ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 29, 2015

Nyosso kufungiwa miaka miwili TFF.

Wakati Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Wakati Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ameweka wazi kuwa shirikisho hilo la soka nchini litamwadhibu Juma Nyosso, beki huyo wa kati wa Mbeya City yuko hatarini kufungiwa miaka miwili kucheza soka kutokana na kurudia tabia yake chafu ya kupenyeza kidole katikati ya makalio ya wachezaji wa timu pinzani.

Aidha, mshambuliaji Donald Ngoma wa Yanga yuko hatarini kufungiwa mechi tatu na kupigwa faini kutokana na kumpiga kichwa kwa makusudi mbali na ulipokuwapo mpira beki wa pembeni kulia wa Simba, Hassan Kessy, wakati wa mechi yao ya Jumamosi.

Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi za TFF, Nyosso yuko hatarini kufungiwa kusakata soka rasmi kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na kumdhalilisha mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco.

Malinzi amesema shirikisho hilo litamchukulia hatua kali nahodha huyo wa Mbeya City, kutokana na tukio hilo.

Rais huyo alisema kuwa adhabu kuhusiana na kitendo cha beki huyo wa zamani wa Ashanti, Simba na timu ya Taifa (Taifa Stars), itatolewa baada ya kamati husika kukutana na kupitia ripoti ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambao ulimalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

"Udhalilishaji uliofanywa leo (juzi) na mchezaji mmoja wa timu ya Ligi Kuu tumeuona, hatua kali zitachukuliwa muda siyo mrefu, tuwe na subira," aliandika Rais Malinzi katika ukurasa wake wa Twitter juzi saa 3:27 usiku.
Nyosso alitumia mwanya wa refa Martin Saanya kutatua mgogoro baina ya wachezaji wa timu hizo na kumtomasa mwenzake nyuma.

Hata hivyo, Bocco alionyesha utulivu na ustaarabu licha ya kuonyesha dalili zote za kukasirishwa na kitendo hicho, kwani alimfuata refa, Martin Saanya, kutoka Morogoro na kuwasilisha malalamiko yake.

Saanya hakuonekana kuyatilia mkazo malalamiko ya Bocco, ambaye alipandisha hasira na kutaka kumpiga Nyosso kama si refa huyo kuwatenganisha.

Benchi la Ufundi la Azam FC lilipeleka ushahidi wa picha kwa refa wa akiba, Soud Lila wa Dar es Salaam ambaye alitoa maelekezo picha hizo zipelekwe kwa Ofisa wa TFF, Iddi Mshangama.

Tukio hilo lilionekana kabisa kumnyima raha, Bocco na kushindwa kucheza katika kiwango chake kuanzia hapo, ingawa Azam FC ilifanikiwa kushinda 2-1.

Hii inakuwa mara ya nne kwa Nyosso kuonekana akifanya hivyo uwanjani, mara ya kwanza akiwa Ashanti United 2007 alimfanyia hivyo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Joseph Kaniki, aliyejibu kwa kumpiga ngumi hali iliyomponza kufungiwa na TFF.

Februari 28 mwaka huu alitenda kadhia hiyo dhidi ya Elias Maguli aliyekuwa akichezea Simba wakati wa tukio hilo, ambalo lilimfanya Nyoso kufungiwa mechi nane na TFF.

Katika ukurasa wake wa Facebook, kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Amir Maftah, jana aliposti picha ya zamani akiwa uwanjani na kuandika: "Duniani tumeletewa kwa sababu. Tukio lililotokea jana (juzi) limenikumbusha machungu ndani ya nafsi yangu. Juma Nyoso si tukio lake la kwanza kufanya ushenzi huo..mechi hii ya kwenye picha alinifanyia tukio kama hilo na kusababisha mimi kumpiga kichwa na kutolewa kwa kadi nyekundu... Najiuliza ila sipati jibu. Nyoso ni mtu wa aina gani? Dini gani? Tamaduni yake ya wapi? Sijapata jibu."

Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda, ametaka wachezaji nchini waungane kukomesha tabia za Nyoso.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mapunda aliandika: "Binafsi nachukua nafasi hii kuwaomba wachezaji wenzangu wanaocheza na waliowahi kucheza soka na wadau wote wa pamoja na mashabiki wa ndani na nje ya nchi KULAANI kwa nguvu zote TABIA na VITENDO VYA AIBU na udhalilishaji anavyofanya mchezaji mwenzetu NYOSO. Hii ni aibu siyo yake pekee bali ni yetu sote wachezaji hasa kwa medani ya kimataifa na tutaonekana 'hopeless' pia na kukosa hata nafasi ya kwenda kucheza soka nje kwa tabia hizi dhalimu. Tunaomba adhabu yake itakayotolewa iwe fundisho."

KANUNI TFF
Kanuni ya 37(24) cha Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2015 kinasema: "Mchezaji yeyote atakayepatikana na hatia ya kufanya makosa makubwa ya kimaadili au kinidhamu, au ya kibaguzi au ya kidhalilishaji au yatakayotafsiriwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa taratibu za mchezo na ubinaadamu atatozwa faini kati ya shilingi milioni moja mpaka milioni tatu au/na kusimamishwa kushiriki michezo mitatu mpaka kumi ya klabu yake yoyote atakayoitumikia katika Ligi Kuu na mashindano mengine rasmi ya TFF au kufungiwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja na miwili."

NGOMA
Picha za video ya mechi ya Simba dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa Wanajangwani kushinda 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi, zinamwonyesha Ngoma akimpiga kichwa makusudi (bila mpira) mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar (Kessy) dakika mbili kabla ya robo saa ya mchezo. Refa Israel Nkongo na wasaidizi wake hawakuchukua hatua zozote dhidi ya Mzimbabwe huyo.

Ingawa Ngoma na Nyosso hawakuadhibiwa na marefa uwanjani, kanuni za ligi msimu zinawabana na zinailazimu TFF kuwachukulia hatua kutokana na ushahidi utakaotolewa.

Kanuni ya 14(28) kinasema: "TFF/TPLB inawajibika kufanyia kazi/uchunguzi na kutolea uamuzi tukio lolote la mchezo wa hatari au lisilo la kawaida, la kudhalilisha au la kibaguzi lililotokea wakati wa mchezo kutokana na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali au taarifa ya mchezo ya Kamishna ambalo mwamuzi hakulichukulia hatua yoyote mchezoni."

TAMBWE PIA YUMO
Kamati ya Nidhamu ya TFF itakapokaa, huenda pia ikatoa hukumu dhidi ya mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe wa Yanga ambaye alifikishwa mbele ya kamati hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kumdhalilisha kwa kumvuta katikati ya miguu beki wa kati wa Simba kutoka Uganda, Juuko Murshid. wakati wa mechi ya watani wa jadi Machi 8 mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: