ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 17, 2015

NISHATI YA JOTOARDHI KUIPANDISHA HADHI HIFADHI YA WANYAMAPORI SELOUS

Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo ya Biashara, Mhandisi Kato Kabaka (aliyesimama) kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania, akitoa elimu ya nishati ya Jotoardhi kwa wafanyakazi wa hifadhi ya wanyamapori Selous na jinsi gani nishati hiyo itaongeza idadi ya watalii.
Wafanyakazi wa hifadhi ya wanyamapori Selous na kampuni ya uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania wakimsikiliza kwa makini Mhandisi Kato Kabaka (hayuko pichani) alipokuwa akiwaelimisha namna nishati ya Jotoardhi itakavyoongeza idadi ya watalii kupitia mabwawa ya kuogelea ya maji moto yatakayojengwa ndani ya hifadhi hiyo.

Bwana Eneck Majahasi (aliyesimama) akihitaji ufafanuzi ikiwa mitambo ya uzalishaji wa nishati ya Jotoardhi itakayojengwa ndani ya hifadhi ya Selous haitakuwa na madhara kwa wanyamapori walioko ndani ya hifadhi.


   Na. Lilian Lundo - Maelezo


Kuendelezwa kwa nishati ya Jotoardhi Tanzania itaipelekea kupanda hadhi kwa hifadhi ya wanyamapori Selous.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo ya Biashara, Mhandisi Kato Kabaka kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania wakati akizungumza na wafanyakazi wa hifadhi ya wanyamapori Selous, kambi ya Matambwe alipokuwa akitoa elimu ya nishati ya Jotoardhi yenye viashiria (majimoto) ndani ya hifadhi hiyo, leo.

“Kama utafiti utaonyesha chanzo cha nishati ya Jotoardhi kipo ndani ya hifadhi, basi nishati hiyo itapelekea hifadhi ya Selous kuongeza idadi ya watalii kwa kujenga mabwawa ya kuogelea yatakayokuwa na maji ya moto na kujenga vibwawa vidogo ndani ya vibanda vya kupumzikia kwa ajili ya kuweka miguu wageni watakao kuwa wakitembelea hifadhi hiyo.” Alisema Mkurugenzi Kato.

Mkurugenzi Kato aliongeza kwa kusema kuwa, mabwawa ya maji moto yatakuwa ni utalii mwingine ambao utakuwa umeongezeka ndani ya hifadhi ya Selous, kwani watalii watakapokuja kuangalia wanyama watapata fulsa ya kupumzika ndani ya mabwawa ya maji ya moto.

Bwana Eneck Majahasi, mfanyakazi wa hifadhi ya Selous alihitaji ufanunuzi kama hakutakuwa na madhara kwa wanyamapori ikiwa mitambo ya uzalishaji wa nishati ya Jotoardhi itajengwa ndani ndani ya hifadhi.

“Kwa sasa kampuni inafanya utafiiti, utakapokamilika wataalam kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania na hifadhi ya wanyamapori Selous wataenda kujifunza namna ambavyo nchi nyingine zimefanikiwa kuzalisha nishati ya Jotoardhi ndani ya hifadhi za wanyamapori,” Alijibu Mkurugenzi Kato.

Akiongeza kujibu swali hilo, Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Bi. Johary Kachwamba alisema kuwa nchi ya Kenya imefanikiwa kuvuna zaidi ya megawati 550 za umeme unaotokana na Jotoardhi na asilimia kubwa ya mitambo ya uzalishaji ipo ndani ya hifadhi za wanyamapori zilizopo maeneo ya Olkaria nchini Kenya. Hivyo Tanzania haina budi kujifunza kutoka Kenya na kufanya vizuri zaidi.

Bwana Tipa Lazaro mfanyakazi wa hifadhi ya wanyamapori Selous aliipongeza timu nzima ya Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania kwa elimu nzuri waliyoitoa juu ya nishati ya Jotoardhi na kusema kuwa wafanyakazi wa hifadhi ya Selous hawana pingamizi lolote juu ya uendelezaji wa utafiti huo ndani ya hifadhi. Kwani kukamilika kwa mradi huo ni mafanikio makubwa kwa taifa la Tanzania.

Serikali ya Tanzania kupitia TANESCO ilisajili kampuni ya kuendeleza nishati itokanayo na Jotoardhi nchini. Mpaka sasa kampuni hiyo imegundua zaidi maeneo 50 yenye viashiria vya Jotoardhi hapa nchini. Maeneo hayo yamegawanyika katika kanda nne, ambazo ni kanda ya kaskazini, kanda ya kusini, kanda ya magharibi na kanda ya mashariki inayohusisha Utete(Pwani), Luhoi(Pwani) na Kisaki(Morogoro) ilipo hifadhi ya Selous.

No comments: