ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 29, 2015

MAALIM SEIF ATEMBELEA KISIMA KINACHOSADIKIWA KUWA NA MAFUTA KATIKA ENEO LA TUNDAUWA,ZANZIBAR


 Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwasalimia watoto Othman na Zainab waliokaa kwenye kisiwa kinachosadikiwa kuwa na mafuta katika eneo la Tundauwa.
 Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipandisha bendera katika tawi la CUF Tandani shehiya ya Kilindi lililokuwa chini ya Chama cha ADC, kuashiria ufunguzi rasmi wa tawi hilo.


Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wanachama wa wanachama wa Jumuiya ya maendeleo ya wanawake Tundauwa. (Hawapo pichani). 
Picha na Salmin Said, OMKR


Na: Hassan Hamad, OMKR
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ametembelea kisima kinachosadikiwa kuwa na mafuta katika eneo la Tundauwa, na kusema kuwa mafuta ya Zanzibar yatachimbwa  katika kipindi kifupi kijacho.

Amesema  kwa miaka mingi Zanzibar imeshindwa kuchimba mafuta yake kutokana na kutokuwepo mikakati imara, na kuahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha kuwa suala hilo linawekewa mikakati imara ya uchimbaji, ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopatikana katika eneo hilo, kisima hicho chenye urefu wa zaidi ya futi 12 elfu na mia saba, kilijengwa miaka 53 iliyopita na kuonesha dalili za kuwepo mafuta.

Wakati huo huo Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ametembelea Jumuiya ya maendeleo ya wanawake Tundauwa, na kutoa wito kwa wananchi wa kijiji hicho kujiunga na jumuiya hiyo ili kupata mafanikio zaidi.

Amesema jumuiya hiyo inayojihusisha na masuala mbali mbali yakiwemo uhifadhi wa mazingira na kilimo, imekuwa mfano mzuri wa kuigwa kutokana na mafanikio inayoyapata tokea kuanzishwa kwake.

“Jumuiya hii inafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano, hivyo natoa wito kwa wananchi wa vijiji hivi kujiunga kwa wingi ili kuleta mafanikio zaidi” amesema Maalim Seif.

Mapema akisoma risala ya Jumuiya hiyo, bibi Raya Abdallah Rashid amesema lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kupambana na umaskini, maradhi pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Amesema Jumuiya hiyo pia imekuwa ikiielimisha jamii juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na dawa za kulevya.

Amesema Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 imepata mafanikio makubwa yakiwemo kutambuliwa kama jumuiya rasmi, kupanda mikoko ekari mbili kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira, ufugaji wa nyuki na kilimo cha mboga mboga.

Hata hivyo bi Raya amesema bado wanakabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na ukosefu wa jengo la ofisi, na kulazimika kuanzisha ujenzi ambapo zaidi ya shilingi milioni saba na nusu tayari zimetumika kwa ajili ya ujenzi huo, na kuomba kupatiwa misaada zaidi ili wamewe ukamilisha ujenzi wao.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, amefungua tawi jipya la CUF Tandani shehiya ya Kilindi lililokuwa chini ya Chama cha ADC.

Amesema Tawi hilo limebadilishwa kutoka ADC na kuwa tawi la CUF baada ya wanachama  25 wa ADC kuamua kujiunga na CUF na kuongeza idadi ya wanachama wa tawi hilo kufikia 103.

Tawi jengine la ADC la eneo la meli tisa Wingwi, pia lilibadilishwa kuwa tawi la CUF baada ya wanachama wake kukihama chama hicho.

No comments: