Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na wajumbe toka nchi wanachama wa WMO.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi pamoja na ujumbe wa Tanzania akiwemo Bwana Mohamed Ngwali, Mkurugenzi wa TMA – Ofisi ya Zanzibar, wanashiriki mkutano mkuu wa 17 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) unaofanyika Uswisi, makao makuu ya Shirika hilo kuanzia tarehe 25 Mei hadi 12 Juni 2015.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huyo, katika mahojiano yaliyofanyika kabla ya kuanza safari Dkt. Kijazi alisema ni muhimu kwa Tanzania kushiriki mkutano huo ili kutekeleza makubaliano ya kimataifa. Aliongeza kusema mkutano huo ni wa 17 na utahusisha uchaguzi na uthibitisho wa Katibu Mkuu wa WMO, uchaguzi wa Rais wa WMO na makamu wake watatu pamoja na uchaguzi wa wajumbe wa Baraza kuu (Executive Council). Aidha Dkt. Kijazi alisema mkutano huo utapitia na kupitisha mipango ya muda mrefu na bajeti ya shirika hilo. ‘ Tanzania itahusika moja kwa moja katika uchaguzi wa Katibu Mkuu, Rais, Makamu wa Rais na wajumbe wa baraza kuu pamoja na kupitisha bajeti na mpango mkakati wa muda mrefu kwa ajili ya shirika hilo’ Alisema Dkt. Kijazi.
Shirika hilo limekuwa likifanya mkutano mkuu kila baada ya miaka minne (4) na kushirikisha nchi wanachama ambao kwa sasa idadi yake ni 191.
Kwa kipindi cha hivi karibuni dunia imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo moja ya agenda ni kuhakikisha mkutano huo unaweka mikakati yenye tija katika kupambana na changamoto hizo sambamba na ajenda nyingine mbalimbali zitakazojadiliwa.
Tunawatakia Dkt. Kijazi na Ujumbe wote wa Tanzania majadiliano yenye tija katika mkutano huo muhimu.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI, OFISA MAHUSIANO MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
No comments:
Post a Comment