Advertisements

Thursday, July 30, 2015

Mwandosya aibua mazito urais CCM.

Mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeendelea kuibua mapya na kuleta mvutano baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, kunukuliwa akisema kuwa majina matano yaliyopelekwa kwenye Kamati Kuu ya CCM (CC) kutoka kwenye Kamati ya Maadili yalijulikana hata kabla ya kikao cha Kamati ya Maadili hakijaketi.

Prof. Mwandosya ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki amenukuliwa akisema hayo kwenye sauti yenye maelezo yake iliyorekodiwa na kusambazwa katika mitandao mbalimbai ya kijamii.

Akizungumza na NIPASHE kwa simu akiwa uwanja wa ndege jana ambao hata hivyo hakuutaja wala alikokuwa akienda, Prof. Mwandosya alisema amepata taarifa za kusambazwa kwa sauti hiyo lakini hafahamu kama yanayozungumzwa humo ni ya kwake.

Prof. Mwandosya alisema anachokumbuka akiwa kijijini kwao Lufilio wilayani Rungwe aliitwa na wazee na kufanya nao mkutano wa ndani wakitaka kujua nini kilichojiri wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais CCM.

“Niliitwa na wazee kwenye mkutano wa ndani wakitaka kujua nini kimetokea na inawezekana yaliyomo ndani ya hiyo clip yana ukweli, lakini wewe unadhani nilichokisema ni uongo?, Si kinalingana na hali halisi ilivyokuwa Dodoma,” alisema.

Hata hivyo, alisema taarifa zilizosambazwa kwamba anataka kuhamia Chadema siyo za kweli.

Katika sauti iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Prof. Mwandosya amenukuliwa akisema kuwa majina ya makada walioingia tano bora katika kinyang’anyiro cha urais yaliyopelekwa Kamati Kuu yalijulikana hata kabla ya kikao cha Kamati ya Maadili hakijaketi.

Alisema Mwenyekiti wa Kamati Kuu, Rais Jakaya Kikwete, alikuwa na majina yake matano mfukoni na kamati yenyewe pia ilikuwa na majina yake.

Akizungumzia madai hayo, Prof. Mwandosya alithibitisha kuwa madai hayo ni ya kweli na kwamba wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa CCM waliokuwapo Dodoma wanalijua hilo.

“Hapo mimi sioni kwamba kuna jambo ambalo limepotoshwa, kwani yote yanayosemwa ni ya kweli na hata wajumbe wote waliokuwa Dodoma kwenye Mkutano Mkuu wanayajua vizuri mambo hayo,” alisema Prof. Mwandosya.

Alisema ingawa hajaisikia sauti inayodaiwa kuwa ni yake, lakini kama ni suala la kusema kuwa mgombea urais mteule wa CCM, Dk. John Magufuli hajawahi kuwa hata mwenyekiti wa tawi la CCM ni kweli.

Alizidi kueleza kuwa, anaona ni sahihi kwa sababu katika kumbukumbu zake hajawahi kusikia wala kumwona Dk. Magufuli akiwa Mwenyekiti wa Chama katika ngazi yoyote.

“Nina kazi nyingi sijafungua mitandao ya kijamii kwa muda mrefu kidogo, lakini kama mambo yanayosemwa ni hayo, sioni kama kuna uongo ndani yake, ningepata shida sana kama mambo yanayozungumziwa yangekuwa siyo ya kweli, katika kumbukumbu zangu sijawahi kusikia Dk. Magufuli amekuwa Mwenyekiti wa Chama au Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama, lakini sasa ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa Chama chetu nadhani hilo liko wazi,” alisema.

Akizungumzia uamuzi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Prof. Mwandosya alisema kuwa Lowassa ametumia haki yake ya kidemokrasia na yeye haoni kama kwa uamuzi huo amefanya kosa lolote.

Alisema vyama vya siasa ni sawa na madhehebu ya dini, ambapo waumini wanayo haki ya kwenda kuabudu katika kanisa wanalolitaka au ambalo imani yao inawatuma na hakuna mtu wa kuwapokonya haki hiyo.

“Alichokiamua Lowassa sidhani kama ana kosa, kwani anayo haki na uhuru wa kufanya alichokifanya, siku hizi kuna makanisa mengi, mtu anapoamua kwenda kuabudu katika kanisa analoona linamfaa huwezi kusema kuwa amekosea, labda ninachoweza kushauri ni CCM kujiuliza sababu za Lowassa kuondoka na ikiwezekana ijisahihishe ili watu wengi zaidi wasiondoke,” alisema.


Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe; Dar na Emmanuel Lengwa, Mbeya
CHANZO: NIPASHE

4 comments:

Anonymous said...

UONGOZI HUTOLEWA NA MUNGU WAPENDWA, HATA KAMA HAJAWAHI KUWA MJUMBE, MUNGU AMEMCHAGUA KUWA NDIYE ATAKUWA RAIS WA WATANZANIA. TUSUBIRI OCTOBA 25. YAANI MUNGU ANASEMA SISI TUTAKAA KIMYA NA MUNGU ATATUPIGANIA. NI NANI ALIYEJUA KWAMBA MAGUFURI ATAKUWA RAIS? KAMA SIYO MIPANGO YA MUNGU? MIE NAONA TUMWACHIE MUNGU AFANYE SEHEMU YAKE. TUACHE MALUMBANO, HAYANA TIJA.

Anonymous said...

NABII YOSIA alikuwa mtoto mdogo saana, lakini Mungu alimtumia kuwa nabii akiongoza watu wakubwa tena wenye kumzidi umri, lakini Mungu alimpatia hekima kama za akina sureiman, msijali kwamba hakuwahi kuwa mjumbe wa shina. Mungu wetu huyu tunayemfahamu ana kila sababu na magufuri. Dunia na inyamaze.

Anonymous said...

No mdau hapo juu umechemka Mungu wetu anania na Lowasa ndio maana kahamia huku kwa watetezi (Ukawa) tangia 1961 ccm tuu tumechoka na manyanyaso na maendeleo ya kuliibia taifa

Anonymous said...

Semeni yote. Tangu imetoka chuoni ulikuwa so productive pale, sasa tangu umekaa sirikalini umefanya nini?