UTANGULIZI
KWAMBA, sisi
wazee wa Tanzania ambao tumewakilisha wazee wenzetu, kutoka mikoa yote nchini,
tuliokutana kuanzia tarehe 24 hadi 26 Juni 2015, hapa Dar es Salaam tumechangia
mawazo yetu katika kuandaa Mkataba huu na kuuridhia. Lengo la Mkataba huu ni
kutambulisha umma wa Watanzania haki zetu, mahitaji yetu na changamoto tunazokumbana
nazo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
KWAMBA, Mkataba huu ni nyenzo ya kuhakikisha kuwa
wagombea wote katika nafasi mbalimbali za uongozi na Serikali kwa ujumla
wanatambua mahitaji yetu na hivyo kuchukua hatua stahiki.
NA
KWAMBA, sisi wazee tumetumikia
Taifa hili katika sekta mbalimbali zilizo rasmi na zisizo rasmi. Na tumekuwa
chimbuko na mhimili wa Taifa letu. Aidha, tumetoka jasho jingi katika
kulifikisha Taifa letu hapa lilipo na bado tunaendelea kutoa mchango wetu. Tulijinyima
sana ili kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu na afya bora ili kujenga
kizazi kitakachoweza kuliendeleza Taifa hili; na sasa tumekuwa wazee.
NA
KWAMBA, pamoja na hayo, sasa tumekuwa
waathirika wakubwa. Wenzetu wanauawa kikatili kwa imani potofu za kishirikina. Tunaathirika
kwa maradhi na kufa kutokana na kukosa matibabu ya uhakika, vipato vya kumudu
gharama za maisha. Hatuna uwakilishi katika vyombo vya maamuzi na hivyo kilio
chetu hakisikiki. Haki na mahitaji ya wazee
hayapewi kipaumbele kutokana na kutokuwepo mfumo wowote wa kutoa
Pensheni jamii kwa wazee wote na pia kukosekana kwa sheria ya wazee.
NA
KWA KUZINGATIA HAYO,
sasa wazee
tunahitaji kulindwa na kuheshimiwa. Tunahitaji kuwekewa mazingira bora
yatakayotufanya tuishi katika utu, usawa na haki na kupata mahitaji ya msingi
kutoka jamii na mamlaka za serikali.Kupitia Mkataba huu, tunahitaji viongozi
watambue umuhimu wa wazee na hivyo kutoa matamko na kuchukua hatua za kulinda haki
za wazee kama zilivyotamkwa katika Mkataba huu ambazo pia zinatambulika katika
Tamko la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Wazee (Na. 46 ya 1991) na mikataba
mingine ya Kimataifa na Kikanda.
SEHEMU YA KWANZA:
HAKI ZA WAZEE
A. Haki za Wazee
1.
Haki ya
Usawa
·
Haki ya
kutobaguliwa.
·
Haki ya
usalama.
·
Haki ya kuishi
maisha bora yenye utu.
·
Haki ya kupata
taarifa zote muhimu, zikiwemo zile zinazohusu wazee na kuelimishwa.
·
Uhuru wa mtu
kwenda atakapo.
2.
Haki ya
Kuheshimiwa
·
Haki ya kupata
heshima na kuthaminiwa na watumishi wa umma pamoja na watu wanaohudumia wazee.
·
Haki ya
kushiriki katika shughuli za kijamii kwa hiari.
B. Haki Kuhusu Huduma, Usalama na Uwakilishi wa
Wazee
1.
Huduma
Muhimu kwa Wazee
·
Haki ya kupata
pensheni.
·
Haki ya kupata
huduma za afya na matibabu bila malipo.
·
Haki ya
kuhudumiwa na wahudumu wa afya ambao wamepata mafunzo maalum kuhusu afya ya
wazee.
·
Haki ya kupata
huduma na usaidizi kutokana na mahitaji maalum.
·
Haki ya kupata
mikopo nafuu.
·
Haki ya kupata
usafiri wa umma bila malipo.
·
Haki ya kufanya
kazi na hivyo kupata kipato.
·
Haki ya kupata
uangalizi na matunzo nyumbani ikiwa mzee hana uwezo wa kufuata huduma.
·
Haki ya kupata
huduma za kisheria bila kulipa au kwa gharama ya Serikali.
2.
Ulinzi na
Usalama
·
Haki ya ulinzi
dhidi ya vitendo vya kubaguliwa, kupuuzwa, kunyanyaswa, kuumizwa au kuuawa.
·
Haki ya
kulindwa dhidi ya kunyang’anywa mali
kama ardhi, nyumba na mali nyingine isipokuwa tu kwa mujibu wa sheria.
·
Haki ya kuishi
katika mazingira ambayo ni salama.
3.
Uwakilishi
na ushiriki
·
Haki ya
kushiriki katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote kupitia uwakilishi wa
wazee.
·
Haki ya
kushirikishwa na kutoa maoni kuhusiana na utengenezaji na mabadiliko ya sera na
sheria zinazogusa wazee.
·
Haki ya
kuanzisha mabaraza maalum ya wazee.
SEHEMU YA PILI:
MASUALA MUHIMU NA HATUA ZA KUCHUKUA
Kama
ishara ya kuheshimu na kulinda haki za wazee na kuhakikisha kuwa haki hizo
zinatekelezwa, sisi Wazee tunahitaji vyama vya siasa na wagombea wa nafasi za
kisiasa katika ngazi zote kuweka katika ilani zao za uchaguzi masuala
yaliyotajwa katika Mkataba huu na kuchukua hatua stahiki kutegemeana na nafasi wanazogombea
na pindi watakapochaguliwa kuhakikisha kuwa masuala haya yanatekelezwa.
1. Pensheni Jamii
kwa wazee
·
Kutoa tamko kwamba
Serikali ina wajibu wa kutunza na kulinda wazee ikiwa ni pamoja na wajibu wa
kuwapa Pensheni Jamii (Social Pension)
kutambua mchango wao katika Taifa.
·
Kwamba wazee
wote kuanzia miaka 60+ wataandikishwa ili kupanga mikakati ya kuwahudumia.
·
Kupanga bajeti
ambayo inajumuisha pensheni jamii kwa wazee wote.
·
Kutoa tamko
kuhusu kuanza pensheni jamii kwa wazee kuanzia Novemba 2015.
2. Huduma ya
Afya
·
Ziwepo takwimu sahihi za wazee za kiafya
zilizochambuliwa.
·
Itengwe fedha ya
kutosha katika bajeti kitaifa na katika halmashauri kwa ajili ya kutoa huduma
kwa wazee.
·
Kuwe na kasma ya masuala ya wazee.
·
Kuwe na Bima ya
Afya kwa wazee na kupata dawa na tiba zote bila malipo.
·
Halmashauri zote kuhakikisha fedha za
kuwalipia wazee kwenye CHF zinatengwa.
·
Kuwepo na dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa yanayoathiri wazee na
kuingiza dawa hizo katika orodha ya dawa muhimu.
·
Ihakikishwe kuwa
wazee wote nchini watapata huduma za afya kupitia vyumba maalum katika vituo
vyote vya afya na hospitali za umma na uwepo wa kitengo maalum cha wazee na
wodi za wazee katika vituo vya afya.
·
Ihakikishwe kuwa hospitali zinazopata
ruzuku ya Serikali zinatoa matibabu bila malipo kwa wazee kulingana na
makubaliano na Serikali.
·
Ihakikishwe
kuwepo vifaa tiba vya kupima magonjwa yanayoathiri wazee.
·
Kuwepo kwa huduma za mikoba (outreach
services) kwa wazee walioko mbali na taasisi za kiafya ili kupata huduma.
·
Itolewe elimu kwa wazee kuhusu Ukimwi na
magonjwa mengine mtambuka na namna ya kuwahudumia walioathirika.
·
Yatolewe
mafunzo kwa watumishi wote wa afya kuhusu haki za wazee na jinsi ya kuhudumia
wazee.
·
Kuwepo wataalam wa afya wenye ujuzi katika
kutoa huduma kwa wazee.
·
Kuwepo uwakilishi wa wazee katika kamati za
kata na bodi za afya za wilaya na mikoa.
·
Kusimamia matumizi bora ya rasilimali na
ukusanyaji wa mapato na kuweka utaratibu wa kupata dawa katika maduka ya dawa
binafsi ikiwa hakuna dawa katika hospitali za umma.
3. Sheria ya
Wazee
·
Ihakikishwe kwamba Sheria ya Wazee (Bara na Zanzibar) inaandaliwa na kufikishwa Bungeni/Baraza la
Wawakilishi.
·
Serikali ya
Tanzania ishiriki kikamilifu katika jitihada za kimataifa za kuwa na Mkataba wa
Haki za wazee.
4. Mauaji ya
Wazee
·
Mada kuhusu uzee na kuzeeka na haki za wazee
ziingizwe katika mitaala ya shule.
·
Jeshi
la Polisi lisimamiwe kikamilifu kutimiza wajibu wake katika kulinda wazee dhidi
ya vitendo vya unyanyasaji, ukatili na mauaji ya wazee kwa kisingizio cha
ushirikina.
·
Halmashauri
zote zielekezwe kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sera ya wazee na miongozo mingine
ya serikali juu ya usalama wa raia na makundi maalumu na waagizwe kutunga
sheria ndogondogo za utekelezaji wa maagizo hayo.
·
Idara
ya Ustawi wa Jamii iaigizwe kuelimisha jamii juu ya athari za imani potofu za
ushirikina na suala zima la matunzo ya wazee.
·
Itungwe sheria mahususi ya kulinda haki za
wazee.
·
Vijana wawezeshwe kujikwamua kiuchumi ili
kuepuka kuwaua wazee kwa nia ya kupata mali.
5. Uwakilishi
na Ushiriki wa wazee
·
Kuwepo na
ushiriki wa wazee katika ngazi zote za maamuzi (WDC, Halmashauri na Bunge).
·
Kuhakikisha
kwamba mabaraza ya wazee yanaanzishwa au kuimarishwa kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa
hadi Taifa na kuyatambua kisheria ili kuwapa wazee sauti na fursa ya kuchangia
mawazo katika ujenzi wa Taifa.
·
Serikali katika
ngazi zote ishirikiane na wazee na kusilikiza mawazo yao kupitia mabaraza ya
wazee. Mfano, viongozi wakitaka kukutana na wazee wafanye hivyo kupitia
mabaraza haya.
·
Kuwepo na
wizara/idara maalum itakayokuwa na wajibu wa kushughulikia masuala ya wazee.
6. Kipato
duni
·
Halmashauri
zote ziagizwe kuwa na takwimu sahihi zinazohusu mahitaji mbalimbali ya wazee.
Mfano, kutambua wazee wanaotunza yatima na watu walioathirika na VVU/UKIMWI.
·
Kuanzisha
mfuko wa wazee kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali za wazee.
·
Huduma
za usafiri wa umma zitolewe bila malipo.
·
kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wanaokaribia
kustaafu kuhusu njia za kukabiliana na matokeo ya kustaafu.
·
kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wazee na
kutoa mikopo nafuu kwa wazee wanazoweza kufanya kazi.
·
Taasisi za fedha ziagizwe kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wazee.
·
Kukomesha utaratibu wa baadhi halmashauri
kuendelea kutoza kodi ya majengo ya
makazi kinyume cha Waraka wa Serikali.
·
Wazee wasamehewe kulipa tozo na michango mbalimbali
kama vile ya shule, mwenge, maabara n.k.
7. Msaada wa Kisheria
·
Wazee wapatiwe msaada wa kisheria kwa
gharama za Serikali ili kulinda haki zao.
8. Vitambulisho
kwa wazee
·
Ihakikishwe kuwa halmashauri zote zinatambua
wazee na kuwapatia vitambulisho ambavyo vitatumika kupata huduma mbalimbali kama
vile matibabu bila malipo, usafiri wa umma bila malipo na pensheni jamii mahali
popote nchini.
Imepitishwa
na wawakilishi wa wazee kutoka mikoa yote nchini walioshiriki katika Mkutano
uliofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Juni, 2015 Blue Pearl Hotel, Dar es
Salaam
2 comments:
wewe ccm nini mbona huna coverage ya ukawa yakutosha
wewe ccm nini mbona huna coverage ya ukawa yakutosha
Post a Comment