HAKUNA adui wala rafiki wa kudumu katika siasa. Huu ni msemo ulioasisiwa na mwanadiplomasia wa Israel, Avil Primor ambaye amepata kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani, ikiwemo ubalozi wa nchi yake nchini Ujerumani (1993-99) na katika Umoja wa Ulaya (1987-91).
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia urafiki kati ya nchi yake na Iran ulivyokuwa. Kabla ya mapinduzi ya nchi hiyo ya Kiarabu ambayo ni taifa la Kiislamu mwaka 1979 yaliyomuweka katika himaya Ayatollah Khomeini, wawili hao walikuwa ni marafiki wa kufa mtu. Enzi hizo, Iran ilikuwa ni ardhi pekee kati ya mataifa yote ya Kiarabu, ambayo yaliruhusu ndege za Israel kutua!
Leo, unapoitaja Iran mbele ya Israel ni sawa na uhai na kifo. Ni maadui ambao kila mmoja anatamani mwenzake ateketee mara moja. Lakini Primor, licha ya kusema hakuna adui wala rafiki wa kudumu katika siasa, aliongeza kuwa kilicho cha kudumu kwa wanasiasa ni masilahi yao!
Hilo ndilo tunalolishuhudia leo baada ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa anapokuwa sehemu ya jeshi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kwa miaka mingi, kimemtaja kama mmoja wa mafisadi wanaostahili kuogopwa katika nchi hii.
Mwaka mmoja kabla hajajiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, Lowassa alikuwa mmoja wa viongozi 11 waliotajwa na Dk. Willbroad Slaa kuwemo katika orodha ya mafisadi iliyojipatia umaarufu kama List of Shame.
Katika orodha ya watu hao waliotajwa, wapo wengine ambao pia wamehusishwa katika kashfa nyingine zilizohusu uporaji wa mabilioni ya shilingi za umma kwa kutumia nafasi zao za kiuongozi walizopata kuzishikilia siku za nyuma au hadi sasa wakiwa katika ofisi za umma.
Akiwa serikalini, tangu enzi za Rais William Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, Lowassa alikuwa mmoja wa viongozi wa juu waliokuwa wakitoa maneno mengi ya kejeli, kashfa na dharau kwa vyama vya upinzani vilipojaribu kwa namna yoyote, kuhatarisha neema za wakubwa wa chama na serikali.
Na Chadema, kimejipatia umaarufu mkubwa kwa jamii ya wanyonge baada ya kuonesha kuwa ni chama chenye nia ya kupambana na ufisadi na kutowajibika kwa viongozi wa umma, kiasi kwamba idadi kubwa ya wafuasi wake ni watu waliokata tamaa na ambao kwa namna moja au nyingine, hawafaidiki moja kwa moja na uwepo wa CCM madarakani.
Uadui wa wawili hawa umemalizika. Leo Chadema wanamtaja Lowassa kama mchapakazi aliyeathiriwa na mfumo wa kifisadi ndani ya CCM na mbunge huyo wa Monduli, anaamini chama chake kipya ndicho pekee kinachoweza kuwaondoa marafiki zake wa siku nyingi madarakani.
Uadui na urafiki unaweza kumalizika wakati wowote, lakini masilahi ya wanasiasa daima huwa ya kudumu. Lengo la Chadema (Ukawa) ni kushika dola, bila kujali inashirikiana na nani na ndivyo pia ilivyo kwa Lowassa, kwamba hamu yake ni kukalia kile kiti cha enzi pale magogoni, bila kujali anafikaje.
Nia yangu hapa ni kujaribu kuwaweka sawa wafuatiliaji wa safu hii, kama nilivyopata kuwapa dokezo wiki iliyopita kuwa wanatakiwa kuwa macho sana na wanasiasa kwa sababu hawaaminiki.
Wanachokisema hakitoki ndani ya mioyo yao, isipokuwa kinatokana na wakati wenye kuhusisha masilahi yao.
Kwa kuwa Lowassa ana watu wengi nyuma yake wanaoweza kuwasaidia Ukawa wakaingia Ikulu, hawana shida kuungana naye, hata kama miongoni mwao, watakuwa ni walewale waliotajwa Septemba ile, pale uwanja wa Mwembeyanga, mwaka 2007.
GPL
1 comment:
Siasa ni nini?
Kwenye malumbano ya siasa kuna michezo michafu na michezo misafi.
Michezo Michafu:
- Kejeli na sifa mbaya za mpinzani ili kuelekeza mawazo ya wapiga kura kwako
- Kuangalia mabaya ya mpinzani hata kama hayajahakikishwa ili kupunguza kasi
- Kumuhusisha mpinzani na watu au maamuzi mabaya ili kuwatoa wengine kumfikiria ni mtu mwema
- Ukweli na uongo ni sehemu ya mapambano katika siasa
Michezo Misafi:
- Kutangaza sera zako na kuzilinganisha na maisha ya wananchi
- Kujihusisha na watu wenye sifa nzuri kwenye jamii ili kupata picha nzuri
- Kujali wataokupigia kura kuonyesha upendo wa aina yoyote
- Kuwaonyesha watu picha za mafanikio ukichaguliwa...
Na mengine mengi. Ukiijua siasa haikusumbui na sio wengi wanajua siasa hususani wale wataopiga kura. Elimu ya aina yeyote ni ya muhimu sana kwenye siasa.
Karibu ulingoni mwa siasa!! Jifunze siasa!!
Post a Comment