ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 28, 2015

Nec yamjibu Lowassa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ( Nec), imesisitiza kuwa inatangaza matokeo kwa kadiri inavyopokea na siyo kwa kupendelea upande wowote au kujali aliyeshinda.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva (pichani), alitoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam jana baada ya kutangaza matokeo ya urais katika majimbo 35.

Jaji Lubuva alisema madai yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa wanatangaza matokeo ya maeneo ambayo Chama Cha Mapinduzi kimeshinda ili kuaminisha umma kuwa ni washindi, siyo ya kweli.

"Wakati huu tusingependa kulumbana na chama au vyama vya siasa hata mgombea yeyote, matokeo tunayoyapokea ndiyo tunayatangaza, malalamiko ya kuwa Nec inatangaza kwa mwelekeo wa kupendelea, siyo kweli, tunatangaza bila upendeleo na kujali ameshinda nani," alibainisha.

Alisema siku ya kwanza (juzi), walipokea majimbo matatu na kuyatangaza na kwamba haikuwa rahisi kusubiri majimbo yote ndipo matokeo yatangazwe.

" Tuliahidi kukamilisha kazi hii kwa wakati kwa kutangaza kwa kadiri tunavyopokea, tukitangaza na ikaonekana mgombea fulani anaongoza, ndivyo tunavyoyapokea na hatuwezi kusubiri yote ndiyo tutangaze," alisema.

Aidha, alisema kauli ya kutaka busara itumike, ni wazi kuwa hadi sasa Nec inatumia busara na ndiyo mana matokeo yanatangazwa na wanajitahidi kutimiza ahadi ya kuhakikisha mshindi anafahamika mapema.

Juzi, mMgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya Chadem, NCCR Mageuzi, NLD na CUF, Edward Lowassa, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Nec inatangaza kwa kuanza na maeneo iliyoshinda CCM ili kuaminisha umma kuwa chama hicho kimeshinda na kuwataka kutumia busara na uugwana.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Anaetakiwa kutumia busara ni Lowasa mwenyewe, kwa kutambua kuwa mbinu chafu za kuvuruga uchaguzi sasa hivi ziko hadharani, kadri anavyozidi kujitutumua na kutoa lawama zisizo kuwa na mashiko, ndivyo anavyojivua nguo hadharani.

Anonymous said...

Kutapatapa kwa mfa maji. Huyu bwana ameshajua kuwa urais umeyeyuka na hivyo anakuja na visingizio vya kila aina. Haitamsaidia kwani Watanzania wameshaamua. Tungoje kesho Magufuli atangazwe rasmi halafu wanao taka kusherehekea tusherehekea na baada ya hapo tuendelee na shughuli zetu za kawaida za kujenga nchi yetu. Tulishawaambia kuanzia mwanzo ingawa hawakutaka kusikiliza, sasa mwisho wa Chadema na ndoa yao ya kujikimu ya Ukawa mwisho wake umefika na watawakumbuka Slaa na Lipumba. #Hapa kazi tu.