Advertisements

Thursday, September 17, 2015

BALOZI SEIF ATOA ONYO KUIBUKA KWA MAKUNDI YA KUSHAMBULIA WATU

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikaribishwa na Daktari Mkuu wa Hospitali ya Jeshi Bububu Luteni Kanali Haroub Yussuf Mwalimu kwenda kumkagua Mwanachama wa CCM Marjan Suleiman Pandu aliyelazwa katika Hospitali hiyo. Marjan alishambuliwa na Vijana juzi usiku wakati akibandika picha za Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dr. Ali mohammed Shein katika maeneo ya Mlandege.
Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Kijana wa Chama cha Mapinduzi Marjani Suleiman Pandu aliyelazwa katika wodi ya Hospitali ya Jeshi Bububu baada ya kuchambuliwa na Vijana juzi usiku hapo Mlandege.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa onyo kwamba Serikali kupitia vyombo vya ulinzi haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu au kikundi chochote kitakachohusika na hujuma au kusababisha madhara kwa watu wasio na hatia.


Alisema Serikali itapambana na tabia iliyoanza kuibuliwa na baadhi ya Vikundi kuanza kushambulia watu wakiwa katika harakati zao za kawaida kwa kisingizio cha kutumia mwavuli wa vugu vugu la Kampeni za Uchaguzi zinazoendelea Nchini.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo mara baada ya kumkaguwa Bwana Marijan Suleiman Pandu Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi aliyelazwa katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Bububu baada ya kushambuliwa na Kundi la Vijana juzi katika Maeneo ya Mlandege Mjini Zanzibar.

Bwana Marijan alivamia na Vijana hao majira ya Saa Moja usiku akiwa katika harakati za kupachika Mabango yaliyolipiwa kihahali na CCM Katika Taasisi zinazohusika yenye Picha za Mgombea wake wa Chama cha Mapinduzi {CCM } anayewania nafasi ya Urais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein.

Balozi Seif akimfariji kijana Marjan kutokana na maumivu aliyoyapata kutokana na kipigo alichokipata alielezea masikitiko yake kutokana na unyama huo ambao mbali ya kumsababishia majeraha lakini pia umekwenda kinyume na sheria za Nchi.

Alisema kitendo hicho kinafaa kulaaniwa kwa nguvu zote na wapenda amani kwa vile kimekiuka maazimio yaliyotiwa saini na kukubaliwa kwa pamoja na Viongozi wa vyama vyote waliosimamisha wagombea wao katika nafasi mbali mbali za Uongozi kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Oktoba.


Mapema Mwanachama huyo wa Chama cha Mapinduzi Bwana Marjan Suleiman Pandu akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba amewashukuru Madaktari wote waliosidia kumpatia huduma ya matibabu katika Hospitali hiyo ya Bububu.

Bwana Marjan alisema hivi sasa anaendelea kupata matibabu ambapo tayari yupo katika hali inayoridhisha baada ya kupata michubuko katika maeneo ya uso wake kutokana na kipigo cha Vijana hao.

Mwanachama huyo wa CCM Bwana Marjan alimuhakikishia Balozi Seif Ali Iddi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kampeni ya Chama cha Mapinduzi kwamba hivi sasa yuko vizuri katika kuendelea kukitumikia Chama chake. 

Alisema mtihani uliompata kamwe hautomvunja moyo bali ni mwanzo wa ukurasa mpya katika kuona juhudi zake pia zinachangia katika kuona chama chake cha Mapinduzi kinaendelea kushika dola baada ya kushinda uchaguzi wa mwezi Oktoba kwa ngazi zote.

Othman Khamis Ame


Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

1 comment:

Anonymous said...

Mbona hukusikika ukilani wale vijana waliokua wakipita na silaha za moto na mapanga mchana katika kila sehemu za mji wa Zanzibar na kuathiri wazanzibari wasio na hatia bure. Wale vijana waliorushia watu sime na mawe Melinne, hukusikika kulani, Hawa wote ni Binaadamu sawa.. Balozi jamii ya Kizanzibari ikufahamu vipi katika uongozi wako.. Taarifa zisiso rasmi huyu kijana alikua anabandua picha za mgombea wa chama cha upinzani....Tujitahidi kuplay fair game. Tusije tukaadhirika..