Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha
aliyekuwa mtangazaji mashuhuri na maarufu wa iliyokuwa Redio Tanzania
(sasa TBC Taifa), Ndugu Mshindo Mukeyenge ambaye alifariki dunia
mwishoni mwa wiki na kuzikwa jana, Jumatatu, Mei 25, 2015.
Katika salamu alizomtumia Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mkoa wa
Dar Es Salaam, Mheshimiwa Sofia Mjema jana, Jumanne, Mei 26, 2015,
Rais Kikwete amesema kuwa kifo cha Mzee Mukeyenge kimelinyang’anya
“taifa letu hakina kubwa ya uzoefu wa utangazaji katika kipindi
ambapo vijana wanaochipukia katika tasnia ya habari, na hasa
utangazaji, walikuwa wanahitaji sana malezi, ushauri na uongozi
wake.”
Rais Kikwete amemwelezea Mzee Mukeyenge kama Mtanzania
aliyetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa letu kupitia kipaji chake
cha utangazaji na kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa kwa
miaka mingi ijayo.
“Aidha, tutaendelea kumkumbuka Ndugu Mshindo Mukeyenge
kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo hapa
nchini, na hasa mchezo wa soka, ambako alichangia kwa
kulihabarisha taifa letu kupitia utangazaji wa mechi nyingi za soka za
kitaifa ama kimataifa,” amesema Rais Kikwete.
Amemwambia Mkuu huyo wa Wilaya, “Kwa hakika nimepokea kwa
huzuni taarifa za kifo cha Ndugu Mshindo Mukeyenge. Napenda
kuungana nawe na wana-Temeke wote katika kuomboleza kifo cha
mwenzetu. Aidha, napenda kukuomba unifikishie salamu zangu za
rambirambi kwa wanafamilia na wote ambao wamepotelewa na
mhimili wao. Wajulishe kuwa naungana nao katika machungu yao na
katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya
Marehemu Mshindo Mukeyenge. Amina”.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Mei, 2015
No comments:
Post a Comment