Monday, October 26, 2015

Mabomu yatumika kutawanya wananchi Dar ,Tanga

By Herieth Makwetta na Burhani Yakub
Dar es Salaam. Vurugu na mabomu ya machozi yalidumu kwa takribani saa tatu katika eneo linaloizunguka ofisi ya Kata ya Charambe ambako wananchi walikuwa wanasubiria matokeo huku mkoani Tanga polisi walilazimika kuwatimua kwa mabomu wananchi waliokuwa wakishangilia baada ya mgombea wao kushinda. .

Wananchi waliokuwa katika vikundi maeneo ya Magala jana walikusanyika katika ofisi za kata ya Charambe tangu saa tatu asubuhi wakisubiri matokeo.

Kundi hilo kubwa lilizidi kukusanyika na hali iliyosababisha vyombo vya usalama kufika eneo hilo kwa lengo la kulinda usalama.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema kwamba matokeo hayo yamekuwa yakisubiriwa ambapo wameshindwa kuyabandika kwa wakati.

"Tumefika hapa tangu saa tatu lakini Mpaka sasa saa tisa matokeo hayajabandikwa, wanazidi kusogeza muda matokeo hayatangazwi, askari wanatutisha Mara watupige na mabomu tunaendelea kusubiri matokeo hatuondoki," alisema Juma Mohamed.

Wakati hayo yakijiri ndani ya kituo hichohicho mawakala na wasimamizi wa Uchaguzi katika Kata ya Charambe iliyopo mtaa wa Mbagala Rangi 3 walikutwa wakilalamikia mafao yao.

Wasimamizi hao walidai kutolipwa fedha zao za siku tatu tangu waanze zoezi hilo Oktoba 24 mwaka huu.

Mmoja wa mawakala hao Zainat Khatibu alisema wamefanya kazi mfululizo kwa siku tatu bila kupatiwa chakula wala huduma yoyote na kushindwa kulipwa posho zao kwa wakati.

"Hatuna nauli, posho, siku ya tatu Leo tupo kituoni hatujalala wala kula na mpaka Leo matokeo yanatarajiwa kubandikwa na sisi hatujapewa chochote mpaka sasa," alisema Zainat.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Charambe Fikiri Mtemukila alisema suala la mawakala ni tatizo ambalo linatatuliwa kwa kuwapeleka Majimatitu wakapewe malipo yao, huku akizungumzia suala la vurugu za wananchi ni kukosa uvumilivu.

"Wananchi wamekusanyika hapa mapema sana , Kata zote huu ndiyo muda wa kubandika matokeo ila wao wamekuwa wakishinikiza wasubiri muda muafaka," alisema Mtemukila.

Tanga. Askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia(FFU) jana walilazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wakazi wa kata za Dugan a Mwanzange jijini Tanga.

Mwananchi lilishuhudia wakazi wa mtaa wa Magomeni waliokuwa wamekusanyika karibu na ofisi ya Serikali ya mtaa wa Magomeni "B" wakikimbia baada ya kusikika mabomu ya machozi.

Katika kata ya Duga,wananchi walikuwa wamekusanyika kwa vikundi kushangilia ushindi wa Khalid Rashid wa CUF aliyeongoza kwa kupata kura 4465 huku aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo,Kombo Rashid akipata WA CCM akipata kura 4132,Wilison Mulube wa ACT-Wazalendo (104) na Ally Nondo wa ADC (47)

"Inakuwaje wanatupiga mabomu wakati kura tumepiga kwa amani bila kupigana na sheria na hata matokeo yametolewa kwa amani sasa tunashangilia wanatupiga mabomu"alilalamika Salehe Patrick.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,Zubery Mwombeji alilazimika kupeleka askari eneo hilo kwa sababu wananchi waliweka mikusanyiko iliyokuwa ikiwaletea fujo wasimamizi wa uchaguzi kutenda kazi zao kwa hatua za mwisho.

"Tulishatangaza siku tatu kabla kuwa wasikusanyike kwa makundi,lakini wao wamevunja sheria na taratibu za uchgauzi"alisema

Kamanda Mwombeji alisisitiza kuwa wananchi wasikusanyike katika makundu mbalimbali.

MWANANCHI

No comments: