ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 11, 2015

Lissu asema Dk Slaa ni Rais ajaye

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa. PICHA | MAKTABA

Moshi. Kuna kila dalili kwamba Chadema na vyama washirika vina mpango wa kumsimamisha Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kugombea urais Oktoba mwaka huu.
Dalili hizo zilijitokeza hadharani juzi kutokana na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliyoitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Majengo, Moshi akimtaja Dk Slaa kama ndiye rais ajaye huku akieleza uwezekano wa Ukawa kuchukua nchi.
Lissu alimtaja Dk Slaa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo kuwa ndiyo wabunge wa Chadema ambao hawajawahi kushindwa na CCM tangu mwaka 1995.
“Historia hiyo itasema mbunge mmoja kati yao (ambao hawajawahi kushindwa na CCM) ni Mzee Ndesamburo na historia hiyo itasema mbunge wa pili ambaye hajawahi kushindwa na CCM ni Dk Willibrod Slaa, rais wetu ajaye,” alisema Lissu.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema, alisema katika historia ya Taifa hili kuna uwezekano mkubwa wa Chadema na vyama washirika kuingia Ikulu baada ya Oktoba.
Vyama washirika ambavyo vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, vimepanga kusimamisha mgombea mmoja katika ngazi zote za uchaguzi kuanzia urais hadi udiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Dk Slaa aligombea urais 2010 na kushika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 2.3 sawa na asilimia 26.34 nyuma ya Rais Jakaya Kikwete aliyeshinda kwa kura milioni 5.3 sawa na asilimia 61.17.
Hadi sasa Ukawa haijateua wagombea wake katika ngazi hizo ambazo ni urais, ubunge na udiwani ambao watachuana na wagombea wa vyama vingine.
Katika mkutano
Katika hotuba yake hiyo, Lissu alisema: “Katika miaka 20 ya kwanza ya mfumo wa vyama vingi, kuna wabunge wawili pekee ambao hawajawahi kushindwa na CCM.”
Kauli hiyo ya Lissu iliwafanya wananchi hao kulipuka kwa furaha na kukatisha hotuba hiyo.
Hata hivyo, Lissu hakufafanua zaidi kuhusu kauli yake hiyo zaidi ya kusisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuenzi mchango wa kiongozi huyo na wa Ndesamburo.
Ukawa kuchukua nchi
Lissu alisema mwaka huu kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, kuna uwezekano mkubwa kwa Chadema na vyama washirika wa Ukawa kushinda uchaguzi na kuchukua nchi.
“Kuna uwezekano mkubwa (kushinda urais) na kwa sababu hiyo kuna uwezekano mkubwa vilevile kwa yeyote atakayeteuliwa kugombea udiwani au ubunge kushinda uchaguzi,” alisema Lissu na kuongeza:
“Uwezekano huo ni mkubwa kuliko kipindi chochote cha miaka 20 ya mfumo wa vyama vingi. Upo uwezekano wa kuwa na wabunge wengi kila mahali. Upo uwezekano mkubwa wa kuunda Serikali.”
Fitina kupenyezwa
Hata hivyo, Lissu alitahadharisha kuwa kutokana na uwezekano huo mkubwa wa Ukawa kuchukua nchi, pia ni kipindi mwafaka cha CCM kupenyeza fitina na majungu ili kufarakanisha umoja huo.
“Kwa sababu ya uwezekano huo huu ndiyo wakati mwafaka wa fitina na majungu na watu kupenyeza vipande 30 vya fedha (rushwa). Huu ndiyo wakati kwa watu kutaka uongozi kwa rushwa,” alisema.
Lissu alifafanua miaka ya nyuma chama hicho kilikuwa kikipata shida ya kupata wagombea lakini kwa kuwa sasa baadhi ya majimbo yana wagombea zaidi ya watano kwa sababu kuna matumaini mbele.
“Kuna majimbo Kanda ya Ziwa yana wagombea 18 kwa sababu kwa mara ya kwanza watu wanaona kuna tumaini. Watu wanaona hiki chama na washirika wake wa Ukawa ni vyama vya kwenda Ikulu.”
“Kwa hiyo kila mtu anataka awe mbunge na kila mtu anataka awe waziri. Ukiwa mbunge uwezekano wa kuwa waziri ni mkubwa. Kwa hiyo ni kipindi cha fitina. Ndiyo kipindi cha majungu,” alisema.
Lissu alitahadharisha kuwa kama viongozi na wanachama wataruhusu hali hiyo itokee ni wazi kuwa Ukawa itaparanganyika na kutoa mwanya kwa CCM kuchukua tena dola.
“Tukifarakana nchi itarudi kwa watu wa Escrow, Epa, Tokomeza na watu wa aina hiyo. Hiki ni kipindi cha kuhakikisha wagombea wetu wote wanakuwa na nidhamu,” alisema Lissu na kuongeza:
“Kamati Kuu yetu (Chadema), imesema tuna majimbo 24 tuliyoyapata 2010. Haya majimbo tunahitaji kuyalinda kwa udi na uvumba. Kamati Kuu imesema haitaruhusu ugomvi na fitina katika majimbo haya.”
Alisema kama chama hicho kitaruhusu kila anayetaka kugombea ubunge katika majimbo hayo afanye anavyotaka, upo uwezekano wa kuyapoteza jambo ambalo hawako tayari nalo.
Lissu alitumia mkutano huo kutoa somo wanaotaka kurithi mikoba ya Ndesamburo akisema kunahitajika nidhamu ya hali ya juu, “hivi ni kweli hivi ‘vimiguu’ vyangu vinaweza kuvaa viatu vya Ndesa?”
Ndesamburo na meya
Kwa upande wake, Ndesamburo alitumia mkutano huo kueleza kuwa alipomtangaza Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael kuwa mrithi wake hakuvunja katiba wala kanuni za chama chake.
“Niliposema sipiganii, nikasema kuna kijana nimemjenga sikufanya masihara. Wala sijavunja kanuni wala katiba ya chama,” alisema Ndesamburo huku akishangiliwa na kuongeza: “Kila mmoja ana haki ya kusema huyu anafaa. Mwenye ubavu aje akashindane na mtu ambaye Ndesamburo amesema anafaa.”
Mwananchi

No comments: