Amri hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, baada ya Lowassa kuanza ziara yake juzi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kushuhudia kero zinazowakabili wananchi.
Kova alisema marufuku hiyo inatokana na jeshi hilo kugundua kuwa kuna wagombea ambao wameanzisha mtindo wa kutembelea maeneo mbalimbali jijini hilo yakiwamo vituo vya daladala, masoko na mengine kwa madai ya kuyatembelea makundi ya watu wenye kipato cha hali ya chini.
Alisema polisi imebainika mikusanyiko mikubwa isiyotegemewa inaashiria uvunjifu wa amani.
“Wakati wa ziara za aina hiyo yamejitokeza makundi ya watu mbalimbali kama vile waendesha bodaboda, machinga na makundi mengine katika namna ambayo imeleta taharuki pamoja na usumbufu unaotokana na kelele, msongamano au shughuli za usafiri kusimama kabisa,” alisema Kova.
Alisema juzi mchana katika makutano ya mtaa wa Swahili na Uhuru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya, alikutana na Lowassa ili kumpa hadhali ya kiusalama.
Kova alisema Mkondya alishindwa kutekeleza jukumu hilo kwa sababu Lowassa alikuwa amezungukwa na waendesha pikipiki wasiopungua 40 na magari mengi na kusababisha msongamano katika eneo hilo.
“Msongamano huo ulileta athari na malalamiko kutoka kwa watumiaji wengine wa barabara jijini Dar es Salaam,” alisema.
Kova alisema jeshi hilo lilibaini kuwa Lowassa alianza kuzunguka katika maeneo ya Wilaya ya Temeke kuanzia Agosti 24, mwaka huu kwa kutumia vyombo vya usafiri zikiwamo daladala.
“Ni lazima ieleweke wazi moja ya kazi za Polisi ni kudhibiti makundi makubwa ya watu katika namna ambayo kiongozi yeyote wa aina ya wagombea urais anatakiwa kulindwa kipindi chote cha kampeni hadi siku ya uchaguzi,” alisema.
Alisema ni vema wagombea hususani wa urais wakaonyesha ushirikiano kwa jeshi hilo ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea.
Vilevile, Kova aliwataka wagombea hao kujihadhiri kwenda katika makundi yasiyo rasmi kwa sababu za kiusalama.
“Tunawashauri viongozi wa vyama na wagombea wao wafuate ratiba za kampeni za mgombea urais/mgombea mwenza kwa vyama vya siasa kama ilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuondoa hisia za kufanyika kampeni nje ya ratiba,” aliongeza.
LOWASSA AKATISHA ZIARA
Wakati huo huo, Lowassa jana aliendelea na ziara yake ya kukagua kero zinazowakabili wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Ziara hiyo ilifanyika zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, kuzindua kampeni za mgombea wao wa urais jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo iliyoanza saa 3 asubuhi, Lowassa alitembelea masoko ya Tandale, Tandika na Kariakoo ambayo hata hivyo, haikuimaliza kutokana na kuzongwa na umati.
Lowassa ambaye jana kama ilivyokuwa juzi aliambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na baadhi ya maofisa wa Chadema, walilazimika kukatisha ziara hiyo kimya kimya, baada ya Kamanda Mkondya kuzuia msafara wake kwa sababu zilizodaiwa kuwa ni za kiusalama.
Akiwa katika mtaa wa Swahili Kariakoo, saa 6:15 mchana, msafara huo ulizuiliwa na Polisi ambao walikuwa wakiwasiliana na baadaye Kamanda Mkondya alilazimika kumfuata Lowassa kwenye gari lake na kuzungumza naye.
Lowassa alifuatwa na Kamanda Mkondya, kwenye gari hilo Toyota Noah yenye namba za usajili T 607 DDR, na kumueleza kuwa msafara huo haukuwa salama kutokana na kuzongwa na umati huo.
Kamanda Mkondya, ambaye alitumia takribani dakika 5 kumuelewesha Lowassa, alisema hakuwa na taarifa ya ziara hiyo na kwamba watu wengi walikuwa wameanza kumfuata, hivyo kumshauri aahirishe kwa ajili ya usalama wake.
Aidha, aliagiza msafara wa magari kugawanyika ili kupisha shughuli kuendelea kufanyika sokoni hapo.
Magari hayo yalianza kutawanyika kutoka mtaa huo kisha gari alilipanda Lowassa kungia mtaa wa Kongo ambako lilizidi kufuatwa na umati uliokuwa ukiimba ‘Lowassa rais’.
Kufuati agizo hilo, gari lililokuwa limebeba waandishi wa habari, lilifuata barabara ya kuelekea Mnazi Mmoja na kuongozana na magari mengine yaliyokuwa kwenye msafara wa kiongozi huyo.
ATEKA MASOKO
Lowassa na Duni waliwasili katika soko la Tandale saa 3:20 asubuhi na kupokelewa na umati ambao haukuwa na taarifa ya ujio wake.
Umati huo ulikuwa ukiimba ‘Rais rais’, ‘unasubiri kuapishwa tu’ ‘hakuna haja ya kupiga kura’ waliendelea kufanya hivyo na kulisukuma gari lake Tandale sokoni hadi stedi ya daladala Argentina.
ANYWA MAZIWA YA MAMALISHE
Akiwa sokoni hapo, Lowassa alikabidhiwa kikombe cha maziwa na mama lishe wakati akipita njia hali iliyomlazimu kuyachukua na kunywa.
Baada ya kupokea maziwa hayo na kuanza kuyanywa, wananchi walianza kushangilia huku wakiendelea kuimba na kutembelea wauza nafaka, mama lishe na wafanyabiashara ya matunda.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Tandale, Mutabu Ally, alimueleza Lowassa kuwa wanakutana na changomoto mbalimbali zikiwamo za kupanda kwa bei ya bidhaa na kukosa faida huku miundombinu ya soko hilo ikiwa mibovu.
Aidha, Ally hakusita kuelezea hisia zake kwa Lowassa kwa wanamuunga mkono na kumuakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
TANDIKA WAFUNGA BIASHARA
Baada ya kuwasilia katika soko la Tandika wilayani Temeke, wafanyabiashara na wateja wake walikumbwa na taharuki na kuacha shughuli zao kwenye kumlaki Lowassa.
Lowassa ambaye aliwasili sokoni hapo majira ya saa 4:30 asubuhi, alisababisha wafanyabiashara na wateja wao kulazimika kukimbia kwenda kumuona.
Nao wafanyabiashara wa maduka walilazimika kufunga maduka yao kudhibiti vibaka kupora bidhaa zao na fedha.
ASHINDWA KUKAGUA BIASHARA TANDIKA.
Katika soko la Tandika, Lowassa alishindwa kufanya ukaguzi kama alivyofanya soko la Tandale kutokana na kufunikwa na umati.
Lowassa alitumia dakika 30 kutembea sokoni humo huku wananchi wakitangulia mbele yake wakiendelea kuimba nyimbo za kumuunga mkono.
Walisikika wakiimba ‘mkombozi wa watanzania’, ‘mziki wa lowassa kuutuliza haiwezekani’ waliendelea kufanya hivyo na katika mitaa aliyopita ya Malumba wananchi walionekana wakitoka ndani na kuunga msafara huo wa waliokuwa wakimshangilia.
Pia, katika msafara huo wafuasi wake walibeba ndoo kichwani wakimaanisha wanashida ya maji.
Wengine walichukua magauni aina ya ‘Dela’ yaliyovalishwa sanamu ambalo lina nembo za CUF na kuanza kumsindikiza nalo.
BODA BODA WAAMSHA HISIA
Katika maeneo ambayo Lowassa alipita katika barabara za Tandale, Morogoro, Mburahati, Kigogo, Tabata, Mandela, Tandika, Kurasini Shimo la Udongo, madereva bodaboda waliomuona walianza kumfuata huku wakishangilia.
Mbali na kuzuiliwa na walinzi wakihisi wanaweza kusababisha msafara huo kuzuiliwa, walizidi kumfuata.
WALINZI WAZIDIWA NGUVU
Katika mitaa ya Tandika sokoni, Lowassa na Duni walifuatwa na umati na kusababisha walinzi wake kuzidiwa na nguvu ya watu waliokuwa wakikimbia na kusababisha vumbi na kutumbukia kwenye matope.
ANUNUA MAJI YA KIROBA
Lowassa akiwa katika soko la Tandika, aliwaungisha vijana waliokuwa wakifanya biashara kwa kununua maharage kilo 20 ambazo hata hivyo, alishindwa kuondoka nazo kutokana na mfuko aliobebea kuchanika.
Maharage hayo yalimwagika chini na watu walianza kuyazoa, pia alinunua maji ya viroba mawili kwa Sh. 10,000 ambayo yalichukuliwa na vijana hao na kuanza kuyanywa na mengine kuyamwaga chini ili kumpunguzia vumbi.
WAHAMASISHANA WATUNZE VITAMBULISHO
Katika maeneo ambako Lowassa alikuwa akishangiliwa, wananchi walikuwa wakiulizana kama wa nakadi za kupigia kura.
Walikuwa wakielezana na kuhamasishana kuwa wavitunze nyumbani hadi siku ya kupiga kura ili waiondoe CCM madarakani.
Ziara ya Lowassa ya jana inafuatia ya juzi aliyofanya ya kukagua kero za usafiri wa daladala wanazopata wananchi.
Akiwa ameambatana na mgombea mweza Duni, Lowassa alipita katika maeneo ya Gongo la Mboto, Chanika na Mbagala.
KAULI YA CHADEMA
Kufuatia kauli ya Polisi kuzuia ziara za Lowassa, Chadema ilisema itaendelea kufanya kampeni zake kwa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi na kwamba nchi haiongozwi kwa maelekezo ya mtu mmoja, bali sheria za nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Hbari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene, alisema Polisi waeleze Lowassa amevunja sheria gani ya nchi kwa kupita maeneo wanayoishi watu.
CHANZO: NIPASHE
4 comments:
Huu ni ujinga mkubwa sana unaofanywa na vyombo vya serikali., wao wanaona kama wanamkomoa EL na Ukawa kumbe kiukweli ndo wanazidi kumpa nguvu kubwa na kumuongezea umaarufu. hivi hawa viongozi shule walisomea wapi?? wasome 48 rules wataelewa haya!!
Huu ni ujinga mkubwa sana unaofanywa na vyombo vya serikali., wao wanaona kama wanamkomoa EL na Ukawa kumbe kiukweli ndo wanazidi kumpa nguvu kubwa na kumuongezea umaarufu. hivi hawa viongozi shule walisomea wapi?? wasome 48 rules wataelewa haya!!
Kuwanja mmemnyima barabarani na mitaani hamtaki kumwina naamini L ni Mtanzania kama Watanzania wengine anahaki ya kuwa mahali popote mda wowote hatakama anafuatwa na umati watu, wanyonge au hata waliochoshwa na manyanyaso ya ccm Chama gani kisichopenda haki za binadamu
mkuu wamezidiwa ndo maana wanafanya haya yote.wana tapa chapa ndebwe ndebwe mlalao wa chali kifo cha mende.wataisoma number mwaka huu na mafuriko haya zuiliki kwa mkono wakipiga goli la mkono watakiona cha mtema kuni.
mwaka huu muziki wa el wataujua tu na kucheza wataka wasitakeee.hata kama chihenu na mwenye mwana wakiimba sana wataisoma number ya el.
asubuhi kweupe el anachukua nchii mafisadi watahamia china mwaka huu.
Post a Comment