Advertisements

Monday, May 4, 2015

Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Katika ukurasa wangu wa facebook mnamo tarehe 25 Aprili 2015 niliandika kuhusu sababu za shilingi kuporomoka thamani na majawabu ya namna ya kurejesha thamani halisi ya sarafu yetu.
Nilieleza “Shilingi kuporomoka dhidi ya dola na kuvuka Dola 1 sawa na Sh2,000 kunasababishwa na sababu kadhaa:-
(1) Woga wa uchaguzi na hivyo Dola nyingi kutoingia nchini (FDI) kusikilizia Serikali ijayo inaundwaje.
(2) Woga wa uchaguzi na hivyo matajiri kununua dola kwa kasi (too many Tshs chasing too few $) ili kuzificha (hoard) nje.
(3) kutouza mazao nje na kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ( current account deficit).
(4) Benki Kuu kutoachia Dola nyingi kwenye soko kutokana na akiba ya fedha za kigeni kupungua.
(5) Kuongezeka kwa huduma ya Deni la Taifa na  malipo ni kwa fedha za kigeni kwa madeni yaliyoiva.
Niliendelea kushauri majawabu “Suluhisho (1) Benki Kuu kuachia Dola za kutosha kwenye soko katika muda mfupi na wa kati (Februari BoT ilifanya hivi na kuongeza Dola 64 milioni kwenye soko bila mafanikio 
Kuongeza mauzo nje hasa ukizingatia kwa sasa ‘our exports becomes cheaper vis a vis foreign exchange) 3) Malipo ya kodi ya Ongezeko la Mtaji kutoka BG (Shell transaction ) na Ophir (Pavilion transaction), malipo haya kwa fedha za kigeni 4) Punguza kununua vitu vya anasa kutoka nje 5) Unafuu wa huduma kwa Deni la Taifa ( Debt relief ) 6) Punguza ujazo wa fedha nchini (mop tshs out)”.
Mjadala mkali umeendelea kuhusu suala hili katika majukwaa mbalimbali. Ni dhahiri kuporomoka kwa shilingi kunaathiri sana Watanzania wa ngazi ya kati hasa wafanyabiashara wa kati wenye kununua huduma na bidhaa kutoka nje. Wenye viwanda wanaotegemea malighafi kutoka nje gharama zao za uzalishaji zimeongezeka zaidi na hivyo kuhatarisha uzalishaji mali nchini.
Licha ya kwamba kuporomoka kwa shilingi kunafanya bidhaa zetu za kuuza nje kuwa rahisi, lakini huchukua muda kuzalisha bidhaa hizo na hasa kilimo kuweza kufaidika hali hiyo. Kwa hiyo ni faida kwa nchi kwa sasa kuwa na sarafu stahimilivu (stable) iliyojengwa kwenye misingi imara ya uchumi. Hata hivyo, inaonekana kuwa sarafu ya Tanzania inahujumiwa. Kuporomoka kwa Shilingi katika wiki za hivi karibuni siyo matokeo ya nguvu za soko bali ni matokeo ya hujuma ( currency manipulations).
Benki kubwa za kigeni nchini, inasemekana, katika miezi ya karibuni zimefanya currency manipulations na kupelekea dola chache kukimbizwa na shilingi nyingi na hivyo bei ya dola kupanda.
Hii inatokana na ukweli kwamba benki zetu kubwa tatu zinazoongoza, zinaendeshwa na wageni. Inasemekana biashara hii hufanyika kati ya matawi ya benki za kigeni hapa nchini na makao makuu yao.
Kuporomoka kwa shilingi kunakotokea hivi sasa hakuendani na kuporomoka kwa miaka ya nyuma kipindi kama hiki (ambacho kwa kawaida ni miezi shilingi hushuka thamani kwa sababu ya watalii kuwa wachache na mauzo ya bidhaa nje kuwa madogo sana). Wastani wa miaka 10 iliyopita inaonyesha kuwa kipindi hiki shilingi hushuka kwa kati ya asilimia nane hadi asilimia 13 na siyo kuporomoka  kwa zaidi ya asilimia 20 kulikotokea hivi sasa.
Kwa mfano mwaka 2011 miezi kama hii (Februari – Mei) Shilingi iliporomoka kutoka Sh1,380 kwa dola moja hadi Sh1,570 sawa na mporomoko wa asilimia 12. Hata hivyo kuanzia mwaka huo hadi mwaka 2014, shilingi imekuwa ikishuka thamani kwa kiwango kidogo sana. Mwaka 2013 thamani ya shilingi ilishuka kwa wastani wa asilimia 1.7. 
Uchambuzi huu wa thamani ya sarafu yetu unaonyesha kuwa kuna zaidi ya nguvu ya soko kunakotokana na mauzo yetu nje kuwa machache. Vilevile kupanda kwa thamani ya Dola ya Marekani duniani hakutoshi kuelezea mporomoko huu wa kasi wa shilingi kuanzia Desemba mwaka 2014 mpaka sasa. Tuhuma za benki kuwa zinahujumu shilingi (currency manipulations) zaweza kuwa na ukweli.
Vilevile, inasemekana kumekuwa na utoroshwaji mkubwa wa dola kutoka nchini kwenda nje ya nchi. Utoroshaji huu unafanyika kupitia wasafiri wanaopita VIP Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam. Utoroshwaji huu unatokana na hofu isiyo ya msingi kwamba uchaguzi utakuwa na vurugu. Utoroshwaji wa fedha ni kinyume sheria zetu. Sheria zetu za fedha za kigeni zinazuia mtu kubeba zaidi ya Dola 10,000 za Marekani zikiwa taslimu, kuingia nazo nchini au kutoka nazo nchini.
Utafiti wa haraka unaonyesha kuwa huu umekuwa ni utaratibu wa kawaida kila mwaka wa uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi uanze.
Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua zifuatazo;
Kufanya uchunguzi wa kushtukiza mara moja kwa benki zote za kigeni zilizopo hapa nchini. Uchunguzi huu utazame biashara ya fedha za kigeni ya benki hizi kwa lengo la kuzuia ‘currency manipulations’ na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya benki yeyote itakayokutwa imehujumu biashara ya fedha za kigeni kwa lengo la kushusha thamani ya shilingi dhidi ya Dola za Marekani.
Polisi na Kitengo cha Kuzuia Utoroshaji wa Fedha (anti money laundering unit) kufanya ukaguzi wa lazima wa watu wote wanaosafiri kwenda nje ikiwamo wanaopita sehemu ya watu mashuhuri (VIP Lounge) ili kudhibiti utoroshaji wa fedha za kigeni kwenda ughaibuni.
Watanzania tufikirie upya nafasi ya benki zetu katika uchumi wa nchi na kufanya maamuzi magumu ya kurejesha baadhi ya Benki katika umiliki mpana zaidi wa Watanzania.
Kwa malengo ya muda wa kati, Benki kubwa 3 nchini ilazimu kuwa na umiliki unaozidi asilimia 51 wa Watanzania. Bila ya kushika mabenki nchi itachezewa sana.
Suluhiho la kudumu la sarafu stahimilivu ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje.
Urari wa Biashara wa Tanzania umepanuka kutoka Dola 1 bilioni mwaka 2004 hadi Dola 6 bilioni mwaka 2013 (BoT 2013) kutokana ununuzi wetu nje kukua kwa kasi kutoka Dola 2.5 bilioni hadi Dola 11 bilioni wakati mauzo yetu nje yakikua kwa kasi ndogo kutoka Dola 1.4 bilioni hadi Dola 5 bilioni katika kipindi hicho.
Isingekuwa uimara katika urari katika uwekezaji na uhamisho wa mitaji, Tanzania ingekuwa na sarafu yenye thamani sawa na takataka. Serikali ihimize uzalishaji mali mashambani na viwandani na kuuza nje biadhaa zilizoongezwa thamani. Zama za kutegemea dhahabu zimekwisha na siyo endelevu. Turudi kwenye misingi bidhaa za kilimo na viwanda.
Tutaendelea kufuatilia thamani ya shilingi hadi Julai na ndipo kipindi kigumu kwa shilingi huwa kihistoria. Hatua zilizoainishwa zisipotazamwa na mamlaka tajwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani yaweza kufikia Sh3,000.
Mwananchi

1 comment:

Mdau said...

Bwana Kabwe amegusa sehemu nyeti kuhusu kuporomoka kwa shilingi,amesisitiza kuzalisha na kuuza bidhaa zetu nje,lakini hakugusa ukiritimba uliopo kwenye sera za serekali kuhusu export licences,mpaka leo Mtanzania haweze kuzalisha na kuuza bidhaa zake nje bila kupitia board Fulani, kwa mfano kuuza kahawa nje bila hupitia vikwazo vingi ikiwamo Tanzania Coffee Board, review and ease the unnecessary huddles the Tanzania Citizen have to go through to export their products.