ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 16, 2015

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD AKUTANA NA WAGOMBEA WA CUF - PEMBA


Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na viongozi pamoja na wagombea wa chama hicho katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Kisiwani Pemba.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na mgombea uwakilishi wa CUF Jimbo la Ole baada ya kutambulishwa kwa wagombea rasmi wa Ubunge na Uwakilishi.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Ismail Jussa Ladhu, akizungumza na viongozi pamoja na wagombea wa chama hicho katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Kisiwani Pemba.

Na: Hassan Hamad (OMKR)
Chama Cha Wananchi CUF kimesema kimejipanga vyema ili kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinapata taarifa za kuwaeleza wananchi kuhusiana na chama hicho kuanzia ngazi za majimbo.
Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kupitia timu za ushindi wa chama hicho kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu ujao, chama hicho kitatoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ngazi zote kuanzia ngazi ya majimbo, Wilaya hadi Taifa.
Amesema lengo la hatua hiyo ni kuondosha urasimu wa upatikanaji wa habari ndani ya chama hicho, ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa zinazokwenda na wakati kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Maalim Seif ameeleza hayo katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro kisiwani Pemba, wakati akizungumza na viongozi pamoja na wagombea wa chama hicho kwa majimbo 18 ya Pemba.
Amefahamisha kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na chama hicho, kamati tendaji za Taifa, Wilaya na Majimbo sasa zinageuka kuwa timu za ushindi, na kuwataka wajumbe wa kamati hizo kufanya kazi kwa mashirikiano ili kuhakikisha kuwa wanakipatia ushindi mkubwa chama hicho.
Amefafanua kuwa Chama hicho hakitokuwa na muhali kwa mtendaji yeyote atakayekiuka maadili ya Chama, na kuwaagiza viongozi wa Wilaya na Majimbo  kuwa makini na kuwawajibisha watendaji watakao zembea.
Wakati huo huo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Ismail Jussa Ladhu amesema wakati chama hicho kikijiandaa kuchukua fomu za uteuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, hakitotoa barua kwa mgombea yeyote aliyeshindwa kulipa madeni yake ndani ya chama hicho.
Amesema Chama hicho hakitokuwa na muhali na jambo hilo, na iwapo mgombea atashindwa kulipa madeni hayo, Kamati tendaji Taifa inaweza kuteua mgombea mwengine wakati wowote.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kudumisha nidhamu ndani ya chama hicho na kuwafanya wanachama kuwa na imani na viongozi wao.
Chama hicho tayari kimetangaza timu yake ya kampeni kwa upande wa Zanzibar inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akisaidiwa na Mansoor Yussuf Himid, ambapo kwa upande wa Pemba kampeni za Urais wa Zanzibar kupitia Chama hicho zitaratibiwa na Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa Mhe. Hamad Massoud Hamad akisaidiwa na Waziri wa Habari Mhe. Said Ali Mbarouk.
Aidha chama hicho cha CUF kimekabidhi seti 40 za jezi na mipira 120 kwa kila jimbo kati ya majimbo 18 ya Pemba na kukamilisha utaratibu wake wa kutoa vifaa kama hivyo kwa majimbo yote 54 ya Zanzibar.

No comments: