Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefuta mzizi wa fitina kuhusiana na tishio la kuzuiwa kufanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kesho kwa kuwataka wajitokeze siyo kwa maelfu bali kwa mamilioni.
Akizungumza katika kongamano la kina mama lililoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema mgombea wao, Edward Lowassa na mgombea mwenza, Juma Dunia Haji, watahutubia mkutano huo kesho na hivyo akawataka wananchi kujitokeza kwa wingi ikiwa ni ishara ya kuelekea mabadiliko ya uongozi katika nchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
“Tulikuwa tunawekewa mizengwe kutumia viwanja vya Jangwani. Na sasa napenda kuchukua fursa hii kuwaalika Watanzania wote kuwa mjitokeze kwa mamilioni kwenye viwanja hivyo na siyo maelfu kwa kuwa mkutano wetu wa kuzindua kampeni utakuwapo siku ya Jumamosi kama ulivyokuwa umepangwa,” alisema.
Aliwataka kina mama wa Jiji la Dar es Salaaam kujitokeza kwa wingi kwa kuwa wasiwasi wao wa kuogopa msongamano wa watu hautakuwapo kwani kuanzia katika mkutano huo (wa Jangwani), Ukawa watakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya kina mama ili wasichanganyikane na wanaume wala kusukumwa.
Mbowe alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na mkanganyiko wa taarifa kuhusiana na matumizi ya viwanja hivyo vya Jangwani kesho kwani kabla ya hapo, Manispaa ya Ilala iliiandikia barua Chadema kuizuia kutumia viwanja hivyo kesho kwa madai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishaomba kuvitumia tena.
Zuio hilo la manispaa lililotokana na barua iliyosainiwa na Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Ilala, Claud Mpelembwa, iliyoandikwa Agosti 25 na kuwa na kumbukumbu namba IMC/UT/M/V0L.11/414. Lilipingwa na viongozi wa Ukawa waliodai kuwa hiyo ni hujuma ya wazi dhidi ya mgombea wao, Edward Lowassa, kwani CCM ilishazindua kampeni zake kwenye viwanja hivyo Jumapili iliyopita.
Hata hivyo, wakati Mbowe akihamasisha wananchi kujitokeza kwa mamilioni kesho ili kuhudhuria kampeni za chama hicho, Mpelembwa hakuthibitisha taarifa hiyo jana na badala, akidai kuwa bado hajapata taarifa za kuwapo kwa mabadiliko.
“Sina taarifa kama ratiba za matumizi ya viwanja hivyo imebadilika,” alisema Mpelembwa.
Hata hivyo, ofisa mwandamizi wa CCM aliiambia Nipashe jana kwa sharti la kutoandikwa jina lake kuwa, chama chao kimeamua kuwaachia Ukawa kutumia viwanja vya Jangwani, lakini wana uhakika kuwa kampeni zao zitakazokuwa jijini Mbeya ndizo zitakazorushwa na vituo vingi vya televisheni nchini kesho kwa vile walishaomba nafasi na kulipia.
LOWASSA ANENA
Akizungumza katika kongamano la Bawacha jana, Lowassa alisema kuwa katika uzinduzi wa kampeni kesho, kuna vigogo zaidi wa CCM watajiunga na upinzani.
“Nawaambia waliobaki CCM waje kwenye mabadiliko na huku hakuna noma, kuna maendeleo... njooni mjiunge na gurudumu la maendeleo. Jumamosi mtaona watakuja wengi tu,” alisema Lowassa.
Alisema ifahamike kuwa nguvu ya umma haiwezi kushindwa na kwamba ana matumaini Oktoba 25, mwaka huu Watanzania watampeleka yeye na wenzake Ikulu.
Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 ambacho amekuwa mbunge, wanawake wamekuwa waaminifu sana katika kupiga kura ukilinganisha na wanaume, hivyo anawaomba wafanye kazi moja tu ya kumtafutia kura.
“Nawaomba wanawake mfanye kazi moja tu ya kunitafutia kura, tukimaliza kazi ya kura tutakutana Ngurdoto kuzungumza mambo yenu. Nataka nikae mahali nitafakari kuhusu maendeleo ya wanawake,” alisema na kuongeza kuwa atakapofanikiwa kuingia Ikulu anakusudia kuleta mabadiliko kwa kasi kubwa.
Awali Katibu Mkuu wa Bawacha, Naomi Kaihula, alisema lengo la kongamano hilo ni kuwaunganisha wanawake pamoja ili washiriki vizuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
REGINA LOWASSA
Mgeni rasmi katika kongamano hilo, Mama Regina Lowassa, alisema kwa kuzingatia kuwa wanawake ni chimbuko la maendeleo, wanatakiwa kufanya mabadiliko ya kweli ili matatizo yanayowakabili yapatiwe ufumbuzi.
JUMA DUNI
Mgombea mwenza, Juma Duni Haji, aliwaomba wanawake kuhakikisha wanashiriki kupiga kura ili kuwawezesha yeye na Lowassa kuingia Ikulu na kuwaahidi kwamba hawatawaangusha.
MAANDALIZI MKUTANO, TISHIO LA UMEME
Mapema jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, aliwaambia waandishi wa habari jijini kuwa walipewa taarifa ya kutumia viwanja hivyo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Alisema mkutano huo unatarajiwa kurushwa moja kwa moja katika vituo vya luninga visivyopungua vinne, lakini hofu yao ni kuhujumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linaloweza kukata umeme katika maeneo mengi ya nchi na kuwakosesha wananchi fursa ya kufuatilia matangazo hayo, kama ambavyo imeshawahi kujitokeza mara kadhaa hapo kabla.
Hata hivyo, Msemaji wa Tanesco, Adrian Severin, alisema hawana ratiba ya kukata umeme na pia akakanusha shirika lao kuwahujumu wapinzani kwa namna yoyote ile na kueleza kuwa kama umeme hukatika, basi huwa ni kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.
“Hakuna ratiba za kukatika umeme mpaka sasa bali kuna kukatika umeme ambako kupo kwenye mpango kazi wa shirika kama kubadilisha nguzo zilizooza na kukata matawi ya miti, hivyo suala la kukata umeme kwa makusudi si la kweli,” alisema Severin.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment