Advertisements

Thursday, July 30, 2015

Lowassa, Ukawa uamuzi mgumu

By Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza kuhama CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema pande hizo mbili zimefanya uamuzi mgumu ambao utanufaisha kila upande.

Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema uamuzi huo wa Lowassa ambaye alitangaza kujiunga na Chadema na kufafanua kuwa amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza safari ya matumaini ni uamuzi mgumu.

Alisema: “Lowassa amefanya uamuzi mgumu kutoka CCM lakini hata wapinzani wamefanya uamuzi mgumu kumpokea.”

Alisema sababu kubwa ya Chadema kukubali kumpokea Lowassa ambaye leo anatarajiwa kuchukua fomu kuwania urais, wakati ilikuwa inamtuhumu kwa ufisadi inatokana na mwanasiasa huyo kuwa na watu wengi wanaomuunga mkono, hali ambayo itaibua ushindani mpya katika siasa nchini.


Ni faida zaidi

Profesa Mpangala alisema pamoja na Lowassa kutuhumiwa na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa kwa ufisadi, uwepo wake ndani ya umoja una faida zaidi kuliko hasara.

“Faida ya Lowassa kwenda Ukawa ni kubwa zaidi kuliko hasara ya kuendelea kumpinga na kumtuhumu kwa ufisadi. Ukawa wanatambua kuwa uwepo wa Lowassa utawapa kura nyingi katika uchaguzi ujao,” alisema.

Profesa huyo alisema si jambo la ajabu kwa mwanasiasa kuhama chama, huku akitolea mfano mwaka 1995 jinsi Augustine Mrema alivyohama CCM kwenda NCCR kuwa,

“Kama si nguvu ya Mwalimu Julius Nyerere pengine angekuwa rais,” alisema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema katika siasa kinachotazamwa zaidi ni nafasi, na kwamba katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu.

“Ila ujio wa Lowassa Chadema lazima utazamwe, ni lazima chama hiki (Chadema) kimtazame kiongozi huyo anakuja na kitu gani? Pia, CCM nao hata kama hawatasema wazi, lakini kuondoka kwa Lowassa kutawatikisa kidogo,” alisema.


Dk Malya alisema Lowassa alikuwa kiongozi katika Serikali iliyoundwa na CCM, hivyo ni lazima aeleze kilichomshinda kukifanya wakati huo na sababu za kutaka kuyafanya yaliyomshinda akiwa ndani ya Ukawa.

Mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema: “Ukitazama kwa makini utagundua kila mmoja anambeba mwenzake, yaani Lowassa anaibeba Chadema na Ukawa na wao pia wanambeba yeye.”

Alisema kama waziri mkuu huyo wa zamani atagombea urais kwa tiketi ya Chadema ni wazi kuwa mpambano utakuwa mkali kati yake na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kwa maelezo kuwa kuna baadhi ya mambo wanaendana.

“Mtaji wa chama cha siasa ni watu na lengo kuu ni kuongoza nchi. Hakuna adui wa kudumu katika siasa. Kilichotokea ni jambo la kawaida tu ila tu watu wamestushwa maana hawakutegemea Lowassa kuwa atakihama CCM,” alisema.

Lissu: Kwanini tumemkubali

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ametaja sababu mbili za Ukawa kumkaribisha Lowassa kuwa mgombea urais wakati chama hicho kilimtaja katika orodha ya mafisadi mwaka 2007.

“Edward Lowassa ni mwanasiasa asiyeeleweka na aliyewagawa watu zaidi kwa sasa katika siasa nchini na amekuwa hivyo kwa muda mrefu. Sisi Chadema tulimweka kwenye orodha ya mafisadi kutokana na kuhusika kwake na kashfa ya Richmond mwaka 2007. Kwa hiyo swali halali kabisa ambalo lazima tulijibu kwa ufasaha ni hili: ‘Kwa nini tumemkubali, siyo tu kumpokea kama mwanachama, bali kumpa heshima ya kuwa mgombea wetu wa urais? Na kwa nini washirika wetu wa Ukawa nao wamemkubali kuwa mgombea wao wa urais?

“Jibu ni kwamba tupo katika kipindi na mazingira ya kipekee ya kisiasa katika nchi yetu. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu kama Taifa, tunaona mfumo tawala ukipasuka vipandevipande. Kwa mara ya kwanza tunaona CCM ikipasuka katikati, na mtu aliyeipasua CCM na mfumo tawala ni Edward Lowassa.

“Sisi Chadema tumefanya kazi kubwa ya kujenga chama tangu 2010. Tuna wagombea wengi na bora katika majimbo mengi ya uchaguzi na ngazi ya madiwani kuliko ambavyo tumewahi kuwa nao kwa miaka yote ya nyuma.

“Hata hivyo, ni ukweli pia kwamba kuna maeneo mengi ya nchi ambako tuko dhaifu sana. Kwa kuingia kwake Chadema na Ukawa, Lowassa anayaingiza maeneo hayo kwenye ulingo wa kisiasa na sisi kuyafikia.

“Na Lowassa ataiporomosha CCM kwa sababu ana nguvu kubwa ndani ya chama hicho kuliko mwanasiasa mwingine yeyote. Katika mazingira ya sasa ya kipekee, tunahitaji kuamua nani ni adui mkubwa zaidi wa nchi yetu na ustawi wake; Edward Lowassa mtuhumiwa wa ufisadi au CCM na mfumo tawala ambao unajenga mazingira yanayostawisha na kulinda ufisadi?

“Sisi Chadema na Ukawa tumeamua kuwa adui yetu mkubwa wa sasa na siku zote ni CCM na mfumo tawala.

Tumemkaribisha Edward Lowassa kwa sababu kuwapo kwake kutaharakisha kuiangamiza CCM na mfumo tawala. Tunaomba wananchi mtuelewe na kutuunga mkono?

Kwa nini Dk Slaa hakuonekana

Katika mkutano wa kumtambulisha Lowassa, baadhi ya viongozi waandamizi wa Chadema hawakuhudhuria, kitendo kilichofafanuliwa jana kuwa walikuwa na majukumu mengine kichama.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba viongozi hao wamechukizwa na uamuzi wa chama hicho kumkubali Lowassa ajiunge Chadema, si za kweli.

Viongozi ambao hawakuonekana katika mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Bahari Beach ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Naibu wake (Bara), John Mnyika na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.

“Kama mnavyojua kwa sasa kuna mambo mengi yanaendelea nchini likiwamo suala la uandikishaji wa wananchi katika daftari la wapigakura,” alisema Mwalimu huku akifafanua kuwa mchakato huo ni moja ya mambo yanayofuatiliwa kwa ukaribu na viongozi wa Chadema.

“Mbona suala hili mnataka kulikuza sana. Ni kitu cha kawaida Chadema ni chama kikubwa na viongozi wake wana shughuli nyingi za kufanya,” alisisitiza.

“Jana, (juzi) Dk Slaa hakuwapo wala Lissu, lakini katika mkutano wa leo (jana) Lissu kaja Dk Slaa hajaja. Na hata leo (jana) Mbowe ambaye tulikuwa naye jana leo hayupo. Kwa hiyo ni suala la utaratibu tu na si kila tukio lazima tuwe wote,” alisema.

Kuchukua fomu

Katika hatua nyingine, Mwalimu alisema leo Lowassa atachukua fomu za kuomba ridhaa ya kuwania urais kupitia Chadema katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam.

“Atachukua fomu kesho (leo) na kutakuwa na shamrashamra za aina yake,” alisema.

Kingunge, Sophia wajitenga

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba wametoa kauli zinazoashiria kujitenga na uamuzi wa Lowassa kuondoka CCM.

Simba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), alisema bado ni mwanachama wa CCM na kuwa uamuzi wa Lowassa ni wa mtu binafsi.

“Mimi haunihusu, bado ni mwanachama wa CCM, tafadhali msinisumbue,” alisema.

Simba, pamoja na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu ya CCM; Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi na Adam Kimbisa waliitisha mkutano wa waandishi wa habari kuipinga kamati hiyo kwa kulikata jina la Lowassa katika mchakato wa kumpata mgombea wa urais.

Aidha, Kingunge ambaye wakati wa kusaka wadhamini katika mchakato wa awali wa urais ndani ya CCM alijitokeza hadharani kumuunga mkono Lowassa alisema hatua yake ya Mbunge huyo wa Monduli kuhamia Chadema ni uamuzi binafsi hivyo hawezi kuutolea maoni yoyote.

“Kama ameondoka, basi anatakiwa aulizwe yeye na wala si mimi kwa sababu kila mtu ana maamuzi yake binafsi,” alisema.

No comments: