Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando akiangalia kadi za matibabu ambazo alizikabidhi kwa wasanii ambao wametimiza taratibu za kujiunga na Mfuko huo.

Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Rehani Athumani akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusiana na utaratibu wa kujiunga na Mfuko huo.

Bw. John Kitime akielezea jambo kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya kupokea kadi yake ya matibabu.

Msanii Aisha Salvador akipokea kadi ya matibabu kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando.
Msanii John Kitime akipokea kadi ya matibabu itakayomwezesha kupata huduma kote nchini.

Baadhi ya wasanii waliohudhuria hafla hiyo pamoja na waandishi wa habari.
Na Grace Michael
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umetekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwahamasisha wasanii nchini kujiunga na huduma za Mfuko huo ambapo leo imekabidhi rasmi kadi za matibabu kwa baadhi ya wasanii ambao wametimiza taratibu zinazotakiwa.
Akikabidhi kadi hizo, Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Michael Mhando amesema kuwa, Mfuko umetekeleza agizo la Rais ambalo alilitoa wakati wa sherehe za kuagwa na kundi hilo zilizofanyika Agosti 6, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City.
“Rais wetu wakati akiagwa na kundi hili, aliwahimiza sana wasanii kujiunga na Mfuko ili wawe na uhakika wa matibabu hivyo sisi kama watendaji tulilichukulia kama agizo kutoka kwa kiongozi wetu na tukalifanyia kazi hivyo nitumie tu fursa hii kuwahimiza na wasanii wengine ambao bado hawajachukua hatua ya kujiunga watumie fursa hii,” alisema Mhando.
Alisema kuwa suala la matibabu ni suala nyeti ambalo kila mmoja anatakiwa kulipa uzito mkubwa ili kuwa na uhakika wa afya yake hivyo ni vyema kujiunga na utaratibu wa bima ya afya ambao unamwezesha mhusika kupata matibabu bila ya gharama yoyote.
Bw. Mhando alisema kuwa wasanii ambao wamekabidhiwa kadi za matibabu watakuwa na fursa ya kupata huduma zote za matibabu zinazogharamiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, sawa na mwanachama mwingine yoyote, kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Mafao hayo yanajumuisha gharama za usajili, gharama za kumwona daktari, vipimo na dawa, huduma za wagonjwa wa nje na kulazwa, dawa zote zilizodhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zitumike katika vituo vya matibabu hapa nchini, huduma za upasuaji mkubwa na mdogo, afya ya kinywa na meno na kadhalika.
Huduma hizi watazipata mahali popote nchini kwenye vituo vilichosajiliwa na Mfuko.
Kwa upande wa Wasanii hao wakiongozwa na John Kitime alisema kuwa kitendo cha kukabidhiwa kadi ya matibabu ni kikubwa mno kwao kutokana na umuhimu wa suala la afya.
“Kwetu sisi siku ya leo ni siku kubwa mno, tunao uhakika wa kutibiwa hata kama hatuna hela kwenye mifuko yetu, tunaushukuru Mfuko kwa jitihada zake ambazo zimetuwezesha kuwa na kadi hizi,” alisema.
No comments:
Post a Comment