Advertisements

Tuesday, July 28, 2015

"KATIKA SIASA HAKUNA MALAIKA WALA SHETANI"-Maria Sarungi

Tanzania tunaweza kujenga jamii ya kidemokrasia na itajengwa na SISI wananchi na si wanasiasa. Kwa sababu wanasiasa wako bize kutwaa madaraka – mwanasiasa yoyote yule – tusidanganyike! Hivyo basi sisi wananchi tukiwa kama wanachama wa vyama, kama wapiga kura, tuhakikishe tunakuwa mashabiki wa demokrasia na uwazi kwanza na si mashabiki wa vyama na wanasiasa.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali kwa upande wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kinachonisukuma kusema kuwa tunachoona hivi sasa ni historia. Bila kupoteza muda mrefu kujaribu kuzungumzia matukio naona kuwa watanzania tungefaidika zaidi kuelewa vyema zaidi nini hasa tunachokiona.

Lazima tukubali kuwa lengo moja kuu (kama si lengo kuu pekee) ya chama chochote cha kisiasa ni kuingia madarakani. Vyama hivi vinaweza kutushawishi kuwa wanataka madaraka haya kwa sababu wanataka kutusaidia na ni haki na wajibu wetu kutathmini na kuamua ni chama kipi kitatusaidia kama jamii kufikia malengo tutakayokubaliana nayo. Lakini kwa kifupi wanataka madaraka. Tukishakubali hali hii, basi tunaweza kuangalia tukio lolote la kisiasa kama ushindani wa kutwaa madaraka. Na ni muhimu tutambue hili bila kujaribu kudai kuwa eti mwanasiasa au chama fulani kinatupenda na kutujali zaidi na kadhalika. Hilo ni suala la mtazamo na kwa sasa tuliweke pembeni.

Ninachotaka tujaribu kuangalia ni kuwa ushindani huu wa kutwaa madaraka pia yapo ndani ya chama chochote cha kisiasa. Na ni kitu kizuri sana. Naamini ndani ya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR tutaendelea kuona malumbano kwa sababu ya uchaguzi mkuu 2015. Ni uchaguzi wa kihistoria kwa sababu rais aliyopo madarakani hatagombea tena (hakuna incumbent) hivyo hata mgombea wa CCM atakuwa ‘mgeni’ kwa wapiga kura. Hivyo vyama vya upinzani vina nafasi kubwa sana wakicheza karata zao vizuri. Lakini pia ndani ya CCM, hakuna mteule mpaka sasa – kwa hiyo yoyote anaweza kuibuka kuwa mgombea. Tukishaweza kuangalia hali ya kisiasa kwa jicho hili tutaona kuwa ndani ya vyama kuna makambi ambayo yanaona kuwa wao wakiendesha chama sasa wanaweza kukihakikishia ushindi chama chao. Hivyo uongozi wa chama nao unawaniwa. Na ninarudia hakuna ubaya wowote tena ni kitu kizuri. Kwani asiyekubali kushindana si mshindani – na ukweli ni kuwa mgombea ambaye atateuliwa tu na chama chake bila kupitia ushindani mkubwa ndani ya chama chake, mara nyingi hawi mgombea mwenye ushwawishi mkubwa. Kusoma zaidi bonyeza HAPA

No comments: