nataka kuoa kwa sababu ya fedha za familia ya Rais Obama, hiyo siyo kweli, nina mapenzi ya dhati kwa Malia,” alisisitiza.

Mwanasheria huyo kijana ambaye hakupenda kutaja umri wake, alisema endapo wazazi wa Malia watakubali, sherehe ya harusi itakuwa ya kimila na itafanyika kijijini kwa wazazi wake.

Kiprono alisema baada ya kumwoa wataishi maisha ya kawaida na hawataishi maisha ya anasa.

“Nitamfundisha Malia kukamua maziwa, kupika ugali na kupika chakula cha asili ya Wakalenjini kama wafanyavyo kina mama,” alisema Kiprono.

Baba yake Obama ni Mkenya na bibi yake aliishi katika Kijiji cha Kogelo, magharibi mwa nchi hiyo.

MWANANCHI

3 comments:

Unknown said...

Endelea kuota ndoto zako hizo. Ila usiende kufanya miti shamba. Hivi huko umesikia Baba mzazi anampeleka Binti yake ili akaposwe? Hiyo ni tamko la dharau.

Anonymous said...

Hizo ni ndoto za mchana bwana Kiprono. Kila la kheri.

Anonymous said...

Pedophile.