Wakati tukijiandaa kuchagua viongozi wetu kesho, matukio kadhaa yaliyojitokeza katika kipindi cha kampeni za uchaguzi huu yalishangaza wengi na huenda ndiyo mambo yatakayobaki katika kumbukumbu, hata baada ya Uchaguzi Mkuu kupita.
Katika makala haya, nimechagua mambo 10 ambayo kwa maoni yangu yatakumbukwa na Watanzania kwa muda mrefu. Baadhi yakivutia na kufurahisha huku mengine yakiacha vilio na majonzi.
Wanasiasa vigeugeu
Kwa miaka zaidi ya minane, vyama vya upinzani vimekuwa vikimtangaza Edward Lowassa (mgombea urais wa Chadema) kama fisadi, lakini alipotemwa na CCM, vilimchukua kuwa mgombea wake kwa kuwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Frederick Sumaye naye aliyekuwa na ‘sintofahamu’ binafsi na Lowassa, ghafla akajiunga naye.
Kigeugeu kikubwa kilionekana pale wawili hawa, ambao wote ni mawaziri wakuu wastaafu, pamoja na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru waliiponda CCM kama vile hawajawahi kuwa huko na kufanya harakati za kutafuta madaraka wakidai kimeishiwa pumzi, hakijafanya chochote miaka 54 ya uhuru.
Marafiki wakosana
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na katibu wake Dk Willibrod Slaa hawakuwa tu viongozi wakuu wa chama hicho, bali maswahiba wakubwa walioelewana sana.
Hali ilikuwa ni hiyo hiyo kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na katibu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Ujio wa Lowassa ulimaliza uswahiba wa marafiki hao. Dk Slaa pia akatofautiana na swahiba wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima hadi wakafichuliana siri zao. Marafiki wakubwa zaidi waliotofautiana na ambao wengi tutawakumbuka ni Rais Jakaya Kikwete na Lowassa ambaye aliwahi kusema kuwa urafiki wao si wa kukutana barabarani.
Hata jiwe tutachagua
Maneno haya yanaelezea taswira ya uhasama kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka huu. Mashabiki na wanachama wa vyama vya siasa wameonyesha ushindani wa kiwango cha juu kuwahi kutokea. Wanaounga mkono vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamenukuliwa wakisema: “Tutamchagua huyo huyo, hata ingekuwa jiwe tutachagua.”
Kauli hizi na nyingine zimeonyesha wananchi wanaamini mabadiliko ya kweli ni kuiondoa CCM madarakani.
Viongozi wa dini na ushenga
Katika uchaguzi huu tumeona viongozi wa dini wakijiongezea majukumu katika ujenzi wa demokrasia. Askofu Gwajima ndiye aliyetajwa kuwa mshenga wa ‘ndoa ya Chadema na Lowasa.’ Kiongozi huyo wa dini akishirikiana na wenzake wamejitokeza hadharani na kutangaza kuwapo kwao upande wa mabadiliko.
Lowassa kivutio
Hata ukipita uchaguzi huu, tutakuwa na mengi ya kukumbuka kuhusu Lowassa ambaye amekuwa ‘Augustine Mrema’ mpya, lakini yeye ni zaidi ya Mrema.
Mrema alivutia watu kwa hotuba zake kali, Lowassa alivutia watu kutokana zaidi na jinsi wapambe na vyombo vya habari vilivyompamba. Kali zaidi ni kuwa licha ya mgombea huyo kushambuliwa kwa maneno makali kutoka kwa wapinzani wake kisiasa, aliendelea kuwa kimya na kuwavutia maelfu ya wananchi kuhudhuria kwenye mikutano yake. Wengi walianguka na kuzirai.
Vifo vya wagombea
Vifo mfululizo vya wagombea vilitokea katika kipindi cha kampeni wakiwamo mawaziri wawili, Dk Abdallah Kigoda (Waziri wa Viwanda na Biashara) na Celina Kombani (Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais- Utumishi). Wengine ni wenyeviti wawili wa vyama Christopher Mtikila (DP) na Dk Emmanuel Makaidi (NLD). Pia wamo wagombea ubunge ambao ni Deo Filikunjombe (CCM- Ludewa) Estomih Mallah (ACT-Wazalendo- Arusha Mjini) na Mohamed Mtoi ( Chadema-Lushoto).
Vyombo vya habari vya kijamii
Vyombo hivi vilikuwa sehemu muhimu ya kampeni. WhatsApp, Facebook, Twitter na blogs zimefanya kazi kubwa ya kusambaza taarifa mbalimbali. Vilikuwa na ziada ya taarifa kuliko vyombo vikuu vya magazeti, redio na runinga.
Ukitaka kuona video za aibu za wagombea, zipo na utazikuta katika vyombo vya kijamii, Halikadhalika vichekesho, utani, kejeli na mijadala mikali. Naamini mauzo ya ‘data’ katika kampuni za simu yameongezeka na kilele cha mauzo ni katika Uchaguzi Mkuu na siku mbili zinazofuata.
Ujio wa ACT
ACT-Wazalendo iIipozindua rasmi kampeni zake za Uchaguzi Mkuu, hakuna aliyedhani kuwa ingeweza kutoa ushindani mkali dhidi ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa.
ACT-Wazalendo imethibitisha kuwa ina nguvu kubwa baada ya kufaulu kusimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali takribani nchi nzima. Pia, mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira ameonyesha uwezo mkubwa wa kuelezea ilani ya chama chake.
Baadhi ya wachambuzi wanasema bila kuzingatia historia na uzoefu unaowabeba Dk John Magufuli (mgombea urais wa CCM) na Lowassa, katika tathmini huru mgombea wa ACT-Wazalendo angewafunika.
Mita 200
Hili ni jambo lililowashangaza wengi kwa sababu huko nyuma halijawahi kujadiliwa na watu walikaa umbali huo kusubiri matokeo. Inaonekana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mwaka huu imefanya tafakuri na kuja na tafsiri mpya ya sheria zinazoelezea jambo hilo. Upinzani nao unahisi katika hili kuna njama za wizi wa kura.
Uchaguzi unaoangaliwa kwa karibu
Jambo jingine litakalokumbukwa kwenye uchaguzi huu ni kuwa uliteka hisia siyo tu za Watanzania bali hata majirani na jamii ya kimataifa. Waangalizi wa kimataifa wengi wamejitokeza, vyombo vya habari vya kimataifa navyo vimejitokeza kwa wingi kufuatilia uchaguzi huu, huku baadhi, kama BBC wakiamua kurusha matangazo yao kutokea hapa.
Uchaguzi huu ni mtihani kwa Tanzania, kwani katika miaka 10 ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete kumekuwa na migogoro ya nchi jirani na kujaribu kusaidia.
Swali ni je, yenyewe itavuka mtihani huu? Maadui wa Tanzania, baadhi yao ni majirani zetu wanaangalia huku wakiombea tuteleze wapate cha kusema, je, watapata cha kusema? Tusubiri.
MWANANCHI
1 comment:
Mungu ni mwema, watanzania tutavuka salama leo 25 Oct. 2015. Mungu ibariki Tz, Mungu ibariki Africa.
Post a Comment