Habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Mwananchi juzi yenye kichwa cha habari ‘Wanawake wa Rombo wakodi wanaume kutoka Kenya’ imeibukia bungeni leo.
Habari hiyo iliandikwa kutokana na kauli aliyoitoa mkuu wa wilaya ya Rombo, Lembris Kipuyo, aliyedai kuwa kutokana na wanaume wa wilaya hiyo kuwa walevi wa kutupa, wake zao wamekuwa wakikodi wanaume kutoka Kenya ili kuwaridhisha kimapenzi.
“Tatizo la ulevi wilayani Rombo na matumizi ya pombe zisizokuwa na viwango ni kubwa sana na linahitaji nguvu kulikabili,” alisema mkuu huyo wa wilaya. “Imefikia wakati wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwaajili ya tendo hilo.”
Akiuliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), amesema habari hiyo imesababisha madhara makubwa katika jimbo lake.
Selesani amesema habari hiyo imewadhalilisha wanaume wa Rombo na wanaiomba serikali iwaombe radhi kwa kilichoandikwa.
Amesema kutokana na habari hiyo wanaume wengi wameanza kuwatilia mashaka wake zao kuwa huenda ‘wamekuwa wakichepuka’ na wakenya na hivyo kusababisha maelewano hafifu ndani ya ndoa.
Akijibu swali hilo, mheshimiwa Pinda alisema binafsi hajaisikia taarifa hiyo kwahiyo hatoweza kuomba radhi hadi pale atakapolifuatilia.
No comments:
Post a Comment