ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 9, 2015

WAZIRI MKUU AISHUKURU LIONS CLUB KWA MISAADA YAKE


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameishukuru taasisi ya Kimataifa ya Lions Club kwa misaada ambayo imekuwa ikiitoa hapa nchini katika nyanja za afya, utunzaji mazingira na uokoaji wakati wa maafa.
Akifungua kongamano la 12 la mwaka linalojumuisha wadau wote wa Lions Club District 411 leo asubuhi (Jumamosi, Mei 9, 2015), Waziri Mkuu alisema anawashukuru wana Lions wote kwani miradi mingi wanayoifanya huwa ni kwa kujitolea tu.

“Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hii kwani kwa sehemu kubwa wanachokifanya ni kile ambacho sisi kama Serikali tulipaswa tukifanye. Wanatoa huduma bure za macho, matibabu ya moyo, wanatoa misaa ya mahema, vyandarua, vyakula pale tunapokumbwa na maafa. Wanafanya kazi nzuri,” alisema.

Akitolea mfano huduma za kijamii kama vile Heart Baby Project, Waziri Mkuu alisema: “Mradi wa Heart Baby Project umedumu kwa miaka karibu 30. Wameshawachukua watoto zaidi ya 3,000 wenye matatizo ya moyo na kuwapeleka India kuwapatia matibabu kwa gharama zao,” alisema.

“Jambo kubwa zaidi la kushukuru ni kwamba asilimia 99.5 ya watoto waliofanyiwa upasuaji, wamepona na hivyo kuweza kuokoa maisha ya watoto wetu,” alisema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wajumbe zaidi ya 500 waliohudhuria Kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Lions International, Raju Manwani alisema taasisi hiyo ina wanachama zaidi ya milioni 1.4 duniani waliosambaa katika nchi 210 ambao hufanya kazi kwa kujitolea.

Naye Mwenyekiti wa Lions Multiple Council, Bw. Teja Kalsi alisema wanapojiandaa kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwa Lions Club, wamejiwekea lengo la kuhakikisha wanatoa huduma kwa watu milioni 100 kwa katika Nyanja zao nne kuu. Hivi sasa taasisis hiyo imetimiza mika 98 tangu kuanzishwa kwake.

“Uanachama ndiyo nguzo yetu kuu lakini pia tuna shauku ya kutimiza watu milioni 100 waliopata huduma zetu katika nyanja za vijana, afya na hasa huduma ya macho, utunzaji wa mazingira na kuwalisha wenye njaa. Tujielekeze huko ili tutimize kaulimbiu yetu isemayo palipo na uhitaji, mwana-lion yupo (Where there’s a need, there’s a lion),” alisema.

Kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Seychelles, Sudan Kusini, India na wenyeji Tanzania.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAMOSI, MEI 9, 2015.

No comments: