ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 3, 2015

NEC yaonya wanaotaka kulinda kura vituoni

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (TUME) imeonya vyama vya siasa, vinavyoshawishi wananchi wabaki katika vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura na kueleza kuwa lengo lao si kwa ajili ya kulinda kura, bali vina agenda ya siri.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema hayo Dar es Salaam jana alipokutana na wanawake na vijana kutoka mikoa mbalimbali. Alibainisha kuwa hatua hiyo itasababisha hofu kwa wapigakura wengine, watakaokuwa wanaenda vituoni kwa kukuta makundi ya watu.

“Tume inashangaa kwa nini vyama vinang’ang’ania kubaki katika vituo vya kupigia kura... inaonekana wana agenda ya siri kwani katika maadili walikubaliana kufuata taratibu zilizokubaliwa,” alisema Jaji Lubuva.

Jaji Lubuva aliwataka wananchi watambue kuwa kama wana nia njema, wasisikilize wanachoambiwa ili kuondoa hofu kwa wapigakura wengine watakaokuwa wanaenda vituoni. Wanawake Alisema wanawake wana nafasi kubwa, kushawishi wanaume na vijana siku ya uchaguzi, kutoshiriki katika vitendo vya vurugu pamoja na kuombea nchi.

Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, ushiriki wa wanawake katika mchakato wa uchaguzi, umekuwa mdogo kutokana na michakato kuanzia katika vyama vya siasa na kuwataka wanawake washiriki katika uchaguzi kuanzia ndani ya vyama, kwani NEC haina mamlaka ya kuteua wagombea.

Jaji Lubuva pia alisema Daftari la Kudumu la Mpigakura, litabandikwa vituoni siku nane kabla ya uchaguzi kama sheria ya uchaguzi inavyotaka. Aidha, alikanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watu kwamba NEC imeshindwa kutoa elimu kwa wapigakura.

Alifafanua kuwa wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa kushirikiana na asasi za kiraia 447, zilizopewa kazi hiyo. Alisema kwa mujibu wa sheria kila mwananchi ana wajibu wa kutoa elimu hiyo kwa mpigakura kwa kushirikiana na Tume.

Daftari wazi Kamishna wa NEC, Profesa Amon Chaligha, akizungumzia uhakiki wa daftari hilo, alisema miaka yote daftari hilo limekuwa likiwekwa wazi kwa mujibu wa sheria, ambayo inataka liwekwe wazi siku nane kabla ya siku ya kupiga kura.

“Siku bado nyingi...zikifika wanaweza kulaumu lakini bado hivyo hakuna sababu ya kulalamika kwani siku zikifika tutabandika vituoni na kuwekwa wazi kwani sasa vitabu vinaendelea kuchapishwa huku vingine vikianza kupelekwa mikoani,” alisema.

Alisema siku watakapokutana na vyama vya siasa, watawapa ‘soft copy’ ya daftari hilo, kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka yote. Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Emmanuel Kawishe, alisema mgombea ubunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani Mtwara, Abdallah Chikota (CCM) pekee ndiye amepita bila kupingwa na atatangazwa mshindi siku ya kupiga kura.

Vijana Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahamoud Hamid alisema vijana ni sehemu muhimu katika mchakato wa uchaguzi, hivyo wasikubali kutumika vibaya kuchochea na kusababisha fujo kwa maslahi ya wanasiasa wachache.

“Vijana wamekuwa wakitumika vibaya hasa wakati huu wa uchaguzi kuchochea na kusababisha fujo, NEC tunawaomba msikubali kutumika kwa maslahi ya wanasiasa wachache,” alisema.

Aliwaasa vijana kutumia uwezo, taaluma na utashi walionao kutoa elimu kwa makundi yote ya vijana kwani wakati huu wa uchaguzi mwamko wa mabadiliko na watu kudai haki umekuwa mkubwa hivyo kuna hatari kwa vijana kutumika vibaya.

“Vijana ni daraja muhimu katika utoaji wa elimu, msikubali kijana hata mmoja ashiriki kutoa taarifa zisizo na maslahi kwa Taifa kwa maslahi ya makundi fulani, bali mhakikishe uchaguzi unakuwa salama,” alisema.

HABARI LEO

5 comments:

Anonymous said...

unajua jaji mstaafu damian lubuva mwenyekiti wa tume kuna nyakati nashindwa kukuelewa iwapo kweli una malengo ya kutaka haki itendeke kwenye uchaguzi huu wiki tatu zijazo.kulinda kura zetu tulizopiga wenyewe unasema tuna agenda ya siri,ni siri ipi hiyo muheshimiwa jaji.jee una kichwa cha panzi umesahau yale uliyotamka awali kwamba matokeo ya kura kwa ngazi zote yaani urais,ubunge na udiwani yatabandikwa vituoni sasa kama yanabandikwa anabandikiwa nani asome?bundi au kunguru wanaolala kwenye miti.maana ya kubandika matokeo ni kuniwezesha mimi niliyepiga kura niyasome,niupime mwelekeo wa kura yangu kisiasa.sasa jaji lubuva hutaki nisubirie.nasema,wewe ndio mwenye agenda ya siri umepanga na uliopanga nao kutuibia kura.kusubiri na fujo wapi na wapi?tunaomba usichochee mtafaruku.acha.aliyekutuma mwambie umegonga mwamba.TUTAPIGA KURA,TUTAYASUBIRIA MATOKEO,TUTASHANGILIA KWA NGUVU,KITUO KWA KITUO.HAPA TUTAKUWA TORRERANCE ZERO,HEBU MTUPISHE,LOWASSA KIDEDEA,DUME LA MADUME.WAKIKEREKWA WATAFUNE MAWE!

Anonymous said...

Mwaka huu ni lazima kukesha ili kulinda kura maana tume yote imeteuliwa na CCM..hebu fikiri tume yote ingekuwa imeteuliwa na chadema unafikiri CCM wangekubali kwenda nyumbani baada ya kupiga kura????

Anonymous said...

Mkeshe au msikeshe, matokeo hayatabadilika. Ndoto ya UKAWA ya kushika dola kwa kuwatumia makada fisadi wakuu wa CCM ni ndoto inayoongozwa na uendawazimu au uvivu wa kufikiri uliokithiri!

Anonymous said...

Wapiga kura wakishamaliza kupiga kura zao lazima waondoka wapende au wasipende na hawa wanaoshabikia kulundikana vituoni wastake kutuleta kasheshe zao. Lubuva na vyombo vyote vya usalama tunaomba mlizingatie hili. Mmeshaona wapi watu wanapiga kura halafu wanakaa vituoni muda wote wakisubiri kura zikihesabiwa. Wanataka wakae makundi yao ya umbeya ili waogopeshe watu wasiotaka shari kwenda kupiga kura zao! Kuna vyama vinane vinawagombea urais na karibu vyama vingine vyote vinawagombea ubunge na udiwani sasa kila chama kikitaka wanachama wake kubaki vituoni baada ya kupiga kura kweli kutakuwa na amani hapo. Tayari kuna watu wengine wameshaanza kuonyesha dalili za kuwa na jazba kweli mahali hapo patakuwa na usalama! Pamoja na haya yote mpangilio na utaratibu wa upigaji kura ni kuwa wapiga kura wataingia na kutoka mara wapigapo kura zao kutokana na ukweli kuwa vituo vyenyewe huwa na nafasi kidogo. Kwa mantiki hii nafasi kubwa itatoka wapi itakayoweza kuhimili msongamano utakao jitokeza ikiwa kila mpiga kura ataamua kubakia kituoni. Hili siyo jambo la masihara na wote tunaopenda amani na usalama wetu lazima tulitilie maanani ili isije ikawa majuto ni mjukuu.