ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 21, 2015

Lowassa ashangiliwa kama Rais, Mbowe anena mazito.

Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa (wa pili kulia), akiwa na viongozi wa Ukawa. Kulia ni Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia. Picha na Dotto Mwaibale

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefichua mazito baada ya kueleza hadharani kuwa kamwe chama chake na washirika wao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawatakubali matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayobainika kuwa yamepikwa.

Kadhalika, alisema ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na mamlaka za serikali iliyopo madarakani kuheshimu maamuzi ya wananchi yatakayotokana na kura watakazopiga kwenye uchaguzi mkuu Jumapili ijayo, kwani kinyume chake ni kuhatarisha amani iliyopo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi wa chama cha National League for Democracy (NLD) aliyefariki dunia wiki iliyopita, Mbowe alisema watakubali matokeo ikiwa mchakato wote wa uchaguzi utakuwa huru, wa haki na usiokuwa na chembe ya mizengwe katika kila hatua.

Chadema na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya Chama cha Wananchi (Cuf), NCCR-Mageuzi na NLD, vimemsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku pia wakishirikiana kusimamisha wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi.

Akieleza zaidi, Mbowe aliyekuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi kuhusu namna walivyojiandaa kupokea matokeo baada ya uchaguzi mkuu Jumapili ijayo, alisema Ukawa itakuwa tayari kupokea matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiwa wataridhika kuwa hatua zote za kisheria na haki za mchakato wa uchaguzi huo kuanzia katika kampeni hadi upigaji kura zimezingatiwa ipasavyo.

Aliongeza kuwa kinyume chake, wao (Ukawa) hawatakuwa tayari kupokea matokeo yatokanayo na hila za namna yoyote ile.

Akifafanua, Mbowe alisema Ukawa haiwezi kukataa matokeo kwa sababu ya kushindwa katika uchaguzi, bali wanachoangalia ni kuzingatiwa kwa haki, sheria na uwazi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo.

“Kupokea matokeo ni mchakato ambao unaanzia katika hatua za kampeni, upigaji kura hadi wakati matokeo yanatangazwa. Siwezi kusema eti tutakataa matokeo kwa sababu tu Nec imetangaza halafu tukaonekana tumeshindwa… la hasha. Bali tutapokea matokeo kama haki, uwazi, sheria na taratibu nyingine zimezingatiwa mpaka kupatikana kwa matokeo,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Sisi Chadema na Ukawa tunaamini kwamba wananchi watamchagua kiongozi wanayemuamini. Lakini kama watu wengine wenye mamlaka ndani ya nchi wakaamua kupindisha sheria na kupindisha maamuzi ya wananchi kupitia sanduku la kura, kamwe hatutakubali matokeo hayo. Na hapo amani tunayoihubiri inaweza kuwa ngumu ‘kui-control’ (kuidhibiti),” alisema.

Kuhusiana na mvutano juu ya wananchi kuondoka vituoni baada ya kupiga kura na siyo kukaa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kura, Mbowe alisema msimao wao wa kulinda kura uko pale pale kwa kuwa wana amini kuwa hiyo ni haki yao kisheria.

“Kura ni mali na kama hivyo ndivyo ni lazima tuilinde, tumepanga kulinda kura zetu kwa amani na utulivu nje ya mita 200 kama sheria inavyosema… tunaomba kila mtu na vyombo vya dola viheshimu,” alisema.

Aliongeza: “Kuhubiri amani bila haki ni kulishana upepo. Mamlaka zote za taifa zina wajibu wa kuheshimu sheria za nchi na kuacha kutumia mamlaka zao vibaya na bila vitisho. Kila mmoja akitekeleza wajibu wake kwa misingi ya sheria, hiyo amani wala haitatafutwa, itapatikana tu.”

Mbali na Mbowe, wengine waliojitokeza katika shughuli ya kuuaga mwili wa Dk. Makaidi ni Lowassa, Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi , Waziri Mkuu Mstaafu aliyehamia kambi ya Ukawa, Frederick Sumaye, Kaimu Katibu Mkuu wa Cuf, Twaha Tasilima, Katibu Mkuu wa NLD, Tozzy Matwanga na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.

Wengine waliokuwapo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee.

MZIRAY
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray na Mwenyekiti wa Chadema Bara, Prof. Abdallah Safari.

Akitoa salamu zake, Mziray alisema viongozi wote wameupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa.
Mbatia alisema Dk. Makaidi alikuwa kiongozi aliyeamini kwenye mageuzi, mabadiliko na kuamini kuwa Tanzania bila CCM inawezekana.

MTOTO WA MAREHEMU
Mtoto wa Marehemu, Oscar Makaidi, alisema baba yake alifariki akiwa katika harakati za kugombania Ubunge Jimbo la Masasi ili kuleta mabadiliko na hivyo akawataka viongozi waliobaki kushirikiana kutimiza ndoto ya marehemu baba yake aliyefariki Oktoba 15 katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi. Dk. Makaidi alizaliwa Masasi, Aprili 10, 1941 na ameacha mjane na watoto kumi.

LOWASSA AITWA RAIS MSIBANI
Baada ya shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya Karimjee, mwili wa Dk. Makaidi ulipelekwa kwenye makaburi ya Sinza na kuzikwa na mamia ya wananchi waliojitokeza.

Katika hatua isiyotarajiwa, baadhi ya wananchi walishindwa kuficha mahaba yao kwa Lowassa katika eneo la makaburi na kujikuta wakimshangilia wakati akiwasili na pia kuondoka, huku wakiimba kwa kumwita ‘Rais, Rais, Rais!’.

Mwili wa marehemu Makaidi uliwasili katika makaburi ya Sinza saa 9:15 alasiri na baada ya kuwasili waombolezaji wengi walianza kumshangilia Lowassa wakati akishuka kutoka kwenye gari alilokuwamo kuelekea katika makaburi hayo, huku naye akiwapungia mkono.

Hata baada ya mazishi, Lowassa alishangiliwa vilevile kwa kuitwa ‘Rais’ wakati akiondoka baada ya yeye na viongozi wa Ukawa wakiwamo Mbowe na Mbatia kuweka maua katika kaburi la Dk. Makaidi.

JAJI MKUU ATAKA MAHAKAMA IACHIWE SUALA LA MITA 200
Wakati Mbowe akisisitiza msimamo wa kuwataka wafuasi wa Ukawa kutorudi nyumbani baada ya kupiga kura na badala yake kukaa umbali wa mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura ili kulinda kura zao, Jaji Mkuu Othman Chande alikataa kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka mahakama iachiwe ili itoe uamuzi wake kwa haki.

Jaji Chande aliyasema hayo jana wakati alipoulizwa na waandishi baada ya kufungua mafunzo kwa majaji na Wasajili Mahakama Kuu Jijini Dar es Salaam, juu ya wajibu wa mahakama katika uchaguzi mkuu na namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika kusimamia kesi za uchaguzi, yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Tayari Mahakama Kuu imeshapanga majaji watatu kushughulikia suala hilo lililoibua mvutano mkali hivi karibuni baina ya viongozi wa Ukawa na wakuu wa Nec na Jeshi la Polisi. Kesi hiyo itaanza kunguruma rasmi leo.

Katika hatua nyingine, Jaji Chande alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wenye mchuano mkali na kwamba mahakama zimejiandaa kumaliza kesi zitakazotokana na uchaguzi huo kabla ya miezi sita inayotajwa kisheria.

Alisema mwaka 2010 kulikuwa na kesi 44 za uchaguzi kwa ngazi za Ubunge na kati yake, 17 zilikwenda hadi hatua ya mwisho baada ya kutolewa ushahidi huku nyingine zikiisha katika hatua za awali.

“Ushindani ni mkali katika uchaguzi huu, tunatarajia kupokea kesi nyingi za uchaguzi. Tumejiandaa kupokea, kusikiliza kwa haraka ili kuwezesha wapigakura kujua mshindi halali ni yupi,” alisema.

Akieleza zaidi, alisema sheria imeweka wazi kuwa anayestahili kufungua kesi siyo mpigakura bali wagombea wenyewe.
Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema wameshirikiana na Ofisi ya Jaji Kiongozi kuandaa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa ni wadau muhimu katika kushughulikia kesi za uchaguzi ili kuwezesha haki kutendeka kwa haraka

GOODLUCK JONATHAN AKIRI NGOMA NZITO CCM, UKAWA
Mkuu wa Jopo la Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola na aliyekuwa Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amekiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu nchini Tanzania una ushindani mkali kutokana na namna vyama vilivyojiandaa lakini akawataka wagombea wote wa nafasi za urais kujiandaa kukubali matokeo kwa maslahi mapana ya taifa lao.

Wagombea wanaochuana kwa karibu ni, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Lowassa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili nchini, Jonathan aliyekubali kuondoka madarakani Mei mwaka huu na kumpisha Muhammad Buhari baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu nchini mwake, alisema katika uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa na hivyo wagombea wajiandae kwa matokeo yoyote ili kuiacha nchi yao ikiwa salama.

Alisema ijapokuwa ushindani ni mkali, Jumuiya ya Madola inaamini kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki na kwamba imani yao kubwa ni Tanzania kusimamia demokrasia iliyokuwapo wakati wote tangu ipatre uhuru wake mwaka 1961.
Jonathan anaongeza jopo lenye waangalizi 14 kutoka mataifa mbalimbali yaliyo wanachama wa Jumuiya ya Madola
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

POLE SANA FAMILI YA MZEE EMANUEL MAKAIDI,POLE SANA WANACHAMA WOTE WA UKAWA,POLESANA WATANZANIA WOTE AMBAO MMEAMUA KWA HIARI YENU BILA KUJALI UWEPO WENU KATIKA ITIKADI TOFAUTI KUIUNGA MKONO UKAWA,HARAKATI ZAKE ZA KUSHIKA DOLA KUPITIA UCHAGUZI MKUU AMBAO UTAFANYIKA NCHINI KOTE SIKU NNE TUU ZIJAZO YAANI JUMAPILI TAREHE 25 OCTOBA 2015.MIMI HIYO JANA NILIKUA MSHIRIKI WA SHUGHULI HII MUHIMU YA KIBINADAMU [SIKUALIKWA,UKINIONA UTASEMA ILISTAHILI],YAANI KUMSINDIKIZA MWENZIO AMBAYE AMEITWA NA MOLA WETU MUUMBA.NILIANZIA KARIMJEE HALL AMBAKO HAPAKUA NA KUULIZWA KADI WALA KIINGILIO NA KISHA KWA USAFIRI WA DALADALA NIKAPANDA GARI YA TEGETA NIKASHUKIA MWENGE NIKAKATISHA KWA MIGUU HADI SINZA MAKABURINI,NILIWAHI MAZISHI.NINACHOTAKA KUSEMA NI KUA NILIIONA HISTORIA YA UMATI,YA HAMASA,YA KUJIANDAA KUPIGA KURA.KWA UJUMLA TUU NISEME, :LOWASSA-MANIA YA LEO TANZANIA MWENYEZI MUNGU PEKEE NDIYE ANAYEJUA VIZURI.NASEMA,MIMI SIWEKI NENO LOLOTE.WATANZANIA TUMTANGULIZE MUNGU JUMAPILI TUIONE SALAMA NA,ATUJAALIE AMANI NA UTULIVU.NAITWA KIUNGWA MILEMETWA.

Anonymous said...

wameona mbali washangiliaji anakuja mheshimiwa lowassa,jiwe kuu la pembeni walilolikataa waashi.ushindi wake katika uchaguzi wa jumapili ni mkubwa mno yaani kama vile uchaguzi wa chama kimoja penye kura ya ndiyo na hapana,pasipo ushindani.ashindane lowassa,atashindana na nani?magufuli keshasema tena mara kadhaa kwamba yeye siyo mwanasiasa na,siasa haijui bali ni mtndaji[wanikanushe].kuna nini hapo tena?kumbuka URAIS NI CHEO CHA JUU CHA SIASA ZA KIRAIA KATIKA NCHI.WANATAKIWA NA WANASHINDANA WANASIASA TUU.lete raha.

Anonymous said...

Kwa ukweli Mbowe hatakubali matokeo ikiwa CCM imeshinda na sababu yake ni kuwa anafikiria atazirudishaje pesa alohongwa kwa ajili ya kampeni - maana walotoa pesa zao wanategemea kitu kutoka kwao - Sasa kama hawajapata Urais watarudishaje deni. @12:57 Kama Lowassa anajiita mwanasiasa basi ni mwizi tuu maana alikuwa CCM alifanya nini esp alivyokuwa Waziri Mkuu? Raisi na Kiongozi bora ni mtendaji na sio msemaji.
MAGUFULI ndio chaguo langu na la watanzania!!!
Nahiyo kuwaambia watu wabaki vituoni eti walinde kura zao ni njia ya kuondosha AMANI- Ni Upumbavu na Ujinga wa UKAWA.

Watanzania wenzangu amkeni - hawa viongozi wote wanaojitia UKAWA washaiba na bado wanataka kuzidi kuiba. Naomba mjiulize huyo mgombea Urais kupita Chadema kwanini anunue njia ya kuingia Ikulu. Chagueni viongozi na sio watawala. Baba wa Taifa alisema mjihadhari na viongozi wanaotumia hela kuingia Ikulu - hizo pesa wamezipata wapi na kama wamekopa jee watazirudishaje.
Amkeni Watanzania wenzangu. Jiulize maswali haya kabla hujapiga kura yako -
Jee Lowassa akiingia Ikulu atafanya nini?
Na alivyokuwa CCM alifanya nini na jee CCM isingemtema angekuwa wapi?
Kwanini wale walomwita Fisadi eti sasa ndio chaguo lao?
Mungu Ibariki Tanzania na Wabariki Watu wake.
Mwenyezi Mungu tujaalia uchaguzi wa AMANI - Amina.
P.S. Tafadhalini msikilizeni Hayati Baba wa Taifa - RIP

https://www.youtube.com/watch?v=6TuNQOm4NFc&feature=youtu.be

https://www.youtube.com/watch?v=fvkWbhmYYxU