Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa Kwanza kutoka kulia akiuhakikishia Ujumbe wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation kwamba Uchaguzi Mkuu wa Tarehe 25 Mwezi huu utafanyika katika misingi ya haki na amani hapa Zanzibar.
Ujumbe huo unaoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Bwana Joseph Butiku wa Pili kutoka Kushoto up[o Zanzibar kukutana na Viongozi wa ngazi za juu kujaribu kusaidia mawazo ya kuona Taifa linaendelea kudumisha amani iliyopo Nchini. Picha na –OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kauli za baadhi ya wanasiasa wakati wanapokuwa majukwaani za kupalilia cheche za kutaka kuibua vurugu zisiwashitue Wananchi kwa vile Serikali itaendelea kuwa makini katika kudumisha usalama na mali zao.
Alisema wapo Viongozi wa Kisiasa ambao wengine wamekabidhiwa majukumu makubwa ya Kiserikali ambao wamekuwa na tabia ya kuendelea kuilaumu Serikali kwa kutumia majukwaa ya kisiasa wakijisahau kwamba wao pia ni sehemu ya Serikali wanayoilalamikia muda wote.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Bwana Joseph Butiku aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa uliojumuisha Viongozi wakuu wa Vyama vya CCM na CUF imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya kuwahudumia Wananchi wote bila ya ubaguzi.
Balozi Seif alisema maamuzi yanayotolewa kutoka katika Vikao vya Baraza la Mapinduzi Zanzibar kwa kuhusisha mawazo ya Viongozi wa pande zote mbili ndio yanayoshushwa chini kwa utekelezaji wake kupitia usimamizi wa watendaji wa Taasisi za Umma.
Alieleza kwamba inashangaza kuona baadhi ya Viongozi hao ambao ni sehemu ya maamuzi hayo huanza kwenda kwa wananchi kuwadanganya na kujifanya kwamba wao hawajahusishwa na maamuzi hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Taasisis ya Mwalimu Nyerere Foundation kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi imeshajipanga vyema katika kuona uchaguzi Mkuu wa Tarehe 25 mwezi huu unafanyika na kumalizika kwa amani.
Balozi Seif aliwatoa hofu Wananchi wote kuitumia vyema bila ya woga haki yao ya Kidemokrasia kwa kwenda vituoni kupiga kura ya kuwachagua viongozi waliowapima wakati wakisikiliza sera zao ili wawaongoze katika kuwaletea maendeleo ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation Bwana Joseph Butiku alisema ujio wao Zanzibar ni mfululizo wa ziara zao za kukutana na baadhi ya Viongozi wa ngazi za juu wa Serikali katika kujaribu kusaidia mawazo ya kuliepusha Taifa kujitumbukiza katika vurugu.
Bwana Butiku alisema zipo kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Kisiasa, Kijamii na hata wa Kidini kwenye maeneo mbali mbali ya Nchi ambazo zimeanza kuonyesha ishara mbaya ya kutaka kuliingiza Taifa katika wimbi la mizozo isiyo na msingi wowote.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere mbali ya majukumu yake kadhaa pia hujikita zaidi katika kusaidia kuelimisha jamii kupitia mfumo wa midahalo pamoja na makongamano yanayojumuisha watu wa rika tofauti nchini.
Othman Khamis Ame
No comments:
Post a Comment