ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 29, 2015

MAHUJAJI 50 KUTOKA TANZANIA WAPOTEA

WAKATI Waislamu kote duniani wakiwa katika simanzi kuu kutokana na vifo vya mahujaji zaidi ya 700 katika mji mtakatifu wa Makka, Saudia Arabia, imethibitika kuwa zaidi ya mahujaji 50 wa Tanzania, hawajulikani walipo.
Aidha, idadi ya mahujaji wa Tanzania waliokufa katika tukio la kukanyangana katika mji huo mtakatifu, imefikia watano, baada ya mtu mmoja zaidi kuthibitika kufa na mwingine kupatikana akiwa majeruhi.
Kutokana na ongezeko hilo la vifo, idadi ya Watanzania waliokufa wakiwa katika ibada ya Hijja, moja ya nguzo kuu ya Kiislamu, sasa imefikia watu watano. Hayo yamethibitishwa jana na Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakari Zuberi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoituma akiwa Makka.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa “Bakwata kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Saudi Arabia, tumepata taarifa kwamba maiti mmoja amepatikana, ametambulika kwa jina la Shafi Khamisi Ali. Pia Nasra Nassor Abdallah amepatikana akiwa amepata majeraha. Mwenyezi Mungu atawapa tahfif Insha Allah.
“Kadhalika tumepokea taarifa ya kutopatikana kwa Watanzania 50 ambao walikuwapo Makka wakati wa tukio hilo. Kati yao 30 walisafiri kupitia taasisi ya Ahlu Daawa, taasisi ya Khidma watu 17 na TCDO watu watatu.”
Taarifa ya Mufti Zuberi imekuja ikiwa ni mwendelezo wa taarifa juu ya tukio la kuhuzunisha, lililotokea wiki iliyopita huko Mina, Saudi Arabia, ambako mahujaji zaidi ya 700 walikufa na wengine kujeruhiwa wakati wakielekea kwenye Jamaraat, ambapo palitokea msongamano mkubwa.
Alisema anatambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa, ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji. Hata hivyo, aliwaomba Waislamu kuwa na moyo wa subira, kwani juhudi za kuwatafuta mahujaji wengine zinaendelea.
Aliwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki na Mwenyezi Mungu, apokee ibada zao, awasamehe madhambi yao na awakusanye katika kundi la waja wema peponi. “Kutokana na mtihani huu kwetu sote, nawaombea dua wafiwa Mola awape subra na ustahmilivu na kuwaombea wagonjwa wapate tahfif.
Pia nawaomba Waislamu wote Tanzania kuwaombea dua waathirika wa mtihani huu. “Mwisho nichukue fursa hii kuwaomba wale wote wenye nafasi ya kuwafariji na kuwasaidia wanafamilia, ambao katika ajali hii wameondokewa na nguzo katika familia hizo wafanye hivyo.
Tuwasaidie wanafamilia hawa kwa hali na mali katika wakati huu mzito sana kwao ili tuwapunguzie majonzi na unyonge walionao,” ilisema taarifa hiyo ya Mufti. Mufti aliushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia.
Alisema wanaendelea kushirikiana na ubalozi huo na vyombo vya serikali ya Saudi Arabia. Alisema maofisa wa Bakwata waliopo Makka, wanaendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wa Tanzania kwa umakini mkubwa.
Tukio hilo limetajwa kuwa baya zaidi kutokea wakati wa Hijja katika kipindi cha miaka 25 iliyopita. Iran imepoteza zaidi ya mahujaji 140. Idadi ya mahujaji wengine waliokufa na nchi wanazotoka kwenye mabano ni 87 (Morocco), 55 (Misri), 20 (Cameroon), 19 (Niger), 18 (India), 18 (Pakistan), 11 ( Chad), 8 (Somalia), 5 (Senegal).
Nchi za Algeria, Uturuki na Tanzania kila mmoja imepoteza mahujaji wanne, ingawa jana kiliripotiwa kifo cha mahujaji mwingine wa Tanzania, hivyo kufanya waliokufa kufikia watano. Nchi za Indonesia, Kenya na Nigeria kila moja imepoteza mahujaji watatu wakati Uholanzi, Burundi na Burkina Faso kila mmoja imepoteza mtu mmoja.
Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, jijini Dar es Salaam jana, ilisema idadi ya watu wa mataifa mbalimbali duniani waliokufa huko Makka, imeongezeka na kufikia 769 na majeruhi wamefikia 934.
Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia Ubalozi wa Tanzania mjini Riyadh, Saudi Arabia, ilisema tukio hilo la Makka, lilitokea Septemba 24 mwaka huu na lilitokana na mkanyagano (stampede) wa mahujaji.
“Wizara kupitia Ubalozi huo inaendelea kufuatilia hatma ya mahujaji wa Tanzania waliopotea katika tukio hilo la ajali ambapo hadi sasa mahujaji wa Tanzania wapatao 50 bado hawajaonekana.
Vikundi wanavyotoka mahujaji hao na idadi yao ni kama ifuatavyo Ahlu Daawa- mahujaji 30, Khidma Islamiyamahujaji 16 na TCDO- mahujaji 4,” ilieleza taarifa hiyo ya Wizara. Vile vile juhudi za Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na viongozi wa vikundi vilivyopoteza mahujaji wao, zimefanikiwa kuutambua mwili wa hujaji mmoja aliyefariki dunia, anayejulikana kwa jina la Shafi Khamis Ali kutoka kikundi cha Ahlu Daawa.
Kutambuliwa kwa mwili wa hujaji huyo, kunafanya idadi ya mahujaji wa Tanzania, waliofariki dunia katika tukio hilo kufikia watano. Pia, Wizara kupitia Ubalozi wake, imepokea taarifa ya kupatikana kwa hujaji mwingine, anayeitwa Nasra Abdullah akiwa hai, naye kutoka kikundi hicho cha Ahlu Daawa.
“Mahujaji wengine wa Tanzania wapo salama, ambapo tarehe 26 Septemba 2015 walimaliza Ibada ya Hijja na tarehe 28 Septemba 2015 wameanza safari ya kurejea nyumbani. Wizara inaendelea kuwaomba wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati serikali ikiendelea kufuatilia” ilisema taarifa hiyo ya Wizara.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya wa Saudi Arabia, Khalid al-Falih, amekaririwa na mashirika ya kimataifa, akisema kuwa Serikali ya Saudi Arabia itachunguza vifo vya mahujaji hao zaidi ya 700 vilivyotokea Makka.
Waziri huyo alieleza kuwa uchunguzi utafanyika, kubaini chanzo cha vifo hivyo, ambavyo havijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 25. “Uchunguzi utafanyika juu ya tukio la kufa mahujaji katika mji wa Mina.
Tunadhani baadhi ya mahujaji walianza kutembea bila kupata maelekezo kutoka kwa wahusika maalumu wa kuwaongoza. Uchunguzi utakuwa wa haraka na tutatoa matokea yake mapema,” alieleza Waziri huyo wa Saudi Arabia.
Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saud Arabia ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu tukio hilo na kwamba baada ya kupata matokeo ya uchunguzi huo, atatoa maamuzi stahiki. Pia, mfalme Salman ameagiza taratibu za Hijja, ziangaliwe upya.
Awali, ilibainika kuwa mahujaji 717 wamepoteza maisha na wengine 800 walijeruhiwa katika tukio hilo la Makka, wakati watu zaidi ya 2,000,000 walipokuwa wakiswali Ibada ya Hijja. Makundi makubwa mawili ya mahujaji, yaligongana yalipokutana wakati yakielekea “kumtupia mawe shetani”, kilometa chache nje ya Makka.

CHANZO: HABARI LEO

No comments: