ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 13, 2015

Ulinzi waimarishwa kwa Magufuli

Polisi wakiimarisha ulinzi karibu na nyumbani kwa mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli chato mkoani Geita baada ya kutangazwa kugombea nafasi hiyo mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma jana. Picha na Baraka Rwesiga

Chato/Dar. Saa chache baada ya Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mteule wa CCM kuwania urais, ulinzi umeimarishwa kwa mgombea mwenyewe, nyumbani kwake eneo la Ada Estate, Dar es Salaam na jimboni Chato mkoani Geita.
Muda mfupi baada ya kuwapo taarifa kuwa Magufuli anaongoza kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu, aliongezewa ulinzi usiku huo na hadi jana muda wote, alionekana akiwa na walinzi watano.
Jimboni Chato, nyumbani kwake eneo la Rubambambangwe, polisi walionekana wakitanda tangu jana asubuhi tofauti na siku nyingine.
Askari hao wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mkama walionekana nyumbani hapo tangu asubuhi hata kabla matokeo yaliyompa ushindi Dk Magufuli  hayajatangazwa.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikwenda nyumbani kwa Dk Magufuli kuzungumza familia yake, hakuruhusiwa na polisi waliokuwa kwenye lango kuu la kuingilia, walidai wamepewa maelekezo ya kutoruhusu watu kuingia.
“Naomba usiingie ndani wala kupiga picha eneo hili, hayo ndiyo maelekezo ninayokupa na niliyopewa, vinginevyo mtafute RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) akupe ruhusa,” alisema mmoja wa askari hao. Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema polisi walikuwa wanatekeleza jukumu lao kwa umma la kulinda raia na mali zao kutokana na wananchi kwa makundi kusherehekea ushindi wa mteule huyo.
Konyo alisema ulinzi huo ulilenga kuweka na kuimarisha usalama kwenye makazi ya familia hiyo.
Hata hivyo, Konyo alipotakiwa kuzungumzia kuzuia watu kupiga picha kwenye makazi hayo alikata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.
Nyumbani kwake, Ada Estate, ulinzi ulianza kuimarishwa mara tu baada ya kiongozi huyo kutangazwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mmoja wa walinzi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema wameongezwa walinzi wengine wanne mara baada ya matokeo ya mjini Dodoma kutangazwa.
Magari kadhaa yenye namba za serikali na magari ya polisi yalionekana yakiingia na kutoka nyumbani kwa Magufuli.
Kadhalika kama ilivyokuwa Chato, walinzi hao walisema wamepewa amri kutoruhusu watoto au mwanafamilia yeyote kutoka nje au kuzungumza na waandishi wa habari.
Majirani wanena
Baadhi ya majirani walimtaja mke wa Magufuli, Janeth  Magufuli kuwa ni mtu asiye na makuu na anayechangamana na wengine katika masuala ya kijamii.
Mmoja wa majirani hao, aliyejitambulisha kwa jina la Yahya alisema Janeth ni jirani mnyenyekevu na mkimya ambaye anashiriki mambo mengi ya kijamii katika eneo hilo la Ada Estate.
“Ukikutana naye hutajua kama ni mke wa waziri, mkimya, wakati mwingine anaenda zake mazoezi, anasali jumuiya na wala hana neno na mtu,” alisema.
 Jirani mwingine, Josephina Murungu alikuwa na maoni tofauti juu ya familia ya Magufuli akisema kutokana na hadhi yao, ni vigumu kuwaomba kiberiti au chumvi.
“Siku zote watu matajiri huwezi hata kuwaomba chumvi, wala kibiriti, ndiyo maana tunashindwa kuwa nao karibu, si kama majirani wengine, kwa kifupi tunawaogopa,” alisema.
 Jirani mwingine Sayuni Msungwa, anayesali nao kwenye Jumuiya na Janeth, alisema wamezoea kukutana kwenye maombi na anamwona  ni mwanamke asiye na makeke wala kupenda kujikweza.
“Ukikutana naye kwenye jumuiya anaonekana mpole sana, huwa namsalimia na ananijibu kwa unyenyekevu, siyo wa kuvaa mavazi ya gharama au vidani, walaaa… mpole tu,” alisema.
Chato wamzungumzia
Baadhi ya wakazi wa mjini Chato, walisema Mkutano Mkuu wa CCM umetenda haki na Dk Magufuli ndiyo chaguo la Watanzania.
Kada wa CCM, Steven Kasika alisema ana imani kubwa na Dk Magufuli hivyo kuchaguliwa kwake si tu kwamba atawarejeshea matumaini wananchi na wanachama wa chama hicho, bali pia wapinzani watamuunga mkono kwa sababu anao uwezo wa kuongoza nchi.
George Mpanduji ambaye ni Katibu wa Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (Tacoga), alisema kuchaguliwa kwa Dk Magufuli kutaisaidia CCM kushinda na kuinusuru sekta ya kilimo.
Mkurugenzi wa Shule ya Emmau English Medium mjini Chato, Onesmos Nyaruba alisema matumaini yake kwa mteule huyo ni makubwa hasa kurejesha imani ya wananchi kwa CCM, ambayo walikuwa wameipoteza.
“Magufuli ni mwajibikaji hivyo mwisho wa mafisadi umefika, atawawajibisha wote waliojilimbikizia mali kinyume na misingi ya chama chake,” alisema Nyaruba.
MWANANCHI

No comments: