MWENYEKITI wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA), Musa Kisoky amesema wanawasiliana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuona namna ya kumsaidia beki wa Mbeya City, Juma Said ‘Nyosso’(pichani juu) aliyefungiwa miaka miwili pamoja na faini ya Sh milioni mbili baada ya kumdhalilisha John Bocco wa Azam FC.
Kisoky amekiri kuwa adhabu aliyopewa Nyosso ni sawa kulingana na Kanuni za Ligi Kuu msimu wa 2015-16 ila mchezaji huyo hakupewa nafasi ya kusikilizwa na wanaomba adhabu ipunguzwe na wao watamtafutia wataalamu wa saikolojia wakae naye ili wamsaidie.
“Adhabu imetokana na Kanuni na Sheria zilizopo za TFF, na Kanuni hiyo ipo wazi inasema mchezaji atakayekutwa na kosa la udhalilishaji kuna kufungiwa mechi tatu mpaka kumi, faini ya milioni moja mpaka tatu, kufungiwa mwaka mmoja mpaka miwili na inategemea huyo anayehukumu anatoa hukumu gani.
“Lakini sisi kwetu tunasema kila siku mpira ni nidhamu, na nidhamu inatakiwa iwepo na unapocheza kwa nidhamu utacheza mpira bila matatizo yoyote. Adhabu hii kikanuni ipo sawa lakini Nyosso ameomba msaada wa chama,” alifafanua Mwenyekiti huyo wa Sputanza.
Pia Kisoky amekiri kuiona video na picha ya mnato ya tukio hilo, lakini Nyosso hajapewa nafasi ya kusikilizwa, na kufafanua kuwa mara nyingi unaweza kuhukumiwa kwa kuangalia na chanzo kilikuwa nini.
Hivyo alisema ukiangalia video hii inaonekana na John Bocco alikuwa na matatizo kwani alimgonga kwenye ugoko Nyosso mara mbili pia akajaribu kumsukuma kwa kiwiko. Kisoky alisema kwenye picha inabidi iangaliwe Bocco kafanya makosa na Nyosso kafanya makosa ila kwa kuwa Sputanza ni chama chao wachezaji, wana haki pia wamelaani hicho kitendo, lakini wana haki ya kuweza kujaribu kutazama wanamsaidiaje pamoja na TFF waone hali halisi kabla ya tukio kutokea.
Nyosso amefungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa muda wa miaka miwili huku akitakiwa kulipa faini ya 2,000,000 kwa kosa la kumdhalilisha Bocco kwenye mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita Chamazi, Dar es Salaam Nyosso amejitetea kwa kuitaka Sputanza kumsaidia katika kupata haki yake.
Beki huyo wa zamani wa Ashanti, Simba na Taifa Stars alimtomasa matako mshambuliaji nyota wa Azam FC, Bocco, tukio ambalo halikuonwa na mwamuzi, lakini Bocco aliliripoti na picha kunaswa na wapigapicha.
Nyosso alikiomba chama hicho kufuatilia suala hilo kwa madai hakutenda kosa hilo, akiamini kitafuatilia kwa kina na hatimaye haki kutendeka. Alidai hakumbuki kama alifanya kosa hilo na anaona kuna nafasi ya kusikilizwa. Hii si mara ya kwanza kwa Nyosso kuadhibiwa na TFF kutokana na kosa kama hilo.
Mapema mwaka huu, alifungiwa mechi nane baada ya kumfanyia kitendo kama hicho aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Elias Maguli.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment