ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 9, 2015

JESHI LA MAGEREZA LAIBUKA MSHINDI WA JUMLA MAONESHO YA WAKULIMA NANE NANE KIKANDA TAASISI ZA MAJESHI YA ULINZI NA USALAMA

Mkuu wa Magereza Mkoani Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Antonino Kilumbi akiwa ameshika vikombe vya ushindi katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati kwa Mwaka 2015. Wengine ni Maafisa Washiriki wa Jeshi la Magereza wa Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane Kanda ya Kati, Dodoma.

Jeshi la Magereza nchini limeibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika katika Kanda ya Kasikazini(Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara), Kanda ya Magharibi(Mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es Salaam) pamoja na Kanda ya Magharibi(Mikoa ya Tabora, Kigoma na Shinyanga) ambapo Jeshi la Magereza limeibuka kidedea katika upande wa Uzalishaji Taasisi za Serikali pamoja na Taasisi za Serikali upande wa Teknolojia na Maonesho Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Jeshi la Magereza ni Miongoni mwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwa na jukumu lake la kuwahifadhi na kuwarekebisha Wafungwa wa aina mbalimbali wawapo Magerezani ili pindi wamalizapo vifungo vyao waweze kuwa raia wema katika jamii. Pia hushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nane Nane Kitaifa na Kikanda kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kupitia shughuli zake mbalimbali za uzalishaji katika Sekta za Kilimo na Mifugo.

Mbali na ushindi huo wa Kikanda, Jeshi la Magereza limeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa(Maarufu kama Nane Nane) katika Mkoa wa Lindi ambapo Jeshi hilo limeibuka Mshindi wa Pili kwa upande wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Kilele cha Maonesho hayo huku Jeshi la Kujenga Taifa likibuka Mshindi wa Kwanza wa Jumla na Mgeni rasmi katika Kilele cha Maonesho hayo Kitaifa alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kutokana na Ushindi huo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja amewapongeza Maafisa na Askari wote walioshiriki kikamilifu katika Maonesho hayo hadi kufanikisha ushindi huo na amewapa changamoto ya kuongeza bidii zaidi katika utendaji wao wa majukumu ya kazi ili katika Maonesho yajayo waweze kufanya vizuri zaidi.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Jeshi la Magereza kuibuka Mshindi wa kwanza kwa upande wa Taasisi za Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika Kikanda hapa nchini tangu Mwaka 2013.

Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kitaifa yamefunguliwa rasmi Agosti 04, 2015 na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Pinda ambapo kauli
mbiu ya Mwaka huu ni "Matokeo Makubwa Sasa" - Tuchague Viongozi Bora kwa Maendeleo
ya Wakulima na Wafugaji.

Imetolewa na Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Lucas Mboje,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Agosti 08, 2015.

No comments: