Katika fainali hiyo, Chadema inayoungwa mkono na Ukawa itafunga kampeni zake katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam huku CCM ikisema suala hilo bado ni siri, lakini vyanzo mbalimbali vikidokeza kuwa huenda ikawa ni katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Dar es Salaam au kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Mikutano hiyo ya mwisho itakuwa ndiyo hitimisho la safari ndefu ya vyama hivyo na vingine kunadi sera zao katika mikoa yote ya Tanzania, kazi iliyodumu kwa takribani siku 64 tangu Agosti 22, mwaka huu.
CCM ilizindua kampeni zake, Agosti 23 katika viwanja vya Jangwani, wakati Chadema ilizindua Agosti 29 katika viwanja hivyo hivyo.
Hata hivyo, Chadema ilipata viwanja hivyo kwa mbinde baada ya CCM kuvilipia kwa siku tatu mfululizo kwa ajili ya matamasha, lakini baada ya majadiliko yaliyoshirikisha mmiliki wa viwanja hivyo, Manispaa ya Ilala na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), chama hicho tawala kilikubali kuwaachia Ukawa.
Chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya CCM kimelieleza Mwananchi kuwa watahitimisha kampeni hizo jijini Mwanza, ili baada ya hapo mgombea urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli aende jimboni kwake Chato, kupiga kura siku inafuata.
Hata hivyo, Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, Januari Makamba alisema atatoa taarifa za wapi chama hicho kitakapomalizia kampeni hizo, wakati muafaka utakapofika.
Kuhusu namna watakavyomaliza kampeni hizo kwa kishindo, Makamba alisema hawawezi kutoa mbinu zao katika siku ya mwisho ya kampeni kwani ni siri ya chama.
Hata hivyo alisema, “Ng’ombe hanenepeshwi siku ya mnada, hiyo ni siku ya kumalizia tu, lakini si ya kumnenepesha ng’ombe,” alisema.
Kuhusu Magufuli kuhitimisha kampeni hizo Mwanza, ili baadaye aende jimboni kwake Chato kwa ajili ya kupiga kura, Makamba alisema anaweza kufanya hivyo lakini si lazima kwani wana uwezo wa kumsafirisha mgombea huyo popote pale atakapokuwa ili akapige kura.
“Mgombea wetu yupo vizuri, amefanya kampeni vizuri kwa kutembea katika majimbo yote kwa barabara, hatuna wasiwasi na siku ya mwisho kwa sababu amefanya kazi yake vizuri,” alisema.
Kwa mujibu wa ratiba ya CCM iliyorekebishwa, Magufuli atamalizia kampeni zake katika mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Monduli, Arusha na Kilimanjaro hadi Oktoba 7. Baada ya hapo itatengenezwa ratiba nyingine mpya ambayo itajumuisha na tarehe ya kuhitimisha kampeni.
Ofisa wa CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi, Thoba Nguvila alisema ratiba kamili ya wapi watakapohitimisha kampeni hizo itajulikana Oktoba 7, baada ya vyama vyote vya siasa kufanya kikao na NEC Oktoba 6.
Nguvila alisema ratiba nyingine ya kuanzia Oktoba 8 itaandaliwa baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya vyama vya siasa na NEC, mnamo Oktoba 6.
Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Claud Mbelembwa ambaye awali ofisi yake ilitoa viwanja hivyo, alisema jana kuwa hana mamlaka ya kuzungumzia viwanja vitakavyotumika bali NEC ndiyo yenye mamlaka hayo.
“Mimi siwezi kuzungumzia hilo nahusika na viwanja watakavyotumia madiwani na wabunge tu, kwa hiyo nenda NEC,” alisema.
Kuhusu gharama za viwanja hivyo, Mbelembwa pia alikataa kutaja bei ya kiwanja na kusema kuwa hawezi kulizungumzia hilo, bila kuweka wazi sababu za kukataa.
“Nina mambo mengi sasa hivi siwezi kuzungumzia hilo, hata hayo masuala ya bei mimi siyazungumzii kwa sasa,” alisema.
Hata hivyo gharama za kawaida za viwanja hivyo ni kiasi cha Sh 50,000 kwa siku.
Mkurugenzi wa uchaguzi, Kailima Kombwey alisema ratiba ya NEC inaonyesha kuwa CCM watahitimisha kampeni hizo, Kawe, viwanja vya Tanganyika Packers na Chadema watazifunga katika viwanja vya Jangwani.
Wakizungumzia kuhusu hitimisho la kampeni hizo, chanzo kutoka Chadema kilithibitisha kuwa kampeni za tarehe 24, zitafanyika katika viwanja vya Jangwani kama ratiba ya NEC inavyoeleza.
Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema wamejiandaa vilivyo ingawa hakutaka kuweka wazi namna watakavyozipamba kampeni hizo.
“Tumejiandaa na tutazifanya kampeni hizo kama ambavyo tulianza, lakini mambo mengine siwezi kueleza zaidi,” alisema.
Vita ya viwanja
Awali Ukawa walinyimwa ruhusa ya kutumia viwanja vya Jangwani Agosti 29 wakati wa uzindunzi wa kampeni zao. Manispaa ya Ilala iliwanyima kibali Ukawa kwa madai kuwa uwanja huo umeshachukuliwa na CCM.
Hata hivyo siku moja kabla ya kampeni hizo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi alitoa idhini kwa Ukawa kutumia uwanja huo.
Mngulumi alisema ofisi yake imefanya majadiliano na NEC na kukubaliana kuwa Ukawa wautumie uwanja huo kwa tarehe 28, wakati CCM ikiwa imebakiwa na siku mbili kuzindua kampeni zao.
Katika hitimisho la kampeni hizo kuna vita ya maeneo ya kuhitimisha pamoja na vita ya vituo vya televisheni, vinavyorusha matukio hayo ya wagombea kurusha kete zao za mwisho.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment