Moshi. Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 imebisha hodi mjini Moshi baada ya mgombea Udiwani kata ya Soweto, Collins Mayyutta kushitakiwa kwa kosa linaloangukia chini ya sheria hiyo.
Mayyuta amefikishwa kortini leo akishitakiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwenye makundi ya WhatsApp dhidi ya mgombea Udiwani wa kata hiyo ya Soweto kwa tiketi ya CCM, Pamela Shuma.
Ujumbe huo ambao hata hivyo haukuonyeshwa kwenye hati ya mashitaka, ulidai Pamella alipewa kiasi kadhaa cha fedha na mgombea mmojawapo wa ubunge Jimbo la Moshi Mjini ili awape wanawake.
Kwa mujibu wa ujumbe huo ambao pia ulitumwa kwenye mojawapo ya makundi ya Whatsapp, Pamela hakugawa fedha hizo kwa makundi ya wanawake kitendo kichofanya mgombea huyo wa ubunge amweke ndani.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,Joachim Tiganga, wakili wa Serikali Lucy Nkyusa, amedai mshitakiwa alisambaza ujumbe huo wa uongo Oktoba 9 mwaka huu huko Soweto.
imedaiwa kuwa siku hiyo, mshitakiwa alisambaza ujumbe huo wa uongo katika makundi hayo ya WhatsApp huku akijua fika kuwa ni wa uongo na taarifa zake zilikuwa zikiupotosha umma.
Hata hivyo, mshitakiwa amekanusha mashitaka hayo na kupewa dhamana kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh1 milioni.
Hakimu Tiganga aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6 mwaka huu wakati itakapotajwa, baada ya wakili Nkyusa kuijulisha mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo la jinai ulikuwa haujakamilika.
Mayyutta anakuwa mtu wa tatu kushitakiwa chini ya sheria hiyo baada ya washitakiwa wengine wawili kushitakiwa katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam wakituhumiwa kukiuka sheria hiyo.
2 comments:
Hii sheria ililengwa kwa kulinda uchaguzi mkuu subiri upite hatutasikia kitu chochote ndio sera za Tanzania haziko kikatiba na hazifuatwi.
Ni wakati huu tu wa uchaguzi ambapo wambea na waongo ndiyo wanahangaika kusambaza habari zao za uzushi na uongo. Baada ya uchaguzi hutasikia haya yote ndiyo maana hutasikia kesi nyingi zikipelekwa mahakamani. Lakini sheria kama hii ni muhimu sana na siyo Tanzania pekee imepitisha sheria kama hii.
Post a Comment