ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 20, 2015

Kopunovic alegeza masharti Simba.

Mserbia Goran Kopunovic.

Sizitaki mbichi hizi zimeanza kujitokeza kwa Mserbia Goran Kopunovic ambaye alishindwana na Simba baada ya kuitaka klabu hiyo kumpa Sh. milioni 100 za ada ya usajili ili kusaini mkataba mpya huku pia akiitaka kumuongeza mshahara na kuwa Sh. milioni 28 kwa mwezi.

Hata hivyo, wakati Simba ikiwa katika mchakato wa kusaka mbadala wake, imeelezwa kuwa kocha huyo ameanza kuwapigia simu viongozi wa klabu hiyo na kuwaambia ameshusha kiwango cha fedha anachotaka kulipwa ili kuendelea kuinoa timu yao.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana kutoka chanzo chetu cha uhakika ndani ya klabu hiyo, zimeeleza Kopunovic sasa emeweka wazi kwamba atakuwa tayari kurejea nchini kuendelea na kazi yake kwa kusaini mkataba mpya kwa dau la Dola za Marekani 40,000 (Sh. milioni 80 za Tanzania) badala ya Dola za Marekani 50,000 (Sh. milioni 100) ambazo alizihitaji awali.

Chanzo hicho kilieleza kuwa ada hiyo ya kusaini mkataba ni kwa muda wa miaka miwili na kwamba mwaka wa kwanza Simba imlipe kiasi cha Dola za Marekani 20,000 na kiasi kilichobaki alipwe mwaka unaofuata.

Kadhalika kilisema kocha huyo amekubali kuinoa Simba kwa mshahara wa Dola za Marekani 6,500 (Sh. milioni 13) kwa mwezi badala ya Dola za Marekani 14,000 (Sh. milioni 28) alizohitaji hivi karibuni kabla ya kurejea Hungary anapoishi na familia yake.

"Kocha amepiga simu jana (juzi) tulikuwa watatu (majina tunayahifadhi) na kusema kuwa sasa amepunguza ofa na kuwa Dola 40,000 za Marekani na atakuwa tayari kulipwa ada ya kusaini mkataba kwa awamu mbili na mshahara wake wa kila mwezi kuwa Dola 6,500," kilisema chanzo hicho.

Kiliongeza kuwa Kopunovic aliingia 'tamaa' ya kupandisha dau baada ya kupata taarifa ya kiasi cha mshahara anacholipwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam, Mcameroon Joseph Omog.

Rais wa Simba, Evans Aveva, aliliambia gazeti hili juzi kuwa bado uongozi wake uko katika mchakato wa kupata kocha kwa kuendelea kupokea maombi mbalimbali na kuyajadili yale ambayo yameshawafikia.

Aveva alisema mpaka jana walikuwa na orodha ya waombaji watano ambao wako tayari kurithi mikoba ya Kopunovic na kiwango cha mishahara wanayohitaji haizidi Dola za Marekani 6,000 (Sh. milioni 12).

Kiongozi huyo aliyeingia madarakani Juni 28, mwaka jana, alisema watakuwa makini katika kufanya maamuzi kwa sababu hawataki tena hali ya 'timuatimua' ya makocha kuwapo msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Kikosi cha Simba kimepewa likizo na kitarejea tena kwenye mazoezi mapema mwezi ujao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: