Aidha, wamebainisha kuwa uchaguzi huo ulikuwa umepangwa vyema na kufanyika kwa amani. Waangalizi hao wamepongeza Watanzania kwa kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikatiba kwa kuwa na uchaguzi wa huru na amani kutawala licha ya kutokea kwa changamoto mbalimbali. Aidha, wamesema kuanzia kipindi chote cha kampeni zilikuwa zenye kusisitiza wajibu wa kila mmoja katika kulinda amani na utulivu nchini na kila mmoja amepiga kura kwa matakwa yake.
Maoni hayo yalitolewa na waangalizi kutoka nchi za Maziwa Makuu (ICGRL), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na Mabunge yao (EP). Akizungumza jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ICGLR, Peter Mositet alisema nchi za Maziwa Makuu ambazo ziko 12, zimepongeza uchaguzi uliofanyika nchini, zikianzia kuwa na kampeni nzuri na kila kitu kilikwenda sawasawa kama ilivyokuwa imepangwa.
Alizitaja nchi hizo za Maziwa Makuu kuwa ni Angola, Burundi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Jamhuri ya Sudan, Sudan Kusini, Zambia na Tanzania. Alisema Watanzania walijitokeza kupiga kura sawasawa, walihesabu kama ilivyostahili na hata matokeo yaliyokuwa yakibandikwa katika vituo yalikwenda kwa kuzingatia sheria pamoja na taratibu nyingine zinazoendelea.
Alisisitiza kuwa yapo masuala kadha wa kadha ya kuangaliwa zaidi ili demokrasia nchini iimarike zaidi kwa kuanzia katika wakati wa kuandikisha idadi ya wapiga kura na hata wakati wa kutolewa kwa matokeo ili yasichukue muda mrefu jambo linaloweza kuharibu morali ya wananchi. Kwa upande wao, waangalizi wa SADC wakiongozwa na Waziri wa Nje na Ushirikiano wa Msumbiji, Oldemiro Julio, walizipongeza Tume za Uchaguzi za Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) licha ya changamoto mbalimbali, lakini taasisi hizo zimeweza kusimamia taaluma na mwishoni kuwaunganisha wapiga kura kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Alisema mbali na kwamba kila waangalizi walioingia nchini walifika kwa nyakati tofauti, lakini wamebaini kuwepo kwa siasa zenye uvumilivu wakati wote wa kampeni, elimu ya uraia kupitia televisheni, redio, na mitandao mbalimbali ya kijamii. Hata hivyo, alisema wakati wa kupiga kura, watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo wazee, walemavu na hata wagonjwa, walipata kipaumbele katika kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao pamoja na kuwepo kwa vifaa kwa ajili ya wasioona.
Kwa upande wao AU, aliyekuwa Rais wa Msumbiiji, Armando Guebuza walipongeza NEC, ZEC, Jeshi la Polisi, vyombo vya habari na wananchi kwa kuwa na uchaguzi uliokuwa salama na huru. Alisema matokeo yanayoendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali, kulingana na nafasi za uongozi walizokuwa wakiwania, yanakwenda vizuri na kwa mujibu wa taratibu na sheria ya uchaguzi na kuwasihi Watanzania kuendelea kuwa wavumilivu kuelekea kukamilisha taratibu zote.
EU katika tathmini yake ya awali, kuhusu mwenendo wa uchaguzi nchini, imebainisha kuwa uchaguzi huo ulikuwa umepangwa vyema na kufanyika kwa amani. Pia timu hiyo, iliyoungana na ya Mabunge ya Nchi za Ulaya (EP), ilisisitiza kuwa imeshuhudia ushindani mkubwa baina ya wagombea hasa upande wa Urais, ikiwa ni pamoja na ushiriki mkubwa wa wananchi katika kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa timu hiyo ya Waangalizi kutoka EU, Judith Sargentini alisema uchaguzi huo kwa kiasi kikubwa umeendeshwa vizuri, ingawa kutokana na upungufu wa uwazi, Tume za Uchaguzi ambazo ni NEC na ZEC, hazikupewa imani kamili na vyama vyote. “Siku ya uchaguzi, hali ilikwenda, watu walijitokeza kwa wingi na kupiga kura kwa utulivu japokuwa kulikuwa na changamoto ndogondogo ziliweza kufanyiwa kazi,” alisema Sargentini.
Alisema timu hiyo ya waangalizi, ilifuatilia taratibu za upigaji kura katika vituo vya kupigia kura 625 kwenye mikoa yote nchini, ambapo uchaguzi huo ulionekana kwenda vyema katika takribani asilimia 96 ya vituo vilivyofanyiwa uangalizi na timu hiyo Tanzania Bara na Zanzibar. Alisema takribani maeneo yote waliyoyafanyia uangalizi, wawakilishi wa vyama vya siasa walikuwemo kwenye vituo hivyo hali iliyochangia kuwepo kwa uwazi na imani juu ya mchakato wa upigaji kura.
“Tathmini ya jumla pia kuhusu utaratibu wa kuhesabu na ufungaji, ilionekana kuwa nzuri sana katika vituo vilivyoangaliwa,” alisema. Alisema EU ilikuwa na waangalizi 141 kwenye mikoa yote nchini na kusisitiza kuwa japokuwa kulikuwa na matatizo madogo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, kilichoonekana kwa ujumla ni mamilioni ya Watanzania kutumia haki yao ya kupiga kura katika mazingira ya amani na kuonesha dhamira ya kuunga mkono mchakato wa demokrasia.
“Waangalizi wa EU walihudhuria zaidi ya shughuli 139 za kampeni nchini kote. Pamoja na mabishano kadhaa kati ya mashabiki wa vyama vinavyopingana, baadhi kwa masikitiko waliishia katika vurugu lakini kwa ujumla, kampeni zilikuwa safi na za kusisimua,” alisisitiza. Kuhusu mifumo ya kisheria, alisema mifumo hiyo inayotawala uchaguzi nchini kote, inatoa msingi mzuri wa uendeshaji wa uchaguzi kidemokrasia ingawa bado kuna baadhi ya mambo ya kisheria hayajafanyiwa kazi tangu uchaguzi uliopita.
“Mambo hayo ni pamoja na kutoruhusiwa kikatiba kwa wagombea binafsi na kutokuweza kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, ambayo hayaendani na misimamo ya kimataifa kwa chaguzi za kidemokrasia,” alisema. Mkuu wa Ujumbe kutoka waangalizi wa EP, Ines Ayala Sender, alisema timu hiyo ilibaini kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa elimu ya uchaguzi hasa katika maeneo ya vijijini.
Pia aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa upande wowote utakaoshindwa kujiandaa kukubali matokeo kwa amani ili kudumisha amani iliyodumu vizazi na vizazi nchini.
HABARAI LEO
No comments:
Post a Comment