ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 9, 2015

MKUU WA WILAYA MISSENYI MH.FADHIL NKURLU AKAMATA SHEHENA LA NGOZI ZA MAGENDO

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mh. Fadhil Nkurlu (kushoto) akimhoji dereva wa lori aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Kabyemela (mwenye tisheti jekundu) baada ya kuwekewa mtego na kukamatwa na shehena ya ngozi ya magendo iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea nchi jirani. Shehena hiyo ilikamatwa katika kizuizi cha Kyaka.
 Baadhi ya ngozi ya magendo iliyokamatwa baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kuweka mtego kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama. Shehena hiyo ya ngozi ya magendo inakisiwa kufika uzito wa takribani tani 10.


Missenyi. 8 Mei, 2015 - Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mh. Fadhil Nkurlu amekamata shehena kubwa ya ngozi ya magendo yenye uzito unaokisiwa tani 10 ikisafirishwa kwenda nje ya nchi bila kibali wala nyaraka zozote za serikali. 

Kutokana na taarifa za ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Missenyi ngozi hiyo ilitokea Kahama ikiwa inaelekea nchini Uganda na ilikamatwa katika kizuizi cha Kyaka, wilayani Missenyi. 

"Tulipata taarifa kutoka kwa raia wazalendo tangu jana yake kwamba kuna bidhaa za magendo ambayo huwa yanapita usiku, ndipo nikawapanga vijana kutoka vikosi vyote vya ulinzi na usalama kuweka mtego huu," alisema DC Nkurlu.

"Hiki ni kipindi ambacho magendo ya kahawa husafirishwa kwa wingi kwenda nje ya nchi na hivyo hukosesha serikali mapato yake stahiki. Lakini tumejipanga ipasavyo na tutahakikisha tunakamata kila aina ya magendo. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayejihusisha katika biashara hii," alisisitiza.

"Napenda kutoa rai kwa wananchi wote wa Missenyi kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa serikali ili kuweza kukamata bidhaa hizi za magendo na kudhibiti mtandao huu haramu," alisema Mh. Nkurlu. 

Hii ni mara ya pili ndani ya wiki hii magendo yanakamatwa ambapo Jumatatu shehena kubwa ya mbao zilikuwa zikisafirishwa kinyemela zilikamatwa na bado zinashikiliwa katika kituo cha polisi cha Kyaka.

No comments: