Advertisements

Thursday, July 30, 2015

MKE MATUNZO, NI SAWA NA MGOMBA KUPALILIWA!


Assalaam alaikum/Bwana Yesu asifiwe! Bila shaka mna afya njema wasomaji wangu. Kikubwa mjue naendelea kuwapenda, kuwathamini na kuwaheshimu kwani mmekuwa mkionesha kukubali kile ambacho nakiandika kupitia safu hii.

Baada ya kuwavalia njuga wanawake kwa muda mrefu, leo niwageukie wanaume hasa ikifahamika kwamba, hakuna aliyekamilika isipokuwa Mwenyezi Mungu tu.

Ndiyo maana leo nimeamua kuwasema wanaume kwa sababu nao ni miongoni mwa watu ambao hawajakamilika na wanastahili kukumbushwa baadhi ya mambo ili ndoa zao ziwe tamu, au siyo jamani?
Ujumbe mwingi ninaopokea kutoka kwa wanaume umenifanya nigundue kuwa wengi wenu mna kasoro na mnatakiwa kuzifanyia kazi ili kulinda ndoa zenu.


Hivi mnafahamu kitu muhimu kwa mwanamke ni suala la kuhakikisha amekula, amepata nguo nzuri na burudani faragha?

Wengi wa wanaume hawalijui hilo kabisa kwani wanadhani mwanamke akishapewa burudani ya ndoa inatosha, wanasahau kuwa kuna umuhimu wa kuhakikisha anapendeza na anakula vizuri pia.

Kuna wanaume kazi yao kuwasifia wake za watu bila kujua kuwa hata mkeo ukimjali atakuwa na mvuto na atasifiwa. Yaani mkeo tangu umemm-nunulia nguo ya harusi ndiyo imetoka, hata siku moja hujawahi kumnunulia hata leso, hujawahi kumpa ‘kijihela’ angalau akanunue nguo.

Huna mawazo ya kumpa hata pesa akanunulie ‘vijiurembo’ ili angalau akipita mbele za watu aonekane ni mke wa mtu anayethaminiwa. Hilo ni tatizo kwenu wanaume.Matunzo hamtoi inavyotakiwa, tena wengine wanajiangalia wao tu. Hivi unajisikiaje pale unapojipendezesha wewe tu wakati mkeo anaonekana yupo yupo tu? Badilikeni jamani, tena nasisitiza mbadilike!

Nimetoleo mfano mgomba kwamba unastahili kupaliliwa na kumwagilia ili uweze kukua vizuri. Vivyo hivyo kwa mkeo. Ili aonekane amependeza, hilo jukumu unalo wewe mume! Usitarajie eti kwa kuwa anajishugulisha basi ajipendezeshe mwenyewe, hiyo ni sawa kweli?

Hatukatai mke kujinunulia nguo, urembo na vitu vingine lakini je kama hana uwezo wa kufanya hivyo afanyeje? Wewe ulipoamua kumuoa si ulijiaminisha kwamba utaweza kumtunza? Sasa mbona humjali na kumtuza ipasavyo?
Wanaume wenye hiyo tabia badilikeni na mchukue majukumu yenu kama waume. Kama huna uwezo, hata mkeo hatakuwa ananung’unika kwani anajua uwezo haupo. Lakini kazi unafanya na pesa unapata kisha hujishughulishi kwa namna yoyote kumfanya mkeo avutie. Hiyo siyo sawa!

Nasikia wapo ambao wanasema eti wakiwapendezesha wake zao wataibiwa, jamani hizo ni dhana potofu! Mkeo kupendeza ni lazima, hilo la kutongozwa liweke kando. Hivi hujui kwamba wanaume ambao hawatunzi wake zao ndiyo wanaongoza kwa kusalitiwa?

Kaa chini na ujiulize wewe mwanaume kwamba, kama mkeo anakula kwa tabu, anavaa kwa shida na hata ile burudani ya faragha anaipata kwa mwezi mara moja tena kwa kulazimisha, utakuwa unamfanyia sawa?

Mwanaume unarudi ndani alfajiri je vile vikuba na asmini mkeo alivyofunga atafunguliwa na nani? Bila shaka mnajua kuwa vionjo hivyo hufunguliwa kwa meno tena na mume mwenyewe ambaye anakuja kumpa burudani mkewe, sasa itakuwaje wewe unayerudi alfajiri ni saa ngapi utafanya hivyo?

Mwanamke anakuwa na hamu na mumewe, akae naye wanywe, wale chakula alichomuandalia lakini atafanya hivyo saa ngapi wakati wewe unarudi usiku?

Ukiulizwa kwa nini unachelewa utasikia kelele za watoto, hivi mkeo ametoka nao kwao au amewapatia kwako? Kwa nini umnyime nafasi mkeo kisa watoto ambao wewe umechangia yeye kuwapata?

GPL

No comments: