Advertisements

Saturday, October 10, 2015

KEMIKALI ZIKITUMIKA IPASAVYO ZITAPUNGUZA ATHARI KWA WATU NA MAZINGIRA.



Meneja kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Mashariki Bw. Daniel Ndiyo akiwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mpango wa kudhibiti majanga yatokanayo na kemikali ambapo Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya kemikali hatari kwa binadamu na mazingira. Kulia ni Afisa Habari wa ofisi hiyo Bw. Sylvester Omary
 Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.



(Na Jovina Bujulu- MAELEZO)
Kukosekana kwa uelewa juu ya hatari na madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali kumetajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha ajali mbali mbali hapa nchini.

Hayo  yamesemwa jijini Dar es salaam  na Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Wakala wa Maabara  ya Mkemia Mkuu  wa Serikali Ndugu Daniel Ndiyo alipokuwa akizungumzia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi  na uthibiti wa kemikali.

“Chanzo kikubwa cha ajali na matukio mengi ya kemikali yanayotokea yanatokana na kukosekana kwa uelewa juu ya hatari na madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali hizo”

“Ajali hizo zinaweza kuzuilika endapo wananchi watapatiwa elimu na uelewa wa matumizi au usimamizi sahihi na salama wa kemikali hizo” alisema ndugu Ndiyo.

Akizungumzia ajali hizo, kwa kipindi cha mwaka 2014, ndugu Ndiyo alitoa mfano wa matukio na ajali zipatazo  11 zilizotolewa taarifa ambazo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 14  pamoja na uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo kuungua moto kwa magari na tani zaidi ya  250 za kemikali.

Akizungumzia  hatua za utekelezaji, usimamizi na udhibiti wa wa kemikali ndugu Ndiyo alisema kuwa sheria na kanuni ya kemikali ya mwaka 2015, inaagiza kuwa kila anayehusika na kemikali kwa kuingiza kutoka nje, kusafirisha, kuuza, kusambaza, kutumia au kwa namna yoyote ile ni lazima awe amesajiliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali nchini.

Aidha Ndugu Ndiyo alisema kuwa baada ya kupitishwa kwa sheria na kanuni za kemikali kumekuwa na mafanikio mbali mbali ikiwa ni pamoja na udhibiti wa kemikali zinazoingizwa nchini tangu usafirishaji, utumiaji na hata uteketezaji wake.

“Hatua hii imesaidia kutambua mapema kemikali zinazoingia nchini, mahali zinapokwenda na matumizi yake, hatua ambayo imesaidia kuzuia kemikali hatarishi ambazo zinaweza kuleta madhara kwa watu na mazingira kuingia na kutumika nchini” aliongeza ndugu Ndiyo.

Sheria ya Usimamizi na Udhibiti  wa kemikali za Viwandani na Majumbani  Sura 182  ilitungwa ili kuhakikisha kuwa kemikali zinatumika katika hali iliyo salama bila kuleta athari kwa watu na mazingira.

No comments: